Majiha: Nilishinda mkanda, asubuhi nikaomba hela ya vitafunwa

TANGU Tanzania inapata huru, bondia Fadhili Majiha maarufu zaidi kama Kiepe Nyani amekuwa Mtanzania na bondia wa kwanza kufikisha hadhi ya nyota nne na nusu akivunja rekodi ya Hassan Mwakinyo aliyewahi kufikisha nyota nne pekee.

Ndiye bondia namba moja Tanzania ‘Tanzania one’ na ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania pekee Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kumiliki mkanda wa Baraza la Ngumi Duniani kwa kanda ya Afrika (WBC Africa) na anashikilia rekodi ya kushika namba tano duniani katika mabondia 1056 kabla ya kuporomoka.

Bondia huyo hatajwi sana, hadi sasa ameweka rekodi nyingi ikiwemo ya kushinda mkanda wa ubingwa WBA Pan Afrika mara mbili katika mataifa mawili tofauti (Kenya na Afrika Kusini) pamoja na kushinda mapambano mengine mawili yasiyokuwa ya ubingwa.

Mwaka 2016 alimchapa Heri Amol wa Indonesia kwa pointi nchini kwao kabla ya mwaka 2021 kumchapa Harvey Horn kwa TKO katika pambano la raundi 10 lililopigwa Uingereza.

Majiha mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 50 akiwa ameshinda 32 kati ya hayo 15 ni kwa KO na amepigwa mara 14 na mara tatu ni kwa KO huku akitoka sare mara nne na nafasi yake duniani kwa sasa akiwa 19 katika mabondia 1056 wakati akiendelea kusalia kuwa bondia namba moja kwa mabondia wote wa Tanzania na Afrika katika uzani wake wa Super Bantam.

Bondia huyo ambaye amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti amefunguka mambo na mikasa mingi aliyokutana nayo kwenye mchezo huo hadi kufikia alipo katika nafasi hiyo.

Majiha anajipambanua ameanza kuupenda mchezo wa ngumi tangu akiwa kijana mdogo akisoma shule ya msingi kutokana na muda mwingi kumwona kaka yake Jafari Majiha aliyekuwa akicheza ngumi wakati huo.

Bondia huyo ameendelea, kaka huyo ndiye sababu kubwa ya yeye kuingia kwenye mchezo huo wakati huo wakiwa wanaishi Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar ingawa baadae kaka yake aliachana na mchezo wa ngumi na kuamua kuwa mwalimu wa mazoezi katika gym mbalimbali.

Pambano la kwanza ulicheza na nani?

“Nakumbuka na nilicheza na Ramadhani Kumbele mwaka 2008, nilimpiga vizuri na baada ya hapo nikawa nawaza kufanya mambo makubwa ikiwemo kufika mbali.

Uliwahi kucheza na Nasibu Ramadhan na alikupiga nini ilikupata?

“Nilicheza na Nasibu mwaka 2012, Nasibu nilimpiga pale Friends Corner, Manzese kwa sababu kila raundi alikuwa anafutwa damu ila katika lile pambano lilikuwa na mambo ya figisu nyingi sana.

“Unajua yupo kiongozi mmoja ameshafariki na nilishamsamehe lakini yeye ndiye alifanya makosa makubwa sana maana pambano langu dhidi ya Nasibu lilikuwa ni la ubingwa wa taifa ambao ulikuwa unatoka kwenye chama cha huyo kiongozi.

“Lakini malengo ya huyo kiongozi na promota yalikuwa ni kutaka Nasibu awe bingwa ili aende kushinda tuzo ambayo ilikuwa ikitolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa).

“Sasa kwa jinsi pambano lilivyokuwa siku ile Nasibu alikuwa amepoteza yaani nilimpiga promota, alikuwa jamaa flani hivi na wao walishakaa kujadili hiyo tuzo na wataipataje kwa kuwa ilikuwa na pesa ndiyo wakampendekeza mpinzani wangu.

“Unajua hadi pambano lilivyokuwa linaisha wao walikuwa hawajapata bingwa na wao walikuwa wapo radhi wampe Nasibu ili wakachukue tuzo na kusababisha kutokea ugomvi mkubwa sana na mwishowe yule kiongozi alichukua kipaza sauti na kwenda kutangaza nje pambano halina mshindi litarudiwa.

