Kamati ya Bunge yaeleza kutoridhishwa bajeti Wizara ya Maji

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imesema bajeti ya Wizara ya Maji ya 2024/25 imepungua, hali inayoonyesha wizara hiyo si miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka huo wa fedha.

Imesema licha ya kuiunga mkono, lakini kupungua kwa bajeti ya maendeleo ya wizara kunaweza kuathiri utekelezaji bora wa miradi kwa kukosa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga amesema hayo leo Alhamisi Mei 9, 2024 alipowasilisha maoni ya kamati bungeni baada ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kusoma taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/25 akiliomba Bunge kuidhinisha Sh627.7 bilioni.

Kiswaga amesema makadirio ya bajeti yote ya Wizara ya Maji yamepungua kwa asilimia 17 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Amesema makadirio ya matumizi kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo yamepungua kwa kiasi cha Sh137.7 bilioni sawa na asilimia 18.4 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Ni mtazamo wa kamati kwamba, kupungua kwa kiasi hiki cha bajeti ya maendeleo kutaathiri utekelezaji wa miradi ya iliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025,” amesema.

Kiswaga amesema makadirio ya matumizi ya kawaida yameongezeka kwa Sh9.2 bilioni sawa na asilimia 1.2 ya bajeti ya mwaka wa fedha unaoisha.

“Kamati haijaridhishwa na bajeti hii, kwani haijazingatia ipasavyo maelekezo kwa Serikali yaliyomo kwenye Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025,” amesema na kuongeza:

“Ilani ya CCM imeahidi kuimarishwa kwa huduma ya majisafi na salama ili ifikapo mwaka 2025 wakazi asilimia 85 waishio vijijini na asilimia 95 ya wakazi waishio mjini wawe wamefikiwa na huduma hiyo.”

Amesema msisitizo wa kamati kwa Serikali ni kuhakikisha bajeti ya Wizara ya Maji inaongezwa kwa Sh137.7 bilioni ili angalau ibaki kama ilivyokuwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Kiswaga amesema bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni asilimia 1.3 ya Bajeti Kuu ya Serikali.

Amesema hali hiyo inaonyesha bajeti ya Wizara ya Maji imepungua kwa asilimia 0.4 ikilinganishwa na ya mwaka wa fedha 2023/2024.

“Bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni asilimia 1.1 ya Bajeti Kuu ya Serikali ya maendeleo ambayo ni asilimia 32. Uchambuzi huo unaonyesha kuwa, Wizara ya Maji si miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka huu wa fedha,” amesema.

Amesema ongezeko hilo la bajeti litawezesha Serikali kutekeleza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvipatia huduma ya maji vijiji 2,581 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.

“Serikali ione umuhimu wa kuongeza fedha katika Mfuko wa Taifa wa Maji kutoka Sh50 inayotolewa sasa kwa kila lita ya dizeli na petroli hadi kufikia Sh100 ili kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema.

Kamati imesema kupungua kwa bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Maji kunaweza kuathiri utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo, hivyo kukosa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji kama vile ujenzi wa mabwawa ya Kidunda, Furkwa na Ndembera/Lugoda unahitaji dhamira ya dhati ya Serikali ya kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili hiyo,” amesema.

Amesema baadhi ya miradi ya maji imechelewa kukamilika kutokana na malimbikizo ya madeni ya wakandarasi hivyo kuathiri utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi, kuongeza gharama na kuathiri masilahi ya wakandarasi.

Amesema kutosambaza maji kwa wananchi maeneo ambayo uchimbaji wa visima umekamilika pia kunaondoa tija ya miradi hiyo na kuleta hasara kwa Serikali.

“Vituo vya kuchotea maji katika baadhi ya maeneo kuwa mbali na makazi ya watu ni kinyume cha Sera ya Maji ya mwaka 2002, inayotaka wananchi kupata maji katika umbali usiozidi mita 400,” amesema.

