Samia: Mradi Liganga, Mchuchuma uanze

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara na ya Mipango na Uwekezaji kukamilisha mchakato wa kuipata kampuni itakayowezesha kuanza kwa mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Kuanza kwa mradi huo uliopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe haraka kunalenga kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya kiwanda cha kuunganisha magari makubwa cha Saturn Corporation Limited, kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam na vingine.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho leo, Samia amesema zipo malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa magari ikiwemo vioo na vyuma.

Kufuatia suala hilo amesema tayari Kiwanda cha vioo kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kimepewa ruhusa na ithibati ili waweze kutumia malighafi iliyopo eneo la Engaruka mkoani Manyara ambako kuna magadi soda.

“Hivyo nikuombe Waziri wa Viwanda na mwenzako wa Uwekezaji, malizieni suala la Liganga na Mchuchuma, tupate kampuni bora itakayoanza kuchimba chuma ile ili iwe malighafi katika viwanda hivi, niwaombe sasa hili limaliziwe kwa haraka,” amesema Samia.

Maagizo haya ya Samia yanakuja wakati ambao kumekuwapo na msukumo kutoka kwa watu mbalimbali juu ya kutaka utekelezaji wa mradi huo kuanza kutokana na faida zake lukuki.

Hili pia linasemwa wakati ambao Sh15.4 bilioni zilishatolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi na taasisi mbalimbali 1,142 ili waweze kupisha mradi huo.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika mwaka 2013 kuhusu uwepo wa madini hayo ziligundua uwepo wa tani milioni 428 za makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140  na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 kinachoweza kuchimbwa kwa miaka 58.

Mradi huu ni miongoni mwa ile ya kimkakati ya nchi huku baadhi ya wadau wa maendeleo na wanasiasa akiwemo Zitto Kabwe, amewahi kunukuliwa na gazeti la hili akisema mradi huo una masilahi makubwa kwa Taifa.

“Tuwe madarakani, tusiwe madarakani tutaendelea kuisema Njombe hasa mradi wa chuma kwa sababu ni muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Inashangaza tunaagiza chuma kutoka nje ya nchi wakati kimelala Ludewa,” alinukuliwa Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo Mei 29 mwaka jana na hatimaye leo ikiwa ni siku 20 kabla ya kauli yake kutimiza mwaka mmoja, mwanga unaanza kuonekana juu ya mradi huo.

Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka Watanzania ikiwemo kampuni kuchangamkia fursa za uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vingine.

Hiyo ni baada ya kubainisha kuwa, kiwanda cha kuunganisha magari alichokifungua kinatumia vipuri 2,400 kwa gari moja, lakini kwa sasa vingi vinatoka nje ya nchi huku akieleza kuwa suala hilo si afya kwa ukuaji wa viwanda.

“Binafsi naiona fursa kubwa sana kwa Watanzania, tunaweza kunufaika zaidi kupitia uwekezaji wa viwanda vingine vya uzalishaji wa vipuri vya magari mitambo pamoja na kuongeza ajira na mapato kama nilivyosema mwanzo,” amesema.

Alitumia kauli hiyo kuitaka wizara ya viwanda kuhakikisha inaunganisha mnyororo wa thamani ili viwanda viweze kusomana, kujua nani anazalisha nini na kiwanda kimoja kinaweza kusaidia vipi kingine.

Related Posts