“Lakini baada ya kurudi gym na kocha wangu, promota wa lile pambano akapiga simu niende ITV wakanipe ubingwa wangu, nilimuuliza kwa nini akanieleza walishindwa kunitangaza pale kwa kuwa Nasibu akishakuwa amesaini na Francis Miyeyusho kwa kuogopa wangelipoteza hilo pambano.

“Bahati mbaya niligombana sana na yule promota ila mwishowe niliamua kuachana navyo kabisa vile vitu ingawa yule kiongozi akiingiza matokeo kwenye boxrec kama nimepigwa akidai nilitaka kumpiga hivyo alifanya kunikomoa.

“Ukiangalia hilo ndiyo pambano pekee ambalo linaonyesha nimepigwa hapa Bongo ila nilipigishwa kutokana na watu ambao walikuwa wakiangalia masilahi yao.

Malipo yalikuaje wakati ule?

“Kiukweli malipo yalikuwa chini sana, mtu anaweza akakuambia chukua 70,000, sasa hapo ndiyo kuna maandalizi na kila kitu na kocha umpe kutokea hapo yaani ilikuwa shida sana.

Hivi pesa ya kwanza kulipwa ilikuwa shilingi ngapi?

“Unajua nishacheza mapambano mengi ya kuburuzwa, nakumbuka nishawahi kupigana nikapewa Sh500 ambayo ilikuwa nauli ya kutoka Ukumbini Luxury Pub, Temeke kurudi kwetu Mwananyamala.

“Siku nyingine ikawa 1000 na mara ya mwisho mama yangu ndiyo alikuja kunifumbua macho baada ya kushinda Mkanda wa Afrika ABU pale Magomeni Kondoa dhidi ya Shaban Madilu ila mwishowe promota hakunipa pesa.

“Niliumia sana maana nilivyorudi nyumbani, asubuhi nikamwomba mama pesa ya vitafunwa, mama akaniuliza wenzangu wanacheza ngumi wanapata pesa ila mimi napewa mibati akimaanisha ule mkanda ambao nilishinda, alininyima kwa muda japo baadae alinipa baada ya kunituma mashine kusaga unga.

Baada ya hapo ndiyo nikajua huu mchezo una faida gani katika suala zima la kipato.

Ilikuaje hadi ukaanza kupata nafasi ya kwenda kupigana nje?

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2009 alikuja bondia wa zamani kunifuata anaitwa George Sabuni na kuniambia nina pambano Afrika Kusini ambalo lilitafutwa na Boniface Wambura kabla ya kuingia TFF wakati huo alikuwa mtu wa ngumi.

“Katika hilo pambano binafsi malipo yangu yalikuwa ni Dola 1500 na niweza kununua godoro, kitanda  na ndiyo nikatoka kwa mama yangu kwenda kupanga.

Vipi suala la mabondia kulipishwa vyakula kwenye ndege lina ukweli wowote?

“Ni kweli hilo jambo lilikuwepo ila upande wangu naweza kusema nilikutana nalo au sijakutana nalo kwa sababu mawakala wa ngumi zamani wamewaburuza watu wengi siyo mimi peke yangu, walianza wakubwa zetu halafu tukafuata sisi.

“Unajua walikuwa na desturi ya kukupa pambano pamoja na malipo ambayo unatakiwa kulipwa na mtu anajikuta anapanda ndege halafu hajui chochote ambacho kinafanyika kwenye ndege.

“Sasa ikawa ile ukinywa chai au kahawa na chochote utakachokula ndiyo mtu utasikia anakwambia unaona vile ambavyo umekula kwenye ndege, nimekulipia vyote hivyo nakata kwenye pesa yako na wewe hauna unachokijua unaona sawa.

Wewe ndiye bondia wa kwanza kushinda mikanda miwili ya ubingwa nje ya Tanzania, ilitokana na kitu gani?

“Kweli nashukuru Mungu, nimeshinda mkanda wa kwanza wa ubingwa wa WBA Pan Africa nchini Kenya Kwa kumpiga Gabriel Ochieg mwaka 2017, kisha nikashinda tena ubingwa huo Afrika Kusini mwaka 2018 kwa kumpiga Rofhiwa Nemushungwa.

