Dar inavyozizidi nchi zaidi ya 10 kwa utajiri Afrika

Pengine ni vigumu kuamini, lakini ndio ukweli wenyewe. Kama Dar es Salaam ingekuwa ni nchi ingekuwa na uchumi mkubwa kuliko mataifa mengi ya Afrika, hata Ulaya pia.

Kwa mujibu wa ripoti ya ufanisi wa kikanda inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kila baada ya miezi mitatu, pato la Dar es Salaam hadi Desemba 2022 lilikuwa Sh29.02 trilioni, ambazo ni sawa na Dola za Marekani 11.18 bilioni.

Uchumi huo ni mkubwa kuliko nchi za Somalia 8.1 bilioni, Mauritania ambayo ilikuwa na Dola bilioni 10.37 na Togo Dola bilioni 8.12.

Mataifa mengine yanayozidiwa uchumi na Dar ni Sudani Kusini, Eswatini, Liberia, Sierra Leone, Djibouti, Afrika ya Kati (CAR) Cape Verde, Lesotho, Eritrea, Guinea Bissau, Ushelisheli, Burundi na Comoro ambazo zote pato lake la taifa ni chini ya Dola bilioni 5.

Mbali na Afrika, zipo pia nchi za Ulaya, Amerika na Asia ambazo uchumi wa Dar es Salaam ni mkubwa kuliko wao. Kwa ufupi kama Dar ingekuwa nchi ingekuwa ya 145 kwa uchumi duniani, hivyo nchi zaidi ya 50 zingekuwa chini yake katika orodha.

Kwa Tanzania, licha ya kuwa nchi ina mikoa 31, lakini Dar es Salaam ndio mkoa wenye nguvu kubwa ya kiuchumi, unaweza kusema ndiyo roho ya uchumi wa Tanzania.

Jambo hilo kwa wakazi wa Dar ambao wanatajwa kuwa wastani wa kipato cha Sh5.4 bilioni kwa mwaka 2022, wanaweza kuliona kama la kujivunia, lakini wachambuzi wa kiuchumi wanaonya katika muktadha wa uchumi jumuishi.

Wataalamu wamesema ni muhimu fursa za kiuchumi zikagawanywa maeneo yote ili kila mkoa uwe na mchango katika pato la Taifa, badala ya kutegemea jiji la Dar es Salaam pekee karibu katika kila kitu.

Sifa yake ya kuwa jiji linaloongoza kwa idadi ya watu Tanzania, uwepo wa miundombinu ya usafirishaji kama bandari, huduma muhimu wanazohitaji wawekezaji zinatajwa kama sababu ya jiji hilo kuwa kitovu cha uchumi wa nchi.

Kauli hizo zinatolewa wakati ambao Ripoti ya Uchumi wa Kikanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa Dar es Salaam inabeba zaidi ya asilimia 60 ya shughuli zote zinazoingiza mapato ya Serikali, ikiwemo viwanda, ukusanyaji mapato, usafirishaji na uzalishaji umeme.

Katika nishati, uchambuzi unaonyesha kuwa asilimia 71.3 ya umeme wote unaotumika Tanzania unazalishwa jijini Dar es Salaam, licha ya kuwa vyanzo vyake ikiwemo gesi inayozalisha asilimia 60 ya umeme inatoka mikoa ya kusini.

Wakati huo pia, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya Sh7.205 trilioni zilikusanywa katika robo ya mwaka iliyoishia Desemba 2023, lakini asilimia 89.3 ya mapato yote yaliyokusanywa yalitoka jiji la Dar es Salaam.

Hiyo ni baada ya jiji hilo kuwa na lengo la kukusanya Sh6.55 trilioni, lakini wakakusanya Sh6.43 trilioni.

Kanda nyingine ambayo walau ilionekana kukusanya mapato yake kwa kiwango kikubwa ni ile ya Kaskazini ambayo ilichangia asilimia 5.2 katika mapato yaliyokusanywa ndani ya kipindi husika.

Kanda nyingine kama ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kusini Mashariki, Nyanda za Juu Kusini zilikusanya kwa asilimia 1, asilimia 1.8, asilimia 1.3 mtawalia.

Kuongoza katika makusanyo ya kodi kulienda sambamba na ufanisi wake ulioonekana katika makusanyo ya Serikali za mitaa ambapo katika Sh592.9 bilioni za nchi nzima, mkoa huo ulichangia asilimia 21.6 ya makusanyo yote.

