Job afichua ishu Yanga | Mwanaspoti

Beki wa Yanga, Dickson Job amesema wamekuwa wakionyesha hali ya kupambana zaidi pindi wanapokutana na timu inayozuia muda mwingi tofauti na wale wanaofunguka.

Nyota huyo ametoa kauli hiyo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na kuiweka Yanga katika nafasi nzuri zaidi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara yake ya tatu mfululizo.

“Hakuna timu nyepesi kwa sababu kila unayocheza nayo ina malengo iliyojiwekea kama ilivyokuwa kwetu pia, sisi wachezaji huwa tunafurahia zaidi kucheza na timu ngumu inayozuia muda mwingi kwani inatuongezea morali ya kupambana,” alisema.

Job mwenye bao moja la Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na kikosi hicho aliongeza kwamba wao kama wachezaji wanatambua kiu kubwa ya mashabiki zao ni kuona wanatwaa ubingwa hivyo sababu hiyo inawafanya kupambana zaidi bila ya kujali wanacheza uwanja gani.

“Bado hatujakamilisha malengo yetu ila hadi hapa tulipofikia kwa kiasi kikubwa tunaona mwanga huko mbeleni, tunafurahia mashabiki zetu wanavyoendelea kutuunga mkono na sisi kama wachezaji tuko bega kwa bega na tunawaahidi hatutawaangusha.”

Ushindi huo umeifanya Yanga kuendeleza rekodi nzuri pindi inapokuwa wenyeji kwani tangu msimu huu umeanza haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara ambapo katika mechi 13 ilizocheza imeshinda zote sawa na kukusanya jumla ya pointi 39.

Katika michezo 13, Yanga imefunga jumla ya mabao 33 na kuruhusu matano tu huku mechi 13 za ugenini iliyocheza imeshinda tisa, sare mbili na kupoteza mbili pia ikiwa imefunga mabao 24 na kuruhusu saba sawa na kukusanya jumla ya pointi 29.

Kwa sasa Yanga imefikisha pointi 68 katika michezo 26 iliyocheza hivyo inahitaji pointi tano tu ili kufikisha 73 ambazo zitawapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa ujumla kwa sababu hazitafikiwa na timu yoyote.

Azam iliyopo nafasi ya pili na pointi 57 hata ikishinda michezo yake yote mitano iliyobakia itafikisha pointi 72, huku Simba inayoshika nafasi ya tatu na pointi 53 ikishinda mechi zake zote sita zilizobakia itamaliza msimu huu na pointi 71.

Related Posts