Dodoma. Serikali imepiga marufuku maofisa uvuvi katika halmashauri kutoza tozo na kudai leseni kwa watu wanaosafirisha samaki chini ya kilo 30.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema hayo leo Mei 8, 2024 alipojibu maswali ya nyongeza ya mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira.
Mbunge huyo amesema kumekuwa na utozaji tofauti wa tozo katika kila halmashauri na kuhoji iwapo Serikali iko tayari kutoa mwongozo kuziwezesha halmashauri kutoza tozo inayofanana.
Lugangira pia amesema kanuni ya usafirishaji samaki ya mwaka 2020 imetoa msamaha wa kodi kwa wavuvi wanasafirisha samaki chini ya kilo 30.
Amesema hivi sasa halmashauri zinatoza tozo na kutaka leseni, hivyo amehoji Serikali iko tayari kutoa mwongozo ili halmashauri hizo zisitoze tozo hiyo?
Naibu Waziri Mnyeti amesema kanuni hizo hupangwa na halmashauri zenyewe kwa sheria na kanuni ndogo-ndogo.
“Wao wanaangalia kutokana na mazingira yao ya wavuvi na wanazipeleka Tamisemi na kupitisha kanuni hizo kama zinakubalika. Sisi tunachofanya ni kutoa mwongozo kuhakikisha kanuni hizo hazivunji sheria mama na sheria ya uvuvi,” amesema.
Amesema wataenda kukaa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kupitia kanuni hizo na iwapo zina changamoto ya kimazingira watazifanyia marekebisho.
Mnyeti amesema wizara itafuatilia kuona kama kuna mwananchi anatozwa tozo kwa kubeba kilo 30 za samaki kwa kuwa sheria inakataza kutozwa kwa uzito chini ya kilo 30 kwa sababu hizo ni kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
“Kama kuna halmashauri inakatisha tozo, kama kuna wananchi wanasumbuliwa, nitoe rai kwa maofisa uvuvi kuacha kuwatowa faini au tozo wananchi kwa kuwa wako ndani ya sheria inayotaka samaki chini ya kilo 30 zisitozwe kodi,” amesema.
Katika swali la msingi Lugangira amehoji ni nini mkakati wa Serikali katika kupunguza baadhi ya tozo na kufuta zingine ili kuleta nafuu kwa wavuvi.
Naibu Waziri Mnyeti amesema mwaka 2020 na mwaka 2022 Serikali ilifanya maboresho ya tozo mbalimbali, hivyo baadhi ya leseni kuunganishwa na tozo nyingine kupunguzwa.
“Tozo ambazo zilipunguzwa ni ushuru wa zao la dagaa wanaozalishwa Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Bahari ya Hindi kutoka Dola za Marekani 0.16 hadi kufikia Dola za Marekani 0.1 kwa kilo na tozo ya dagaa wa Ziwa Tanganyika kutoka Dola Marekani 0.5 hadi kufikia Dola 0.3 kwa kilo,” amesema.
Amesema gharama za tozo ya kusafirisha minofu ya samaki ya sangara nje ya nchi ilipunguzwa kutoka Dola za 0.2 za Marekani nhadi kufikia Dola 0.1 kwa kilo.
Naibu waziri amesema Serikali imepunguza ushuru wa uingizaji mazao ya bahari nchini kutoka Dola 2.5 za Marekani hadi kufikia Dola 0.5 kwa kilo kwa mazao ya ngisi, pweza na kaa.
Mnyeti amesema maeneo mengine ambayo yamefanyiwa maboresho ni kupunguza gharama ya ada za leseni za kusafirisha dagaa kutoka Dola 1,000 hadi kufikia Dola 250 kwa dagaa wa maji chumvi na maji baridi.
“Wizara itaendelea kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi nchini kadiri itakavyowezekana na kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi nchini,” amesema.