Licha ya kuwa makusanyo hayakutofautiana sana na kanda nyingine, lakini bado ilibaki kushika namba moja, huku ikifuatiwa kwa karibu na Kanda ya Ziwa iliyochangia asilimia 20.7, Kanda ya Kati asilimia 15.4, Kusini Mashariki asilimia 14.6, Nyanda za Juu Kusini asilimia 13.7 na Kanda ya Kaskazini asilimia 13.9.

Wakati ambao mtandao wa benki umeenea na matawi kuwepo mikoa yote Tanzania, bado asilimia 55.9 ya mikopo yote iliyotolewa hadi Desemba 2023 ilikuwa kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Kanda nyingine ziligawana mikopo hiyo kwa kiasi kidogo ambapo Kanda ya Kati ilikuwa na asilimia 13.2, Kusini Mashariki asilimia 5, Nyanda za Juu Kusini (2.6), Kanda ya Kaskazini asilimia 10.2 na Kanda ya Ziwa asilimia 13.2.

Utolewaji wa mikopo hiyo ulienda sambamba na huduma za kifedha zilizokuwa zikitolewa ambapo Dar es Salaam kwa mujibu wa takwimu wanaongoza kwa kuweka amana zao benki.

Katika zaidi ya Sh32.619 trilioni zilizowekwa benki hadi Desemba 2023, asilimia 63.3 zote zilitokea jijini Dar es Salaam ambayo ilifuatiwa kwa mbali na Kanda ya Kaskazini iliyobeba asilimia 11.2 ya amana zilizowekwa benki.

Kanda ya Kati ilikuwa na asilimia 9.5, Kanda ya Ziwa asilimia 8.3, Nyanda za Juu Kusini asilimia 4.8, Kanda ya Kusini Mashariki asilimia 2.8.

Katika usafirishaji abiria na mizigo kupitia bandari na viwanja vya ndege vinavyopatikana nchini, huduma kubwa ilikuwa ikitolewa kupitia Dar es Salaam.

Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude anasema mara zote Dar es Salaam inaonekana kufanya vizuri kwa sababu ni sehemu ambayo ina miundombinu rafiki kwa ajili ya biashara, maji, barabara na umeme.

Pia ukaribu wa jiji hilo na bandari na njia nyingine za usafirishaji inafanya iwe sehemu rahisi ya kufanya uwekezaji na mtu kuifikiria kwanza akitaka kuwekeza, tofauti na mikoa kama Singida na Mtwara ambapo ataona gharama za usafirishaji zitaongezeka.

Amesema pia uchumi kubaki eneo moja itafanya kila mtu kutamani kuhamia huko, jambo litakalofanya idadi ya watu kukua kwa kasi, huduma za kijamii zitakuwa zinahitajika kila wakati na zitakuwa zinaenda kinyume na mipango ya nchi.

“Hii itafanya mikoa mingine ishindwe kunyanyuka kiuchumi na watu kujiinua kiuchumi, jambo ambalo litazorotesha kasi ya utokomezaji umasikini, hivyo inafanya kiwango cha watu kujikwamua kiuchumi kuwa kidogo,” anasema Mkude.

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo anasema uwepo wa vitu vya asili kama bandari katika jiji la Dar es Salaam inakuwa ni moja ya faida kwa mkoa huo.

Uwepo wake unafanya baadhi ya shughuli kufanyika sana ndani ya jiji hilo, tofauti na sehemu nyingine ambazo hazina bandari.

Hata hivyo, anashauri kuwa ni vyema shughuli za uzalishaji mali zikatawanywa kila sehemu ili kuondoa ile dhana kuwa ili mtu atoke kimaisha lazima aende Dar es Salaam ambapo vitu vingi vinapatikana.

Akitolea mfano wa uzalishaji umeme nchini, anasema kulikuwa hakuna haja ya gesi ambayo inazalisha umeme kwa zaidi ya asilimia 60 kusafirishwa kutoka mikoa ya Kusini kuja Dar es Salaam ili umeme uzalishwe na kusambazwa tena mikoani.

