Shekilango alivyofariki katikati ya misheni maalumu Uganda

Dar es Saalam. Miaka 44 imetimia tangu kufariki kwa kiongozi Mtanzania, Hussein Shekilango ambaye barabara maarufu ya Shekilango ilipewa jina hilo kwa heshima yake.

Ilikuwa Jumapili ya Mei 11, 1980, Tanzania ilipompoteza waziri wake, Shekilango katika ajali ya ndege iliyotokea Arusha. Shekilango alikuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Korogwe Mjini (1975 – 1980).

Jumapili ya Novemba 9, 1975, mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo, Rais Julius Nyerere alitangaza Baraza jipya la Mawaziri lililokuwa na wizara mbili mpya ambazo ni Wizara ya Sheria na Wizara ya Mipango ya Utumishi.

Pia, alifanya marekebisho ya muundo wa wizara za zamani ambayo yalisababisha kuwepo kwa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Maji, Umeme na Madini, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Biashara. Miongoni mwa walioingia katika baraza hilo ni Shekilango, alipoteuliwa kuwa Waziri Katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Baraza hilo lilikuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe, Rashidi Kawawa (Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais), Amir Jamal (Fedha na Mipango), Ibrahim Kaduma (Mambo ya Nchi za Nje), Ali Hassan Mwinyi (Mambo ya Ndani), Edward Sokoine (Ulinzi), Julie Manning (Sheria) na John Malecela (Kilimo).

Wengine ni Cleopa Msuya (Viwanda), Alphonse Rulegura (Biashara), Wilbert Chagula (Maji, Umeme na Madini), Alfred Tandau (Mawasiliano), Nicolas Kuhanga (Mipango ya Utumishi), Isael (Israel) Elinawinga (Elimu), Leader Stirling (Afya) na Mrisho Sarakikya (Utamaduni na Vijana).

Wengine ni Daudi Mwakawago (Habari na Utangazaji), Solomoni Saibul (Maliasili na Utalii), Thabita Siwale (Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini), Crispin Tungaraza (Kazi na Ustawi wa Jamii), Louis Sazia (Ujenzi), Hasnu Makame (Ofisi ya Rais–Ustawishaji wa Makao Makuu), Peter Siyovelwa (Ofisi ya Rais).

Mawaziri wadogo walioteuliwa katika baraza hilo ni Isaac Sepetu (Mambo ya Nchi za Nje), Seif Bakari (Ulinzi), Edward Barongo (Kilimo), Chrisant Mzindakaya (Viwanda), Nazar Nyoni (Elimu), Mustafa Nyang’anyi (Afya), Robert Ng’itu (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Ali Mchumo (Ofisi ya Waziri).

Februari 13, 1977 Rais Nyerere alifanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri na kumpandisha cheo Waziri wa Ulinzi, Edward Sokoine kuwa Waziri Mkuu kuchukua nafasi ya Rashidi Kawawa.

Katika mabadiliko hayo, mawaziri wapya wanane waliteuliwa na saba waliondolewa kwenye Baraza la Mawaziri. Mawaziri saba walibadilisha nyadhifa zao, lakini Shekilango alibaki katika nafasi ileile ya awali.

Mwaka 1978 vilipozuka vita vya Kagera, vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vilihitimisha utawala wa aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Uganda, Idi Amin, na kukabidhi madaraka kwa Profesa Yusufu Lule kama Rais wa mpito wa nchi hiyo.

Hata hivyo, urais wa Profesa Lule ulidumu kwa siku 68 tu tangu Aprili 13 hadi Juni 20, 1979. Kosa lake kubwa ni kutolitii Baraza la Ushauri la Taifa (NCC). Alikuwa akiteua mawaziri na manaibu waziri bila kushauriana na baraza hilo. Kwa maana hiyo, Lule akawa ni Rais aliyeitawala Uganda kwa muda mfupi zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Baada ya Lule kuondolewa madarakani usiku wa manane, kwa mara nyingine Uganda ikawa haina rais. Majina matatu yalipendekezwa—Paulo Muwanga, Edward Rugumayo na Godfrey Binaisa. Hatimaye Binaisa alikabidhiwa madaraka.

