Jubilee Allianz kuanza kutoa bima ya kilimo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katika jitihada za kuwahakikishia usalama wakulima Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz imetangaza kuanza kutoa bima ya mazao kwa wakulima.

Mpango huo umetangazwa Mei 9,2024 wakati wa hafla ya kuwatambua mawakala wanaoshirikiana nao na kuwapongeza kwa kufanya vizuri.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mtendaji Mkuu wa Jubilee Allianz, Dipankar Acharya, amesema mpango huo unalenga kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini.

Meneja wa Mawakala katika Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz, Mary Ndege, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika tasnia ya bima.

Naye Meneja wa Mawakala, Mary Ndege, amesema kwa muda mrefu sekta ya kilimo ilionekana kusahaulika hivyo bima itawawezesha kuwakinga na majanga.

“Kilimo ni mojawapo ya sekta inayoiingizia kipato nchi yetu ndiyo maana tunatamani watu wanaoingia kwenye kilimo wasijisikie kwamba wakipata hasara itakuwaje…tunatamani wajisikie kwamba wakiwa katika kilimo kuna usalama,” amesema Mary.

Amesema pia tasnia ya bima ina fursa kubwa na kuwashauri vijana waliohitimu taaluma hiyo kutosubiri kuajiriwa badala yake wajiajiri.

“Kwenye tasnia ya bima kuna fursa ya kujiajiri, wewe ambaye ni mhitimu wa taaluma ya bima tunaomba utamani kujiajiri, unaweza kutoka shule na kujisajili kuwa wakala na ukaanza kujiingizia kipato mapema,” amesema.

Aidha amesema waliona ni vyema kuwapongeza mawakala kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakifanya kwa lengo la kuwatia moyo ili kuboresha utendaji wao.

Katika hafla hiyo Wakala aliyeibuka mshindi wa jumla Jesse James, amesema; “Zawadi tulizopewa zimetuongezea nguvu ya kuzidi kupambana katika sekta hii ya bima ambayo ina fursa nyingi.

Related Posts