Mpizani wa Rais Paul Kagame, Diane Rwigara ametangaza kuwania tena urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai 15, 2024mwaka huu.
Mbali na Diane, Rais Kagame ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, anatarajiwa kupambana na Frank Habineza wa Chama cha Green na mgombea binafsi Philippe Mpayimana, kwenye uchaguzi huo.
Diane, 42, kiongozi wa Chama cha People Salvation Movement, alianza harakati za kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2017 lakini hakupitishwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
Pia, mfanyabiashara huyo ambaye kitaaluma ni mhasibu, ni mwanaharakati wa haki za wanawake.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Rwigara ameandika jana Mei 8 kuwa anafungua ukurasa mpya kwenye uwanja wa kisiasa na kuwaomba Wanyarwanda wamuunge mkono ili kuandikisha historia.
“Ukurasa mpya kwa Rwanda unaanza sasa. Kwa pamoja tutatengeneza historia. Niungeni mkono kwa ajili ya urais.”
Katika uchaguzi wa mwaka 2017 ambao Rais Kagame alishinda kwa asilimia 98.8, Rwigara alizuiwa na Tume ya Uchaguzi kushiriki kwa madai kuwa aliwasilisha majina ya watu waliokufa kama wadhamini wake wa kugombea kiti hicho.
Mbali na kuzuiwa kugombea, Rwigara na familia yake walianza kuandamwa na mikasa ya vyombo vya ulinzi.
Hatimaye Diane na ndugu zake Anne Rwigara (sasa marehemu) na mama yao, Adeline Rwigara, walituhumiwa kughushi nyaraka katika mchakato wa kutafuta wadhamini ili aweze kugombea urais kwenye uchaguzi uliomalizika miezi miwili iliyopita.
Agosti 30, 2017, nyumba ya Rwigara ilivamiwa huku polisi wakisema alikuwa anachunguzwa kwa kughushi na kukwepa kulipa ushuru.
Wakati huo, mwaka 2017, siku moja baada ya kutangaza nia yake ya kuwania urais, mitandaoni zilionekana picha zikimwonyesha akiwa utupu, katika kile alichosema alilengwa kisiasa ili kumyamazisha.
Hata hivyo, alizikana picha hizo akisema zimetengenezwa kwa umahiri wa hali ya juu ili kumdhalilisha na kumpunguzia nguvu kutimiza azma yake.
Akihojiwa na Kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, kabla ya kujitosa katika uchaguzi, Diane alisema anajua kitakachompata lakini haogopi tena.
“Fisi akikukimbiza muda mrefu woga huwa unapotea,” alisema huku akikiri kuwa anaumizwa na hali ilivyo hasa ya watu kushindwa kuongea kwa uwazi kwa sababu ya hofu.
Desemba 28, 2023 mdogo wake Anne Rwigara (41), alifariki dunia akiwa California, nchini Marekani.
Mama yake Anne, Adeline Rwigara, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kifo cha bintiye ni cha kutatanisha, kwani hakuwa mgonjwa.
Kwa mujibu wa taarifa, Anne alianza kusumbuliwa na maumivu ya tumbo kabla ya umauti kumfika.
Anne Rwigara pia amejitokeza mara kadhaa katika kesi ambazo familia yake imefungua kuhusiana na mali zao, kikiwamo kiwanda cha tumbaku cha Premier.
Sababu kuu ya kila kitu wakati huo ilikuwa kodi ambayo Serikali ilisema inaidai familia ya Rwigara.
Anne na mama yake walikaa gerezani kwa mwaka mmoja nchini Rwanda kwa tuhuma za kukwepa kulipa ushuru na makosa yaliyohusiana na uchaguzi nchini Rwanda.
Baba yao, Assiponal Rwigara, alifariki kwa ajali ya gari mwaka 2015, lakini familia hiyo ilidai kuwa kifo hicho kilipangwa, japo hawakusema kilipangwa na nani.
Licha ya kuwa familia ya kitajiri nchini humo, hawakuwahi kufurahia utajiri huo tangu baba yao alipofariki kifo cha utata mwaka 2015.
Juni 2018, Mamlaka ya Mapato ya Rwanda iliuza mashine za kiwanda cha tumbaku cha familia hiyo kwa zaidi ya Sh5 bilioni kwa nia ya kurejesha kile walichodai kuwa ni malimbikizo ya kodi ya zaidi ya Sh17 bilioni.
Mnada wa awali wa mali ya biashara ya familia ya Rwigara ya tumbaku iliyosindikwa ulipata zaidi ya Sh995 milioni.
Oktoba 5, 2018, mahakama iliamuru kuachiwa huru kwa Diane na mama yake, Adeline kwa dhamana; hii ilikuja wiki chache baada ya kuachiwa kwa wafungwa 2,140, ikiwa ni pamoja na Victoire Ingabire na Kizito Mihigo.
Hata hivyo, Diane na mama yake waliambiwa wasiondoke katika mji mkuu Kigali, bila kibali na kuwa kesi yao ingeendelea.
Licha ya Rwanda kutajwa kuongoza duniani kwa kuwa na wabunge wanawake zaidi ya asilimia 61, mateso huwakuta wale wanaoipinga Serikali.
Mwaka 2003, Alvera Mukabaramba alijaribu kugombea urais lakini alijitoa na kuungana na Rais Kagame.
Mwaka 2010, Victorie Ingabire aliyekuwa akiishi Uholanzi alikwenda Rwanda kugombea urais, lakini aliingia matatizo baada ya kuzungumzia mauaji ya kimbari na kudaiwa kuwa aliyakana, hivyo alihukumiwa kifungo cha miaka 15.
Leon Orsmond, mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Afrika Kusini, ambaye alimsaidia Diane katika kampeni yake ya mitandao ya kijamii pia alipotea nchini Rwanda tangu Februari 2018.
Kabla ya kutoweka, Orsmond hakuficha chuki yake kwa Serikali ya Kagame.