Geita. Ni takribani umbali wa kilomita 35 kutoka Geita mjini, mwendo wa dakika 50 hatimaye msafara wa wadau wa elimu unawasili katika Shule ya Sekondari Bung’wangoko.
Ziara ya wadau hao shuleni hapo ni shamrashamra za maadhimisho ya Juma la Kimataifa la Elimu (Gawe) linaloadhimishwa mkoani Geita.
Kama ilivyo ada ya Waafrika mgeni anapofika anakaribishwa kwa ukarimu, hivyo ndivyo ilivyofanyika kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo waliwapokea wageni kwa shangwe na vigelegele na burudani mbalimbali.
Kati ya burudani nyingi zilizotolewa ni igizo la wanafunzi lililogusa hisia za wengi, hasa katika nafasi ya muhusika mkuu iliyoigizwa na Elizabeth Ernest mwanafunzi wa kidato cha kwanza.
Maudhui ya igizo hilo lilikuwa ni mimba na ndoa za utotoni namna inavyowaathiri watoto wa kike katika jamii ya kisukuma ambao ni miongoni mwa wenyeji wa Mkoa wa Geita.
Kujiamini na uwezo wake wa kujielezea kwenye hadhira ilionyesha dhahiri kuna kitu cha ziada ndani ya binti huyu.
Nilipozungumza naye ndipo nilipobaini kwamba nilikuwa sahihi, binti huyu ni miongoni mwa wasichana wenye kiu kubwa ya kupata elimu na yuko tayari kufanya lolote kutimiza azma hiyo.
“Huwa nafurahi nikiwaona watumishi wakiwa wamependeza wanaenda kazini, naamini hata mimi naweza kuwa kama wao ndiyo maana naweka nguvu darasani nikijua njia pekee itakayoniwezesha kufanikisha hilo ni elimu,” anasema Elizabeth.
Binti huyu wa miaka 18, ni miongoni mwa wasichana waliokumbana na kadhia ya kutakiwa kuolewa wakiwa na umri mdogo, lakini alifanikiwa kuvuka kiunzi hicho.
Baada ya kumaliza darasa la saba akiwa na miaka 11, familia yake ikapanga mpango wa kumuozesha kwa mojawapo ya wazee katika kijiji anachoishi, kutokana na kile kilichoaminika kwamba safari yake ya elimu imeishia hapo kinachofuata ni kuanzisha familia.
Elizabeth hakukubaliana na uamuzi huo kwa kuwa aliamini ndoto zake haziwezi kutimia endapo angekubali kuolewa, hilo likamsababishia kutoroka nyumbani.
“Sikukubaliana na uamuzi wa kuolewa nilikuwa mdogo kiumri ingawa kimwonekano nilionekana mkubwa, sikukubali kwa sababu niliamini nina safari ndefu ya elimu ili kutimiza ndoto zangu.”
“Nikafikia uamuzi wa kutoroka kwenda Mwanza. Kwa kutumia fedha za ujira niliopata kutokana na vibarua vya kulima nilifanikiwa kupata nauli iliyonifikisha Mwanza.
“Si kwamba nilikuwa nafahamu naenda wapi na kufanya nini, ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika Mwanza na nilipofika stendi sikuwa na uelekeo. Nilikutana na mwanafunzi nikamsimulia mkasa wangu akaniambia niende nyumbani kwao,”anasema Elizabeth.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya ya binti huyu, aliishi kwenye familia hiyo mpya hadi pale walipomtafutia kazi za ndani jijini Mbeya.
Uchapakazi na uaminifu mkubwa alioonyesha kwa bosi wake ulimfanya kumpandisha kutoka mfanyakazi wa ndani hadi kuwa mhudumu wa dukani.
“Yule bosi wangu alikuwa mama mwenye upendo, alivutiwa na namna ninavyofanya kazi akajenga uaminifu mkubwa kwangu, haikuchukua muda mrefu akaniingiza ndani kwenye sehemu ya fedha nilifanya kazi yangu kwa ufanisi mkubwa,”anasema.
Anasema baada ya kukaa nje ya mfumo wa elimu kwa takribani miaka minne, siku moja alifika mteja ambaye aliguswa na uwezo wake kiakili na kuanza kumuhoji.
Anasema, ”kuna mzee mmoja alikuwa anakuja dukani, siku moja akaanza kunihoji kwa nini nipo hapo na sio shuleni nikamueleza mkasa niliopitia na alionekana kuguswa mno.
“Yule mzee akaanza kuniambia kuhusu tamko la Serikali la kuwaruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni, akawa ananionyesha video mtandaoni na kuniuliza kama naweza kurejea shuleni na kunishawishi nirudi nyumbani. Nikamwambia niko tayari na akanilipia ada nisome masomo ya ziada kabla ya kurudi shuleni,”anasema.
Huo ukawa mwanzo mpya wa maisha ya Elizabeth, baada ya kujengwa kifikra, mzee huyo alimsaidia pia kupata nafasi katika shule ya msingi kwa kurudia darasa la sita akiwa na miaka 16.
Haikuwa rahisi kwa jamii kumpokea Elizabeth hasa kutokana na umri wake kutoendana na mwanafunzi wa darasa la sita, alikutana na kila aina ya udhalilishaji na kukatishwa tamaa.
Anasema, “Nilikuwa naambiwa maneno ya kukatisha tamaa kwamba umri na mwonekano wangu haustahili kuwepo shuleni, natakiwa niolewe lakini kwa kuwa nilifahamu lengo langu ni lipi sikuwayumbishwa na maneno hayo.
“Niliendelea na shule hatimaye nikamaliza elimu ya msingi nikiwa na miaka 17 na nikafanikiwa kufaulu vizuri, nilipata A tano na B mbili nikachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Bung’wangoko,”anasema.
Januari 2024 akaanza safari yake ya elimu ya sekondari akiwa na hofu ya namna atakavyopokelewa lakini bahati ilikuwa upande wake walimu na wanafunzi wenziye walimpokea vyema.
Changamoto pekee ambayo amebaki nayo ni namna jamii inavyomtazama na kuendelea kumkatisha tamaa kwamba umri wake hatakiwi kuchangamana na wanafunzi wengine bali aolewe.
“Wananiambia mimi ni mzee sitakiwi kujichanganya na wanafunzi, sehemu pekee ninayotakiwa kuwepo ni kwenye ndoa, sikubaliani na wanachokisema na ndiyo sababu sijali nasimamia kile ninachokiamini.
“Nataka kuwa muuguzi wa hospitali, naamini ili kutimiza ndoto hiyo ni lazima nisome hivyo hakuna namna naweza kuacha shule kwa sababu ya maneno ya watu, nitasoma na nitahitimu masomo yangu,”anasema.
Elizabeth anawasihi wasichana wengine kutokubali kukatishwa tamaa kwa namna yoyote ile na badala yake wasimamie ndoto zao, kwa kuweka kipaumbele kwenye elimu.
Akimzungumzia mwanafunzi huyo, Mkuu wa shule hiyo, Jackson Barnabas anamtaja Elizabeth miongoni mwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma.
“Anafanya vizuri darasani, kwa kifupi ni mwanafunzi ambaye anafundishika na kuelewa anachofundishwa ndani ya muda mfupi, ingawa tunaona kuna changamoto anazokutana nazo nyumbani.”
“Kwenye jamii ya kisukuma mwamko wa elimu uko chini hasa kwa watoto wa kike, hivyo kuna mazingira ambayo anakutana nayo kwa namna moja au nyingine yanampa vikwazo ila anapambana,”anasema mwalimu huyo.