Lissu, Halima Mdee hapatoshi

VITA ya maneno kati ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu na Mbunge Viti Maalum aliyefukuzwa na chama hicho, Halima Mdee, kuhusu madudu aliyoyaibua katika chaguzi za ndani, imeendelea kupamba moto mitandaoni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Vita hiyo iliibuka baada ya Mdee kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), tarehe 3 Mei 2024, kukosoa hatua ya Lissu kutoa hadharani tuhuma za uwepo wa fedha chafu, katika mchakato wa uchaguzi wa ndani wa Chadema.

Kupitia ukurasa wake wa X Mdee aliandika “wengine wanajiandaa na uchaguzi, wengine wanatupiana mishale na kudhalilishana mbele ya wananchi. Nadhani mchawi wa kwanza ni yule aliyewaongopea mkakati utawasaidia, haitakusaidia wala haisadii taasisi iliyojengwa na wengi ambayo unadhani utaipata kwa kupaka matope wengine. Tunaokujua hatushangai, but wasiokujua wanahoji hizo busara zako.”

Lissu na Mdee

Kufuatia ujumbe huo, jana akizungumza na wananchi wilayani Mpwapwa, jijini Dodoma, Lissu alimjibu Mdee huku akimhoji juu ya uhalali wake wa kumkosoa ilhali yeye si mwanachama wa Chadema.

“Nimeona kidogo Halima Mdee, wale wabunge waliohongwa, wale waliokuwa Chadema viongozi waliohongwa na kina Ndugai na Magufuli wakaapishwa uchochoroni wakafanywa wabunge wasiokuwa na chama na yeye analalamikia hotuba yangu ya Iringa niliyosema tujihadhari na pesa ya Abdul na mama yake zitatuchafulia chama, naye amenirushia mawe,” alisema Lissu.

Baada ya Lissu kumjibu Mdee, mbunge huyo viti maalum ambaye hatma ya uanachama wake unasubiria utekelezaji wa agizo la Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, lililoitaka Baraza Kuu la Chadema kupitia upya rufaa zao za kupinga kufukuzwa ndani ya chama hicho, alidai anapuuza majibu yake kwani ni porojo.

“Kumbe ulinisoma na kunielewa vyema. Hizo porojo nyingine nazipuuza maana najua nawe wajua ni porojo tu, kikubwa umenipata. Nilisema tunaokujua hatukushangai, japo wenye akili wameshakusoma na wanakupotezea kimtindo. Narudia mchawi wako mkuu ni yule aliyekudanganya kwamba utakuwa salama kwa kuishambulia taasisi una uchu wa kuiongoza japo kanda ilikushinda,” alijibu Mdee.

Related Posts