TAS yataka juhudi za pamoja kukabili unyanyapaa, ukatili

Dar es Salaam. Tukio la kujeruhiwa mtoto mwenye ualbino mkoani Geita limekiibua Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), kikiikumbusha Serikali na mamlaka husika kuhusu uhitaji wa juhudi za pamoja za kukabiliana na unyanyapaa na ukatili.

TAS imesema juhudi hizo ni pamoja na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kumalizia haraka mchakato wa upitishwaji rasimu ya mpango kazi wa Taifa kwa watu wenye ualbino wa mwaka 2023/24 – 2027/28 ili hatua za utekelezaji zifuate.

Mei 4, 2024 saa mbili usiku mkoani Geita limeripotiwa tukio la mtoto Julius Kazungu (10) mwenye ualbino kunusurika kifo, baada ya kushambuliwa na mtu asiyejulikana kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2024 Mratibu wa dawati la watetezi wenye ulemavu katika Mtandano wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Perpetua Senkoro amesema wamesikitishwa na kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo kueleza uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo halikuwa na dhamira ya kumkata viungo muhusika.

“Tunaamini Jeshi la Polisi ndilo walinzi wetu lakini tumeshangazwa na kauli ya kamanda, ndiyo kwanza uchunguzi umeanza hata kabla hawajamkamata mtuhumiwa tayari wameshajua dhamira yake hakutaka kiungo,” amesema Senkoro.

Amesema kumekuwa na matukio mengi ambayo yametokea lakini changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa ushahidi ili hukumu ya kesi iweze kutolewa.

Mwenyekiti wa TAS, Abdillah Omary amesema wanatoa wito kwa mamlaka husika kuharakisha uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.

“Wakati wanaendelea na uchunguzi tunaisihi Serikali na vyombo vya usalama kuimarisha usalama kwa familia ya mtoto Kazungu pamoja na watu wenye ualbino nchini,” amesema Omary.

Akizungumzia kujeruhiwa mtoto huyo, Kamanda Jongo alithibitisha tukio hilo na kueleza uchunguzi wa awali unaonyesha ni tukio la kupanga ili kuzua taharuki kuwa watu wenye ualbino hawako salama.

“Tunasema hivi kwa sababu kuna watu wameenda kumhoji mama lakini wameeleza taarifa tofauti na waliyopewa, wanasema mtoto amejeruhiwa akiwa ndani na nia ilikua kuondoka na mkono wa kulia, lakini hizi ni taarifa za uongo na inaonyesha hawa watu walikuwa wanatengeneza stori kuonyesha wenye ualbino hawako salama,” alisema.

Kamanda Jongo alisema mtoto alitumwa na mama yake kuchota maji usiku na kwa mujibu wa daktari ni majeraha ya kawaida.

Alisema kifaa alichotumia mkataji kilikuwa cha ncha kali na angetaka kumuua au kuondoka na mkono angeondoka nao.

Kamanda Jongo alisema majeraha hayajafika kwenye mfupa lakini angekua na nia ya kukata kwa makato waliyozoea lingefika kwenye fuvu.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo na kuwataka wazazi wa watoto wenye ualbino kutokuwa na taharuki, kwani ndani yao wapo watu wanaotengeneza mazingira kuonyesha hawako salama jambo ambalo si sahihi.

Related Posts