HAIJAISHA hadi iishe ndiyo kauli wanayoishi nayo timu ya Mtibwa Sugar huku matumaini yao makubwa yakiwa ni kwamba msimu ujao wataendelea tena kukiwasha Ligi Kuu ya NBC licha ya kwamba hivi sasa wana hali mbaya.
Timu hiyo yenye maskani yake Turiani mkoani Morogoro, imepata matumaini hayo baada ya leo Mei 9, 2024 kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye viunga vyao vya kujidai, Manungu Complex.
Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili katika kujinasua na janga la kushuka daraja ambapo kabla ya leo Mtibwa Sugar ilikuwa nafasi ya 16 kwenye msimamo baada ya mechi 25 na alama 17 huku Tabora United ya 15 ikikusanya alama 23 katika michezo 25.
Waliofufua matumaini ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo huo ni Jimyson Mwanuke aliyefunga bao la kwanza dakika ya 15 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Charles Ilanfya ambaye naye alifunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 56 akimalizia pasi ya Seif Karihe huku lile la tatu likifungwa na Nickson Mosha dakika ya 79.
Kivutio kikubwa katika mchezo huo alikuwa kiungo mshambuliaji wa Tabora United, Najim Mussa ambaye alionekana kuwa maeneo muhimu uwanjani muda wote hadi mwisho.
Kubwa zaidi ambalo watazamaji waliofika uwanjani hapo liliwashangaza ni kitendo cha timu hizo kuwahi kurudi uwanjani kipindi cha pili kabla ya waamuzi jambo lililotafsiriwa kwamba kila mmoja alikuwa akiitaka mechi.
Ushindi wa leo kwa Mtibwa Sugar ulikuwa na maana kubwa sana baada ya kucheza mechi sita sawa na dakika 540 bila ya ushindi kwani mara ya mwisho kupata alama tatu ilikuwa Machi 9 mwaka huu walipoifunga Tanzania Prisons mabao 2-1.
Baada ya hapo wamecheza michezo sita mfululizo bila ya ushindi wakifungwa minne dhidi ya KMC (1-0), JKT Tanzania (2-1), Simba (2-0) na Azam (2-0), huku sare mbili dhidi ya Kagera Sugar (0-0) na Geita Gold (2-2).
Licha ya Mtibwa Sugar kupata ushindi huo lakini wameendelea kuzibeba timu zingine 15 kwa kusalia mkiani mwa ligi hiyo ambapo mpaka sasa wamekusanya alama 20 baada ya michezo 26 huku wakiwa wamefungwa mabao 43 wao wakifunga 26. Tabora United nao wamesalia nafasi ya 15 wakikusanya alama 23 wakicheza mechi 26.
Kocha wa Tabora United, Masoud Djuma amesema wachezaji wake hawakucheza kwenye kiwango bora ndiyo maana timu yake imepoteza mchezo huo ambapo ameahidi kurejea kufanya vizuri mechi nne zilizosalia.
“Hatukuwa kwenye ubora wetu ndiyo maana tumepoteza mchezo huu, wapinzani wetu Mtibwa walikuwa bora kuliko sisi, tulimiliki eneo la kiungo lakini hata zile nafasi chache tulizotengeneza hatukuzitumia hivyo tunaenda kujipanga ili mechi zilizobaki tufanye vizuri na timu imalize ligi kwenye nafasi salama.”
Kocha wa Mtibwa, Zuberi Katwila amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma ambapo amesema ushindi huo unawapa kujiamini kuelekea mechi za ligi zilizobaki huku akisisitiza kuwa timu yake bado inahitaji kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
“Nawapongeza wachezaji kwa kujituma na kupata matokeo haya, huu mchezo ulikuwa muhimu kwetu sote maana hatupo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, lakini tumeshinda, ushindi huu unatupa kujiamini ili tuweze kushinda michezo iliyobaki, hatujakata tamaa lolote linaweza kutokea na kwa mechi nne zilizobaki tutacheza kufa au kupona ili ligi ikimalizika tuone tutakuwa wapi maana malengo yetu bado ni kucheza ligi kuu kwa msimu ujao.”
Mechi nne zilizobaki kwa Mtibwa Sugar itacheza dhidi ya Yanga (Mei 13 nyumbani), Namungo (Mei 20 nyumbani), Mashujaa (Mei 25 ugenini) na Ihefu (Mei 28 ugenini).
Tabora United wao mechi nne zilizosalia watacheza dhidi ya Mashujaa (Mei 12 nyumbani), Ihefu (Mei 20 nyumbani), Yanga (Mei 25 ugenini) na Namungo (Mei 28 ugenini).