Mfumo wa wanachama unavyopoteza timu Ligi Kuu

Imebaki historia. Ndivyo unavyoweza kusema kuelezea maisha yanavyokwenda kasi hasa kwa timu zilizokuwa chini ya wanachama ambazo zilitisha miaka ya nyuma na sasa imebaki stori.

Hii ni kutokana na zama kubadilika hasa baada ya teknolojia mpya ya mfumo wa mabadiliko ya kiuendeshaji kuziacha nyuma timu ambazo zilitegemea nguvu ya wanachama.

Licha ya kwamba nguvu ya wanachama kubaki kuwa na faida, lakini siyo kutegemewa kwa mchango wa kila mwaka bali kujitoa katika sapoti ya kila mara. Mwanaspoti linakuletea baadhi ya timu zilizokuwa katika mfumo wa wanachama zilivyopotea kwenye ramani na kuziacha zile za  Ttaasisi, kampuni na binafsi kutawala soka la sasa.

Wakongwe hao walikuwa tishio miaka ya 1980 hadi kutwaa taji la Ligi Kuu 1986, lakini kwa sasa wanajikongoja katika Ligi ya Mkoa wa Mbeya. Timu hiyo yenye makazi yake katika Mji wa Tukuyu ilikuwa chini ya wanachama na ilizipa upinzani Simba na Yanga, lakini kwa sasa haina hili wala lile.

Hata msimu huu licha ya kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Mbeya, haikufurukuta kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilikoondoka patupu jijini Dodoma.

Bingwa wa Ligi Kuu 1967 kwa sasa anaendelea kujitafuta kwenye Championship tangu aliposhuka daraja 2002 na hana dalili za kurejea. Timu hiyo ya jijini Dar es Salaam ilikuwa katika mfumo wa wanachama na uhai wake ulitegemea zaidi michango ya wadau kwa kutembeza bakuli. Kwa sasa wakongwe hao hawapandi wala kushuka wakibaki Championship na muda mwingine First League, lakini yote ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia kwenye soka duniani.

Timu hiyo ya jijini Mwanza baada ya kushuka daraja msimu wa 2015/16 huenda ikapotea kabisa kutokana mfumo iliokuwa nao.

‘Wanakishamapanda’ hao wenye historia kwenye soka la Tanzania ni miongoni mwa timu zenye vitega uchumi  ikiwa na jengo katikati ya Jiji la Mwanza, lakini halina faida yoyote kwa klabu. Chama hilo ambalo muda wote haliishiwi vurugu kwa wanachama wake, imesababisha kupotea kwake katika ramani ya soka nchini kutokana na mfumo ilioutegemea wa kuchangia kwa wanachama.

Ilikuwa timu pekee mkoani Njombe ambayo iliwapa burudani wakazi wa mkoani humo kwa soka lake, lakini kwa sasa imebaki historia baada ya kupotea kwenye ramani za soka nchini.

Njombe Mji ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2016/17 kisha kushuka daraja msimu wa 2020/21 na haina dalili za kurejea tena kufuatia kushushwa madaraja hadi ngazi ya Wilaya.

Timu hiyo ilikumbwa na rungu hilo baada ya kutofika uwanjani kwenye mechi za First League kwa madai ya ukata na mtaji wake mkubwa ilitegemea nguvu ya wanachama wake kujichanga.

Kama ilivyokuwa kwa Toto Africans, Mbao FC nayo kwa sasa haipo kwenye ramani za soka kwani baada ya kushuka daraja msimu wa 2020/21 kupitia ‘play off’ imepotea. Timu hiyo ilipanda kikanuni ikiwa nafasi ya nne baada ya Geita Gold Mine (kwa sasa Geita Gol), JKT Kanembwa, Polisi Tabora na JKT Oljoro kushushwa daraja kwa tuhuma za kupanga matokeo. Mbao ilikuwa na mashabiki wengi jijini Mwanza na kuweka historia ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Simba jijini Dodoma ilifungwa mabao 2-1 ikiwa ni msimu wa kwanza ilipocheza Ligi Kuu. Kwa muda wote timu hiyo ilikuwa chini ya wanachama na tangu iliposhuka walimkabidhi kocha wa zamani wa Taifa Stars, Ammy Ninje aliyeahidi kuisuka upya, lakini sasa haisikiki.