Amezungumzia gharama kubwa ya maunganisho mapya ya maji akisema inawanyima wananchi wa hali ya chini hasa wa vijijini kupata haki ya huduma ya maji.

Ameeleza wataalamu wa maunganisho mapya ya maji kuwa mbali, kunasababisha upotevu mkubwa wa maji pale mivujo inapotokea.

“Kutokutumika ipasavyo kwa mitambo iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kuchimba visima nchini kunaondoa tija iliyokusudiwa ya kuwapatia wananchi majisafi na salama,” amesema.

Kamati imesema ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika uandaaji wa miradi ya maji umechangia uwepo wa migogoro na uharibifu wa miundombinu ya maji, ikiwamo madai ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi kutokulipwa kwa wakati kama sheria ya fidia inavyoelekeza na maji katika baadhi ya miradi kutokuwa na ubora.

Kamati imeitaka Serikali ihakikishe inalipa malimbikizo ya madeni yote ya wakandarasi kabla ya Juni 30, 2024, ili miradi ikamilike na kuwanufaisha wananchi.

Pia, imeitaka Serikali kuhakikisha maji yanayosambazwa yanakuwa na ubora unaohitajika kwa matumizi ya wananchi.

Akiwasilisha bungeni bajeti ya Wizara ya Maji, Waziri Aweso amesema katika mwaka 2023/24, wizara iliidhinishiwa Sh756. 2 bilioni.

“Kati ya fedha hizo Sh60.3 bilioni zilikuwa za matumizi ya kawaida na Sh695.8 bilioni ni fedha za maendeleo,” amesema.

Amesema hadi Aprili 2024, Wizara imepokea Sh639.4 bilioni sawa na asilimia 84.6 ya bajeti iliyoidhinishwa.

Kati ya fedha zilizopokelewa, amesema Sh593.3 bilioni ni za kutekeleza miradi ya maendeleo na Sh46 bilioni ni za matumizi ya kawaida.

Kuhusu ubora wa maji katika vyanzo vya maji amesema vimekuwa vikitofautiana kulingana na jiografia, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu na hali ya miamba.

“Takwimu zinaonyesha hali ya ubora wa maji kwenye vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi inawezesha ustawi wa ikolojia, hivyo vinaweza kuendelezwa kwa matumizi ya sekta mbalimbali,” amesema.

Amesema, “pamoja na hali hiyo ya ubora wa maji, bado kunahitajika jitihada za pamoja za kuzuia uchafuzi, kurejesha na kuimarisha ubora wa maji wa asili katika vyanzo vya maji,” amesema.

Aweso amesema maji yanayosambazwa vijijini na mijini yameendelea kukidhi viwango vya kitaifa vya ubora wa maji ya kunywa, hivyo kulinda afya ya jamii kwa ujumla.

Amesema hali hiyo inatokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika ujenzi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji, usimamizi na udhibiti wa ubora katika mifumo ya usambazaji maji kuanzia kwenye vyanzo hadi kwa watumiaji.

Kuhusu upatikanaji wa huduma ya majisafi na mazingira vijijini, amesema Serikali ina azma ya kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wanapata huduma bora na endelevu ya majisafi na salama kwa zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Aweso amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeendelea na jitihada za kujenga na kukarabati miradi ya maji, kupanua mitandao ya kuyasambaza, na kuimarisha usimamizi wa huduma ya vijijini.

Jitihada hizo amesema zimewezesha kuongezeka upatikanaji wa huduma ya maji kutoka wastani wa asilimia 77 Desemba, 2022 hadi kufikia wastani wa asilimia 79.6 Desemba, 2023.

“Kiwango kilichoongezeka kimetokana na kutekelezwa kwa miradi 632 yenye vituo vya kuchotea 7,956, vyenye uwezo wa kuhudumia wananchi 4,740,959,” amesema.

Amesema hilo linafanya jumla ya wananchi wa vijijini wanaopata huduma ya maji kufikia 34,950,368 kati ya wananchi 39,232,999 waishio vijijini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Related Posts