“Lakini kwa mapambano ya nje nimeshinda mara nne, nimempiga bingwa wa Indonesia nikarudi na kikombe  nikaja nikampiga bingwa Uingereza na hao wengine na hiyo ni kwa sababu baada ya kujua ngumi zina faida na umuhimu gani.”

Mbali ya rekodi kubwa uliyonayo ila bado mashabiki hawakujui shida kitu gani?

“Binafsi namshukuru Mungu maana kufahamika nafahamika sana tena muda mrefu wakati ule tunacheza Derby ambazo zinajaza watu kweli.

“Nadhani mengine ni mitazamo ya watu ambao wengi wao wanachukua na mara zote wamekuwa wakisema hivyo kila ninapokuwa na pambano ila kama mashabiki ninao wa kutosha kutokana na namna uwezo wangu ulivyo ndani ya ulingo.

Kitu gani kikubwa umekipata kutoka kwenye ngumi?

“Nashukuru Mungu wakati napata mapambano ya nje nilifanikiwa kununua kiwanja Mbande Kisewe lakini bahati mbaya nikadhulumiwa na kesi ikafika mahakamani ila kutokana na mizunguko ya safari za nje, nikashindwa kufuatilia kesi.

“Kutokana na hivyo niliamua pia kusamehe ila sasa nashukuru Mungu, ngumi kwangu ni kazi ambayo ina mafanikio na kuweza kununua tena kiwanja huko Chamazi na kujenga nyumbani ambayo naishi na familia yangu.

“Binafsi nakosa vitu vingi sana, maana zamani sikuwa na usimamizi lakini sasa nipo chini ya HB Sadc Boxing Promotion, imani yangu nipo chini yao na vile vitu ambavyo navikosa basi naweza nikavipata.

“Kitu kikubwa kwa bondia kwa mwaka unatakiwa angalau upate mapambano manne au matatu lakini kwa kipindi fulani tulikuwa tunakaa mwaka au miaka miwili bila ya kupigana na mara nyingi inachangiwa na figisu za watu ambao wanakimbilia kwenye kigezo cha kudai tunataka pesa nyingi.

Kelele za huko mtaani wanasema hutaki kuongeza kilo, unapigana kwenye kilo za watoto?

“Kawaida kilo haziongezwi ila huwa zinaongezeka zenyewe maana kama ukiangalia kwa upande wangu kama sijafanya mazoezi huwa nafika kilo 60 na nikiwa nafanya ndiyo zinashuka hadi 55.

“Naweza kukupa mfano Seleman Kidunda alikuwa na kilo 97, lakini alitakiwa kucheza na Asemahle Wellem wa Afrika Kusini kilo 76  hivyo alivyokuwa akifanya mazoezi zilishuka hadi 76.

Kuna madai mabondia mnalogana wenyewe kwa wenyewe hasa kwa mapambano ya ndani?

“Ushirikina upo lakini kila mtu ana imani yake kwa sababu wapo wanaoamini hivyo na wapo wanaomwamini Mungu na wapo ambao wanaamini upepo na wengine miti yaani kila mmoja ana lake.

“Sijawahi kukutana na changamoto za kupigana halafu mpinzani simwoni ulingoni, ila kuna wakati nilikuwa najiandaa na pambano la ndani nilipata tatizo kubwa kabisa.

“Nakumbuka kuna siku nilikuwa nakimbia ‘road work’, nikafika maeneo ya Mabibo kwenda Ubungo kuna kitu kilinipitia ghafla lakini sikujua ni kitu gani ikasababisha hata kumeza mate siwezi na mwishowe hali yangu ikawa mbaya sana.

“Unajua hata niliyekuwa nakimbia naye hakuweza kuelewa kitu maana namwambia namna nilivyokuwa nimepata tatizo yeye akawa ananiona kawaida na kadri muda ulivyokuwa unakwenda sura yangu ilikuwa inavimba pamoja na mwili wote na kupumua ikawa shida.

