Kibaha. Mwili wa mwanafunzi Angel John anayedaiwa kuuwawa na kisha kutumbukizwa kwenye shimo la choo umezikwa.
Angel aliyekuwa akisoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Carisa mjini Kibaha alipotea Mei 6, 2024 alipomfuata dada yake aliyekuwa ameenda kusuka jirani na makazi yao.
Mwili wake ulipatikana Mei 7, 2024 ndani ya shimo la choo akiwa amefariki dunia.
Mazishi yamefanyika leo Mei 9,2024 kwenye makaburi ya Mwendapole Kibaha mkoani hapa, yakiwa yametawaliwa na simanzi kwa ndugu jamaa na marafiki waliohudhuria ibada na hata makaburini.
Wakati watu mbalimbali wanatoa heshima za mwisho kanisani baada ya mahubiri yaliyotolewa na Mchungaji wa Kanisa Anglikana Tumbi Kibaha, Exavia Mpambichile mama mzazi wa mwanafunzi huyo alishindwa kuaga mwili wa mwanaye.
Mchungaji aliyeongoza mahubiri Exavia Mpambichile amesikika akisema “Kama mama mzazi ameshindwa kustahimili kutoa heshima za mwisho kwa mwanaye mwacheni.”
Akitoa salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Muhidini Muhidini amewataka wananchi wa maeneo hayo kushirikiana kwenye masuala ya ulinzi ili kudumisha usalama.
“Nawaomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake atambue kama kuna mgeni ameingia asisite kutuletea taarifa ili tumtambue anakotoka na mwenyeji wake nani,”amesema.
Mapema leo Mei 9, 2024 taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa mwanafunzi huyo aliuawa kisha kutumbukizwa kwenye shimo hilo la choo.
Alisema jeshi hilo linaendelea na msako kumpata mtu au watu waliohusika na mauaji hayo, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi umebaini mtoto huyo aliuawa na kisha kutumbukizwa kwenye shimo hilo, tofauti na taarifa iliyotolewa awali,” inaeleza taarifa hiyo.”
“Hivyo, Jeshi la Polisi limeshaanza msako kuwatafuta watu au mtu aliyehusika na tukio hilo,” ilieleza taarifa hiyo.