Wadau wataja mbinu kukabili mafuriko, uharibifu miundombinu

Dar es Salaam. Wakati mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali nchini zikiendelea kuleta athari za kiuchumi na kukwamisha baadhi ya shughuli hasa usafirishaji, wadau wameshauri mbinu zinazoweza kutumika kukabili athari zake.

Pia, wameitaka Serikali ya Tanzania kuwa na utaratibu wa kufanya tathimini ya miundombinu kabla ya masika ili kuweza kupunguza athari zinazoweza kutokea.

Wametoa maoni hayo leo usiku Jumatano Mei 8, 2024 katika mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukijadili mada isemayo: “Nini kifanyike kukabiliana na athari za mvua?”

Akichangia maoni katika mjadala huo, mmoja wa wananchi Benedict Haule ameishauri Serikali kabla ya kuanza kipindi cha masika ni vyema kufanya tathimini ya makazi, miundombinu maeneo yote ya vijijini na athari gani zinaweza kujitokeza.

“Lengo ni kuangalia athari zilizotokea ni zipi na mvua zijazo zitasababisha athari gani, kwa hiyo lazima tathimini ya jumla ifanyike. Pia, ni muhimu kuundwa kwa mpango mkakati wa kuwapa watu elimu namna ya kukabiliana na athari za mvua tukijua kabisa jiografia ya maeneo yetu yametofautiana,” amesema Haule.

Mbali na tathimini alionyesha shaka kwa nini kila sehemu zinazoathirika zinakuwa zilezile huku akitaka Serikali ibuni njia ya namna ya kudhibiti matukio hayo kutokea mara kwa mara.

Moja ya mbinu iliyoshauriwa ni kuvuna maji ya mvua, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude amesema hali ya mvua nyingi inaweza kuwa ya kawaida ambayo wananchi wanaweza kuishi nayo baadaye ikiwa nchi itajipanga kwenye sekta za msingi za kiuchumi kwa kutumia maji tunayoyapata kuhifadhi ili baadaye kwenye jua kali yatumike.

“Pia, kuna haja ya kufanya utaalamu wa kiinjinia unaozingatia matukio kama ya mafuriko, hivyo miundombinu yetu iangaliwe ikiwezekana kufanyiwa utafiti kwa yale maeneo ambayo yapo hatarini zaidi ili kuwa na mpango mwingine ikitokea imeathirika tuweze kurejesha katika mazingira ya awali na shughuli za uzalishaji zikaendelea,” amesema Mkude.

Mbali na hilo ameitaka wizara kama ya kilimo ambayo ni msingi wa maisha ya watu wengi kuangalia kuwa na kilimo kinachozingatia hali ya hewa ili iwe ya mvua nyingi au jua kali, kwa sababu zote zina athari zinazofanana ikiwamo kukosa msimu wa kilimo.

Katika hilo la kilimo, Mhariri wa Jarida la Uchumi kutoka Gazeti la Mwananchi, Ephraim Bahemu amesema yapo mazao ambayo hayawezi kustahimili mvua nyingi yanayoweza kuathiriwa na mvua huku matumizi ya bima katika kilimo yakiwa yako chini.

“Watu wengi walioathirika hawajakata bima na hawa watu ambao wameathirika wasipoangaliwa kwa jicho la pekee ni masikini wa siku zijazo. Hivyo ni muhimu Serikali ikaangalia namna ya kuwarudishia hali zao za kiuchumi wakulima ambao mazao yao yamesomwa na mafuriko ili ili hao watu wasiwe mzigo kesho kwa watu wengine,” amesema Bahemu.

“Sasa tunachopaswa kufanya kukabiliana na matukio haya, kwanza Serikali imeweka mikakati, tuna Mpango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi 2021-2026.

“Nashauri wote tuupitie tuone nini Serikali imefanya kuandaa mkakati huo ambao mkakati huo umeelekeza kila mtu afanye juhudi fulani kukabiliana na matukio mabaya ya hewa,” amesema.

Kufuatia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ladislaus Chang’a amesema linalopaswa kufanyika sasa ni wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa zinazotolewa na TMA zikiwamo za utabiri na tahadhari.

“Serikali imewekeza sana kuimarisha TMA kwa mtizamo mpana kwa kuona jinsi ambavyo taarifa na uelewa wa nini kitatokea ni msingi mkubwa wa kukabiliana na hizi changamoto, hivyo Tanzania ipo mstari wa mbele kuwekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa,” amesema Chang’a.

Related Posts