“Tulijikongoja hadi kufika Gym ndipo mwalimu wangu aliniona na alishangaa nikamwelezea, wakanichukua na kunipeleka kwa shekhe, nikaombewa dua na kupewa makombe pamoja na mafuta maalum ya kupaka Mungu anasaidia nikarejea kwenye hali ya kawaida.

“Ukweli hayo mambo kwa Tanzania yapo ila upande wangu siamini sana kwa sababu nina imani yangu na sehemu ambazo nimezunguka na hiyo ndiyo sababu napenda sana kucheza na mabondia wa nje kuliko ndani.

Nini kilisababisha hadi kufikia kwenye rekodi za juu kwenye ngumi?

“Kwanza nilifika nafasi ya tano hadi namba sita duniani ila baada ya mtandao kucheza ndiyo nimeweze kufika hadi nafasi ya 19 duniani, Afrika bado nipo namba moja, Tanzania namba moja na kwenye uzani wangu ni namba moja.

“Lakini imepungua nusu nyota licha ya awali kuwa nne na nusu na uone kulivyokuwa na maajabu wakati nina nyota nne na nusu Ibrahim Class alikuwa na nyota mbili na nusu ila sasa ana tatu na nusu.

Abedi Zugo alikuwa na nne ila sasa ana tatu, Mwakinyo Hassani alikuwa na mbili na nusu ila ilivyocheza akapata tatu lakini amerudi kwenye mbili na nusu.

“Sijaelewa kwa sababu gani ila kwa upande wangu naona kukaa kwa muda mrefu imechangia maana katika uzito wangu kuna mabondia wengi ambao kila kukikacha wanapanda ulingoni.

Uliwezaje kumpiga Bongani?

“Unajua kwanza unatakiwa kushuru Mungu halafu kuna vitu kuvikubali na siyo mimi bali hata Watanzania walikubali, Bongani Mahlangu nilimtaka kwa sababu kuna vitu niliviangalia kutoka kwake kama uchezaji wake na jinsi alivyo.

“Nilisema kabisa Bongani hawezi kunipiga na kilikuwa kilio changu lakini Watanzania walikuwa hawakisikii na baada ya kupigwa Tony Rashid  walitolewa mabondia wanne nikiwemo mimi na wengine Ghana na walisema hawa ndiyo wanaweza kumpiga Bongani.

“Lakini ukweli sikupewa hiyo nafasi kabisa ingawa mwenyewe nilikuwa najua naweza kumpiga na kilio changu Mungu alikisikia wakatokea HB Sadc ambao waliamua kuwekeza kwangu.

“Waliniambia wananipa mapambano mawili na nikipoteza basi hawatafanya biashara na mimi, pambano la kwanza wakanipa Mfilipino nikampiga Mwanza na kisha nikamchapa Bongani.

“Nilifurahi kucheza na Bongani kwa sababu nilitaka kuwadhirishia Watanzania nipo na naweza ila bahati mbaya hatupewi nafasi na nilivyopewa nafasi nimeonyesha kile ambacho ninacho kupitia kwa Bongani.

“Bongani nilimkaribisha na tena akaongea sana maneno mabovu maana alisema hajawahi kupigwa na bondia mfupi katika maisha yake ngumi na siyo yeye hata baba yake pia na akawa na asilimia mia za kunipiga na mimi nikawa na asilimia za kumpiga yeye.

“Unajua asilimia 99 walikuwa wanajua naenda kupigwa na Bongani ila niliweza kuwaonyesha Watanzani, nataka niwaambie kuna mambo mazuri mengi yanakuja.

Nini kilipelekea kidole kimevunjika wakati wa pambano lako na Bongani?

“Sijui nini kilitokea ila najua nilimpiga ngumi ya kushoto ambayo nikajua kidole kimeteguka na hata nilivyorudi kwenye kona yangu nilimwambia kidole kimeteguka na akaniambia kama vipi niache nisiendelee lakini nilimwambia siwezi kuachia natamalizana naye.

“Lakini ilitokea raundi ya tatu kidole changu kilikuwa kimevunjika ila baada ya pambano na kufanya vipimo ndiyo nilijua kuwa kimevunjika maana mkono ulivimba sana,” anasema Majiha.

Related Posts