SERIKALI imepunguza kodi ya makampuni kwa asilimia 20, kutoka asilimia 30 hadi 10, kwa kipindi cha miaka mitano ya mwanzo, lengo likiwa ni kuchochea uwekezaji katika sekta ya viwanda. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Hayo yamesemwa leo tarehe 9 Mei 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua kiwanda cha kuunganisha malori na matipa cha Saturn Corporation Limited, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa nchi amesema Serikali yake itaendelea kujenga uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindanishi katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Rais Samia amesema sekta hiyo inaongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi na kukuza uchumi jumuishi na kusaidia kuondoa umasikini.
Kuhusu kiwanda hicho cha kuunganisha malori, Rais Samia amesema bidhaa zitakazozalishwa zinasaidia kupunguza gharama pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja 250 na zisizo za moja kwa moja 1,800.