Dodoma. Serikali katika mwaka wa fedha 2024/25 imetenga Sh252.70 bilioni kwa ajili ya kuwalipa watumishi 219,924 waliokasimiwa kupandishwa vyeo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema hayo leo Mei 8, 2024 alipojibu swali la mbunge wa Lupembe, Edwin Enosy.
Amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuboresha masilahi ya watumishi wa umma nchini.
Ridhiwani amesema Serikali imeendelea kutekeleza hatua na afua mbalimbali za kuboresha masilahi ya watumishi wa umma.
Akitaja baadhi ya mikakati amesema Julai, 2022 Serikali iliongeza kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.
Naibu waziri huyo amesema Serikali imeweka nyongeza ya mwaka ya mishahara, akieleza Sh153.92 bilioni zimetengwa katika mwaka wa fedha 2023/24 na Sh150.87 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 ili kugharamia nyongeza ya mwaka ya mishahara.
“Serikali imehuisha viwango vya malipo ya posho ya safari za kikazi ndani ya nchi na posho ya saa ya ziada kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa umma kumudu gharama za maisha kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi,” amesema.
Ridhiwani amesema Serikali pia imerejesha utaratibu wa kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki kila baada ya miaka mitatu badala ya miaka minne kuanzia mwaka huu wa fedha.
“Kwa msingi wa uamuzi huo, Serikali inaendelea na zoezi la kuwapandisha vyeo watumishi 81,515 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 kwa gharama ya Sh130.47 bilioni kwa mwaka na watumishi wengine 219,924 wamekasimiwa kupandishwa vyeo katika ikama na bajeti ya mwaka 2024/25 kwa gharama ya Sh252.70 bilioni kwa mwaka,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea na ulipaji wa madai ya malimbikizo ya mishahara akieleza madai ya watumishi wa umma 26,331 yenye jumla ya Sh39.05 bilioni kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika na taasisi za umma yamehakikiwa na kulipwa kwa watumishi stahiki.
Naibu waziri amesema Serikali imeridhia kulipa mishahara ya wafanyakazi wa mamlaka za Serikali za mitaa 113 zilizopo nchini zenye jumla ya watumishi 691 kwa awamu.
“Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha masilahi ya watumishi wa umma ikiwemo, kutenga fedha katika bajeti kwa ajili ya kugharimia nyongeza ya mishahara ya kila mwaka, posho na marupurupu kwa watumishi kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu ili kuongeza motisha na chachu ya uwajibikaji,” amesema.