Uamuzi wa Polisi wasubiriwa maziko ya mwanafunzi aliyepotea, mwili kukutwa shimoni

Kibaha. Wazazi wa Angel John, aliyepotea na baadaye mwili wake kukutwa kwenye shimo la choo akiwa amefariki dunia, eneo la Mwendapole, Kibaha wanasubiri uamuzi wa Jeshi la Polisi ili kuendelea na taratibu za mazishi.

Mwili wa Angel (8), mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Carisa, aliyeondoka nyumbani kumfuata dada yake aliyeenda kusuka ulipatikana jana Mei 7, 2024 kwenye shimo la choo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 8, 2024 baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Mseveni John amesema walienda polisi kupata utaratibu wa namna watakavyopewa ruhusa ya kuchukua mwili lakini wakaambiwa wasubiri.

“Tuko Hospitali ya Tumbi, polisi wamesema tusubiri kwanza maana tukio hili ni zito,” amesema akizungumza na mwandishi kwa simu.

Mseveni amesema wanaendelea kusubiri hadi watakapoelekezwa yanayopaswa kufanyika.

Angel aliyekuwa akiishi Mwendapole, Kibaha mkoani Pwani alipotea Mei 6, 2024 baada ya kuondoka nyumbani kwao akimfuata dada yake aliyekuwa amekwenda kusuka mtaa wa jirani na makazi ya familia yao.

Akizungumza jana Mei 7, 2024 baba mzazi wa mwanafunzi huyo, John alisema alipata taarifa za mwanaye kupotea aliporejea nyumbani akitoka kazini saa 11.00 jioni.

“Niliporudi kutoka kazini niliambiwa mwanangu amepotea tukaenda polisi kutoa taarifa, lakini wakatuambia hawawezi kupokea taarifa ya tukio ambalo halijamaliza saa 24, hivyo tulirudi tukaendelee kumtafuta,” amesema.

Mseveni ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Tumbi amesema walimtafuta usiku mzima wakipita mitaa kadhaa hakupatikana.

Amesema asubuhi ya Mei 7, 2024 mwili wake ulikutwa ndani ya shimo la choo ambacho hakijaanza kutumika.

Related Posts