Timu hiyo ilikuwa na utamu wake ilipotwaa Kombe la Muungano 1998, ikiwa kwenye nguvu ya wanachama waliokuwa wakiipa nguvu mwanzo mwisho.

Kwa sasa chama hilo la mjini Songea pumzi imekata na misimu miwili nyuma ilishindwa kusafiri kwa changamoto ya ukata hadi kushushwa daraja.

Ilifikia hatua ya wakongwe hao kuzuiwa hotelini Dar es Salaam kabla ya staa wa zamani na sasa Namungo, Erasto Nyoni kuokoa jahazi, lakini sasa imepotea.

Tangu ilipoanda msimu wa 2014/15, Stand United ilikuwa na nguvu kubwa ya wanachama mjini Shinyanga hadi kuipa jina la ‘Chama la Wana’ kutokana na sapoti waliyoipa timu hiyo.

Hata hivyo chama hilo lilijikuta katika mvutano baada ya kampuni moja kutaka kuweka mzigo kwa masharti ya kuibadili kuwa kwenye mfumo wa kampuni na kusababisha mgogoro hadi kujitoa kuidhamini.

Hali hiyo iliifanya timu hiyo kubaki kuwa na nguvu ya wanachama na kwa sasa waliokuwa wakiikingia kifua hawaonekani tena na timu imekuwa ya kushuka na kupanda ikiishia championship.

Walijulikana zaidi kama ‘Wana kimanumanu’ jijini Tanga wakishindana zaidi na ndugu zao, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ na kufanya jiji hilo kuwa na dabi ya kweli.

Kwa sasa timu hiyo ipo First League tangu iliposhuka msimu wa 2015/16 kwa mpigo sambamba na Mgambo Shooting na Coastal Union ambayo ilirejea tena na sasa inatesa Ligi Kuu. Hata hivyo, Coastal Union ndio timu pekee hadi sasa inayoendeshwa kwa mfumo wa wanachama japokuwa kuna mikono pia ya matajiri wanaoiwezesha.

Timu hiyo ya mjini Iringa kwa sasa imeacha historia tu kwani tangu ishuke daraja msimu wa 2019/20 haina dalili za kurejea ikikumbana na rungu la kushushwa daraja.

Wanapaluhengo waliocheza fainali ya FA msimu wa 2019/20 walikuwa wakiendeshwa na michango ya wanachama na sasa hakuna kinachoendelea.

Lipuli ilikuwa na upinzani mkali ikizipa wakati mgumu timu kubwa hasa Yanga, lakini baadaye ilikwenda na maji huku ukata ukitajwa kuchangia mkwamo wake.

Timu nyingine zilizokuwa chini ya wanachama ni Ashanti United (Dar es Salaam) ambayo imepotea, Pamba FC (Mwanza ambayo kwa sasa inamilikiwa na Halmashauri ya jiji hilo ikifahamika Pamba Jiji na sasa imerejea kwa nguvu ya halmashauri hiyo jiji).

Mtaalamu wa uongozi wa michezo, Fredrick Masolwa anasema timu za wanachama zinapotea kwa sababu tofauti ikiwamo kuwa mbali na mfumo wa uendeshaji, lakini  pia uwazi na ubinafsi wa baadhi ya viongozi ni tatizo.

Anasema zamani kulikuwapo na ushirikishwaji kwa wanachama katika mikutano ya mapato na matumizi, lakini hayo yote yamepotea na imebaki kuwa vikundi vya watu fulani na kufanya mashabiki kusubiri matokeo viwanjani.

“Hata mfumo mabadiliko ya uendeshaji unaweza kuwa na faida au hasara kama hautawekwa mpango mkakati endelevu kuliko kumtegemea mtu binafsi, mfano hai ni Coastal Union na wala si wengine,” anasema Masolwa.

Naye Kulwa Bundala anasema pamoja na faida ya mfumo wa uendeshaji wa kampuni kuwa na faida, lakini asilimia kubwa huzibeba timu zenye mashabiki wengi akitaja mfano wa Yanga na Simba.

“Mwekezaji yeyote kwenye soka lazima aangalie faida atakayoipata kwa kile anachokiweka. Hili litasaidia timu kuwa imara lakini litazibeba timu kubwa tunaona namna Simba na Yanga zilivyo,” anasema.

Related Posts