Wakati Binaisa akifurahia kuchaguliwa na NCC kuwa Rais wa Uganda huku akiwa amejificha kwenye hoteli ya Nile Mansions, Redio Uganda, mchana wa Jumatano ya Juni 20, 1979, ilitangaza kuwa raia wa nchi hiyo walianza kukusanyika mitaani kupinga urais wake.

Hadi kufikia jioni kuelekea usiku mitaa ya Kampala ilikuwa imejaa watu waliokuwa wakiimba “Tunamtaka Lule. Tunamtaka Lule”. Usiku kucha raia walizidi kumiminika mitaani. Kelele zilizidi kiasi kwamba Binaisa alishindwa kupata usingizi.

Majeshi ya Tanzania yaliingia Kampala kujaribu kuleta hali ya utulivu, lakini wengine walirushiwa mawe. Wakati huu, Profesa Lule alikuwa amezuiliwa kwenye Ikulu ya Entebbe ambako alikuwa akipatiwa tu taarifa za maandamano. Hii ilimfanya aendelee kudai kuwa yeye ni Rais halali wa Uganda.

Wafanyakazi na wafanyabiashara wengi mjini Kampala waligoma. Lakini Waziri wa Ulinzi, Yoweri Museveni, akaenda kwenye studio za Redio Uganda na kupiga marufuku maandamano yoyote. Waandamanaji waliondoka mitaani, lakini biashara zilisimama.

Binaisa na Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, wakalazimika kufikiria namna ya kushughulika na tatizo la Lule. Kwa kuwa bado Lule alikuwa akidai kuwa yeye ni Rais wa Uganda, na huku Uganda ikiwa na Rais mwingine, basi hakupaswa kuendelea kubaki Uganda. Aliitwa na Mwalimu Nyerere kwenda Dar es Salaam.

Lule alisafiri kwenda Dar es Salaam akisindikizwa na mmoja wa viongozi wa NCC, Dani Wadada Nabudere. Kwa mujibu wa kitabu “UPC and National-Democratic Liberation in Uganda” cha Yoga Adhola, Lule alipokewa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Rashid Kawawa na katibu wa Rais, Joseph Butiku na kupelekwa Ikulu.

Kibao kinachoonyesha eneo la Shekilango lilopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Asubuhi iliyofuata, Nyerere alifika kumwona na kuongea naye. Alimwambia alipata taarifa za kutatanisha kutoka Entebbe, nyingine zikisema Lule amejiuzulu kwa hiari yake na nyingine zikidai amelazimishwa. Nyerere alimtaka amwambie ukweli ni upi. Lule alimjibu Nyerere kuwa hakuja Dar es Salaam kujadili masuala hayo.

Msaidizi wa Lule, James Senabulya, kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na Ssemujju Ibrahim Nganda na kuchapishwa kwenye gazeti ‘The Observer’ la Agosti 10, 2009, Nyerere alimpelekea Lule waraka na kumwambia “weka saini hapa kuwa umeng’atuka urais wa Uganda kwa sababu kwa sasa tuna Rais mwingine.”

Lule aligoma. Lakini aliendelea kubaki Dar es Salaam kwa siku kadhaa. Siku chache baadaye Nyerere, au wajumbe wake, alimwendea tena Lule na kutaka kujua kama ameshabadili mawazo. Lule aligoma. Lakini Nyerere alimtembelea tena Lule mara kadhaa.

Wakati mmoja akamuuliza Lule swali: “Unadhani bado wewe ni Rais halali wa Uganda?” Hii ilimkera Lule. Nabudere akamwambia Lule aache kuendelea kulalamika. Lule akasema dhamira yake inamsuta na kwamba alitaka Uganda kuwe na kura ya maoni.

Nabudere akamwambia kwa hali ya ghasia iliyoko Uganda, hilo la kura ya maoni haliwezekani. Akamwambia kuwa kama atatoa kauli ya kumuunga mkono Binaisa, hakutakuwa na shida yeye kurejea Uganda. Nyerere alianza kumwona Lule kama mkaidi.

Baadaye Nyerere akasema kama Lule hatakana kauli yake ya kwamba yeye ni Rais wa Uganda, hataruhusiwa kuondoka Dar es Salaam.

Vuguvugu la vita vya Uganda na Tanzania lilipomalizika na hali ya Uganda kuwa ngumu, ndipo Hussein Shekilango alitumwa na Rais Nyerere kwenda kuweka mambo sawa na kuisimamia serikali mpya ya mpito ya Uganda akisaidiwa na Balozi Faraji Kilumanga.

