LICHA ya nidhamu bora ya uzuiaji kwa Kagera Sugar ila imeshindwa kuizuia Yanga hadi dakika za mwisho baada ya kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Bao la Yanga katika mchezo huo limefungwa na kiungo, Mudathir Yahya dakika ya 82 likiwa ni la tisa kwake katika Ligi Kuu Bara msimu huu akimfikia nyota wenzake, Maxi Mpia Nzengeli.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Februari 2, mwaka huu uliisha kwa suluhu.
Mechi ya mwisho baina ya timu hiziĀ msimu uliopita, Aprili 11 mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga ilishinda mabao 5-0, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI aliyefunga matatu ‘Hat-Trick’, huku nyota wa zamani wa kikosi hicho, Fiston Mayele na Bernard Morrison wakifunga moja kila mmoja wao.
Mchezo wa mwisho kwa Kagera Sugar kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara ulikuwa ni mabao 3-0, ikiwa chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Luc Eymael kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Januari 15, 2020.
Tangu mwaka huo Kagera imecheza michezo tisa mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kuonja ladha ya ushindi dhidi ya Yanga na kati ya hiyo imepoteza saba na kutoka sare miwili.
Mchezo uliozalisha mabao mengi baina ya timu hizi Yanga ilishinda mabao 6-2, Oktoba 22, 2016 kwenye Uwanja wa Kaitaba huku ikishuhudiwa viongozi wa Kagera wakiwasimamisha nyota wawili wa timu hiyo kipa, Hussein Shariff ‘Casillas’ na beki, Erick Kyaruzi kwa kile kilichoelezwa kuihujumu.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Obrey Chirwa na Donald Ngoma waliofunga mawili kila mmoja, huku Simon Msuva na Deus Kaseke wakifunga moja kila mmoja na ya Kagera Sugar yalifungwa na Mbaraka Yusuph.
Yanga imeendeleza rekodi nzuri katika Ligi Kuu Bara inapocheza ikiwa uwanja wa nyumbani kwa sababu haijawahi kupoteza au kutoka sare tangu msimu huu wa 2023/2024 umeanza.
Huu unakuwa ni mchezo wa 13 kwa Yanga ikiwa mwenyeji na kati ya hiyo imeshinda yote sawa na kukusanya pointi 39 na imefunga jumla ya mabao 33 na kuruhusu matano tu.
Kwa upande wa michezo mingine 13 iliyocheza ya ugeniniĀ msimu huu, Yanga imeshinda tisa, sare miwili na kupoteza pia miwili na kati ya hiyo imefunga mabao 24 na kuruhusu saba sawa na kukusanya jumla ya pointi zake 29.
Ushindi huu unaifanya Yanga kufikisha pointi 68 katika michezo 26 iliyocheza, hivyo inahitaji pointi tano tu ili kufikisha 73 zitakazowapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa jumla tangu mwaka 1965 na kwa sababu hazitaweza kufikiwa na timu yoyote.
Iko hivi, Azam FC inayoshika nafasi ya pili na pointi 57 hata ikishinda michezo yake yote mitano iliyobakia itafikisha pointi 72, huku Simba inayoshika nafasi ya tatu na pointi 53 ikishinda mechi zake zote sita zilizobakia itamaliza msimu huu na pointi 71.
Kagera inafikisha michezo 26 ya Ligi Kuu Bara msimu huu na kati ya hiyo imeshinda sita, sare 12 na kupoteza minane ikiwa nafasi ya saba na pointi 30.
@Tanzanite Negrito