“Mfano maji yako Kidatu, Mtera, Mwalimu Nyerere umeme unazalishwa huko, hivyo hata hili ingewezekana kutengeneza umeme huko badala ya kuleta Dar es Salaam uzalishe na kuusambaza,” anasema Dk Kinyondo.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema uchumi unapokuwa sehemu moja unakuwa si jumuishi na badala yake unatakiwa utawanyike ili watu waweze kufikiwa na fursa sehemu walipo bila kuwapo kwa ulazima wa wao kutoka eneo moja kwenda jingine.

Amesema uchumi unapokuwa umejikita katika eneo moja kama Dar es Salaam inavuta watu wengi kukimbilia eneo hilo, jambo ambalo linaleta changamoto katika upangaji mji, kushughulikia changamoto tofauti na fursa hizo zinapotawanyika maeneo mengi ukuaji wa idadi ya watu na makazi vingetawanyika.

“Tuchukulie mfano, Kimbunga Hidaya kingekuja kama kilivyokuwa kinasemwa, kikaipiga Dar es Salaam vilivyo, kikaharibu miundombinu, viwanda ingekuwa ni hatari kubwa katika uchumi wetu,” anasema Dk Olomi.

Kufuatia suala hilo, amesema kwa sababu za kiusalama kusambaza ukuaji wa uchumi, kuweka miundombinu inayovutia uwekezaji katika maeneo mengine na kuitumia ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa.

Dk Olomi anasema ili kuondoa utegemezi wa eneo moja katika kuendesha nchi, ni vyema ikaangaliwa namna ya kusambaza huduma zinazowezesha uwekezaji kama nishati, barabara, reli, vyuo vya ufundi kuvisambaza, kusambaza vivutio na huduma muhimu.

Anasema hilo litawezekana kwa kutoa unafuu wa kodi kwa wawekezaji ikiwa wanajenga kiwanda katika eneo ambalo limelengwa kwa ajili ya ukuaji au maeneo ambayo hayavutii watu kama Dar es Salaam.

“Miundombinu inayovutia watu, ikiwemo huduma muhimu kama afya, shule, baadhi ya wawekezaji wanapotaka kuajiri watu waajiriwa wanaanza kuangalia nikienda mfano Rukwa mtoto wangu atasoma wapi, nikitaka kwenda nitafikaje, nitatumia siku ngapi barabarani, kuna uwanja wa ndege, kuna nyumba ya mimi kukaa kule,” anasema Dk Olomi.

Anasema haya yataweza kufanyika ikiwa kutakuwa na mkakati wa kuendeleza maeneo maalumu ya uwekezaji kwa kupewa huduma zote muhimu zinazovutia wawekezaji, jambo ambalo litaleta matokeo chanya kwa sababu ni ngumu kuwekeza kila sehemu.

Profesa Kinyondo anasema nchi sasa inaweza kutengeneza maeneo ya vitega uchumi katika maeneo husika, huku akitolea mifano ya mikoa inayopakana na nchi jirani kama Kigoma na Kagera.

“Lakini wakati wa Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius) viwanda viliwekwa kimkakati, kiwanda cha katani Tanga kwa sababu inazalishwa kwa wingi, pamba – Mwanza, Mgololo kiwanda cha karatasi kwa sababu kuna mbao nyingi, baadaye hii ilipotea lakini ukifanya hivyo unaweza kusambaza fursa hizi za kiuchumi,” amesema Profesa Kinyondo.

Hali hiyo itasaidia kuondoa ukuaji wa idadi ya watu katika eneo dogo, huku akieleza kuwa hata kelele za mafuriko zinazosikika ni kwa sababu ya ukuaji wa mji ambao umefanya watu kujenga katika njia za maji.

Mkude anashauri kuwa ni vyema kuweka miundombinu unganishi, ikiwemo reli ili kuweka urahisi katika usafirishaji bidhaa huku akiwa na matumaini kuwa huenda reli ya kisasa ikaleta mapinduzi, ikiwemo kupunguza gharama za usafirishaji baada ya ile ya Tanzania – Zambia kushindwa kuonyesha ufanisi mkubwa.

“Pia umeme unaendelea kuimarika huenda baada ya kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) uwezekano wa Shirika la Umeme Tanzania kufikia mikoa mingi inaweza kufanya watu kuvutiwa kuwekeza katika maeneo mengine, jambo ambalo litafanya uchumi kukua,” amesema Mkude.

Related Posts