Dar es Salaam. Zaidi ya nusu ya magereza nchini, yamehama kutoka matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na sasa yanatumia nishati safi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia alitoa agizo mwaka jana, akitaka kuanzia Januari, 2024 taasisi zote za umma na binafsi zinazolisha watu 100 hadi 300 zitumie nishati safi ya kupikia.
Katika utekelezaji wa hilo, Jafo amesema kati ya magereza 126 yaliyopo nchini, 76 yanatumia nishati safi kwa sasa.
Si magereza pekee, amesema vyuo vya elimu 35 vilivyopo, kati ya hivyo 30 vinatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia.
Jafo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Mei 8, 2024 alipozungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024/2034.
Amesema jukumu la wizara anayoiongoza ni kuhakikisha utekelezwaji wa mkakati huo unaenda kama ilivyotarajiwa.
Dk Jafo amesisitiza umuhimu wa mabadiliko ya nishati kwa kuwa kuni na mkaa inaathiri uhai wa watu.
Amesema takribani watu milioni 2.3 hadi milioni nne wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati chafu Afrika.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema ili kudhibiti matumizi ya mkaa jijini humo, tayari kuna mpango umeandaliwa.
Mpango huo amesema ni pamoja na kukubaliana na mbinu za kudhibiti matumizi ya mkaa Dar es Salaam, huku mikoa mingine ikidhibiti ukataji wa miti.
Wakati Chalamila akisema hayo, takwimu zinaeleza asilimia 70 ya mkaa unaozalishwa nchini unatumika katika Jiji la Dar es Salaam.
Amesema namna ya kudhibiti matumizi ya mkaa ni kuongeza mahitaji yake ili bei ipae, huku nishati nyingine zikipunguzwa bei.
“Tudhibiti usambazaji wa mkaa ili kuongeza mahitaji, hapa tutasababisha bei yake iongezeke na bei ya nishati nyingine safi tupunguze ili watu waone rahisi kutumia nishati safi,” amesema Chalamila.