Dodoma. Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na Kimbunga Hidaya ni Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro.
Licha ya eneo hilo kuwa kwenye mkondo wa maji, lakini Kimbunga Hidaya kinatajwa kusababisha maafa ya watu saba, kubomoa nyumba 43 zilizokuwa zikitumika kwa makazi na kuharibu ekari 23,501 za mazao mbalimbali mashambani.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa maswali ya papo kwa papo bungeni jijini Dodoma, leo Mei 9, 2024.
Majaliwa amesema katika halmashauri hiyo juma la kata nne za Viwanja 60, Mbasa, Kibaoni na Katindiuka zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za mvua zilizosababisha mafuriko baada mto Lumemo kujaa na kumwaga maji kwenye makazi ya watu.
Mbali na athari hizo, pia nyumba 512 zilizingirwa na maji na kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara zinazounganisha wilaya kwa wilaya, barabara za vijiji na mitaa pamoja na miundombinu ya Reli ya TAZARA.
Mazao yaliyoharibiwa ni pamoja na mahindi, mpunga na mazao mengine mchanganyiko na mifugo.