Babati. Athuman Misanya (31) na Paulo John (23) wakazi wa Mamire na Magugu, wilayani Babati mkoani Manyara, wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 baada ya kukutwa na nyama ya twiga.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Victor Kimario alitoa hukumu hiyo jana jioni, baada ya kujiridhisha pasipo na shaka kuwa washtakiwa hao wametenda kosa hilo.
Hakimu Kimario amewatia hatiani Misanya na John kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kutaifishwa kwa pikipiki na ndoo waliyokuwa wamebebea nyama hiyo.
Amesema watu hao wawili bado vijana wenye uwezo wa kufanya kazi halali ya kujipatia kipato lakini wameamua kujielekeza kwenye ujangili wa kuua wanyamapori kwa lengo la kuuza nyama jambo ambalo halikubaliki.
“Hivyo, nawahukumu kifungo cha miaka 20 kila mmoja ili liwe fundisho kwa vijana wengine wanaotamani kufanya kitendo kama hiki ambacho ni kinyume na sheria,” amesema Hakimu Kimario.
Hata hivyo, amesema watu hao wana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kama hawajaridhika na hukumu hiyo.
Awali, waendesha mashtaka wa Serikali wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shaidu Kajwangya na Getrude Kariongi, wakishirikiana na Wakili Mwanaidi Chuma, walisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Februari 2, 2024.
Kajwangya alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo kwenye Jumuiya ya Wanyamapori Burunge kwa kukutwa na kichwa cha twiga, nyama, mkia na ngozi, ikiwa kwenye ndoo.
Amesema washtakiwa walitumia usafiri wa pikipiki katika kutenda uhalifu huo na walikutwa na nyara hizo za Serikali wakiwa wamezipakia kwenye chombo hicho.
Hivyo, akaiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili kutoa onyo kwa watu wengine wanaofanya ujangili kwa wanyamapori.
Naye Wakili Chuma amesema twiga ni mnyama mwenye nembo ya Taifa na kivutio kizuri cha utalii na kuiingizia nchi mapato kupitia watalii wanaotembelea maeneo hayo.