Shekilango alikabidhiwa jukumu maalumu la kuwa mratibu kati ya serikali ya Uganda na Tanzania baada ya kumalizika vita hivyo na kutuliza hali ya ghasia iliyokuwa Uganda.

Akiwa nchini Uganda, Shekilango na Balozi Kilumanga walipanga kukutana na Mwalimu Nyerere mjini Arusha ambako alikuwa kwenye ziara ya kiserikali ili kumpa mrejesho wa mtafaruku uliokuwa ukiendelea nchini Uganda kati ya Rais Binaisa na Kiongozi wa Jeshi la Uganda, Jenerali David Oyite Ojok.

Asubuhi ya Alhamisi ya Aprili 24, 1980, Redio Uganda ikatangaza kuwa Binaisa amemsimamisha kazi Jenerali Ojok na kumteua kuwa Balozi wa Uganda nchini Algeria. Huu ndio ukawa mwanzo wa mwisho wa Binaisa.

Maofisa wa serikali walianza kutekwa. Binaisa mwenyewe alikuwa Ikulu ya Entebbe akiogopa hata kutoka. Mawasiliano yake yote yalikatwa isipokuwa simu ambayo aliitumia kuwapigia waandishi wa habari waliokuwa Kampala akiwaambia kuwa yeye bado ni Rais wa Uganda.

Museveni, Muwanga na Ojok wakaanza kushirikiana kummaliza Binaisa. Tume ya Kijeshi ikaanza utaratibu wa kumwondoa Binaisa madarakani. Tume hiyo ingeweza kuzuiwa tu na JWTZ.

Katikati ya usuluhisi wa migogoro yote hiyo alikuwako Hussein Shekilango. Lakini mapema Jumapili, Mei 11, 1980, Shekilango aliongoza msafara wa maofisa wa serikali ya Tanzania uliokuwa ukitoka Uganda kuelekea Arusha kwa ndege ndogo aina ya Casena 402 yenye uwezo wa kubeba abiria wanane.

Siku hiyo ndege ya JWTZ ilipata ajali na kuanguka katika Kijiji cha Engwiki, wilayani Monduli Mkoa wa Arusha. Ililipuka baada ya kugonga kilima cha Komoloniki ilipokuwa ikielekea Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Askari wa Chuo cha Uongozi wa Kijeshi Monduli na wananchi wa kijiji cha Engwiki walitumia saa tano kutafuta na kukusanya mabaki ya miili ya abiria wa ndege hiyo.

Abiria waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na Shekilango, Balozi Faraji Kilumanga ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda na msaidizi mkuu wa Shekilango, Faraji Iddi Msechu; askari wa JWTZ, Koplo Petro Kalegi Magunda, Private Stephen Mlawa, Luteni Mally na Luteni Luoga.

Siku moja baadaye, Jumatatu ya Mei 12, 1980, Godfrey Binaisa aliondolewa kwenye kiti chake cha urais wa Uganda na shughuli zote za urais zikasimamiwa na Tume ya Kijeshi chini ya uenyekiti wa Paulo Muwanga na makamu wake, Yoweri Museveni. Uongozi wa Muwanga na Museveni uliongoza shughuli hizo kwa siku 10—kuanzia Mei 12 hadi Mei 22, 1980.

Kuanzia Mei 22 Tume ya Kijeshi ilikabidhi madaraka yake kwa Tume ya Rais ambayo ilisimamia kazi hiyo kuanzia hapo Desemba 15, 1980 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu nchini humo na matokeo kutangazwa.

Uchaguzi Mkuu uliitishwa na kufanyika Jumatano ya Desemba 10, 1980 na chama cha Uganda People’s Congress (UPC) cha Milton Obote kilitangazwa kushinda uchaguzi huo na Obote kurejea madarakani kama Rais wa Uganda kwa mara ya pili. Waangalizi wa kimataifa walisema uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki.

Wakati hayo yakiendelea, Waziri Shekilango alizikwa Jitengeni, Mombo, Korogwe mkoani Tanga. Wakati wa kifo chake ujenzi wa barabara ya Sinza ndio ulikuwa umeanza. Katika kumuenzi Shekilango, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam uliipa barabara hiyo jina lake.

Related Posts