TANZANIA Commercial Bank BANK (TCB) imefanya mapinduzi yanayolenga Vikundi vya kuweka na kukopa yaani Vikoba ili kumwezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kukopa Kidijitali ndani ya Kikoba kidigitali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, huo leo Mei 09, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Benki, Adamu Mihayo amesema kuwa Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali, kwani Kikoba inabeba dhana pana ya uwazi, ujumuishi na usalama katika uwekaji wa akiba na usimamizi bora wa kifedha.
Amesema kuwa Maendeleo ya kiteknolojia yanayoyashuhudiwa yamewafanya watu wengi kuwa wajuzi wa mambo ya kidijitali na kuunganishwa pamoja. Hali hii imebadilisha namna wateja wengi wanavyofanya miamala na kutumia huduma za kibenki.
“Mabadiliko haya yameisukuma sekta ya kibenki kuwekeza katika teknolojia mbalimbali ili kumpa mteja suluhisho la huduma za kibenki za kuaminika na salama.
“Tukitumia nyenzo hi ya teknolojia tunaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua na kujitegemea.” Ameeleza
Mihayo ameeleza kuwa Mapinduzi haya yataboresha dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka akiba na kukopeshana.
“Tunawasogezea wateja wetu huduma hii viganjani wao ikiwa na ufanisi zaidi na urahisi maradufu. Ubunifu huuni hatua muhimu katika sekta ya kibenki katika ulimwengu huu wa kidigitali.” Amefafanua
“Kikoba” ni neno lililotoholewa kutoka katika jina VICOBA yaani vikundi vya kuweka akiba pamoja. Huduma hii sasa inapatikana kiurahisi kupitia simu ya mkononi. TCB Benki imeshirikiana na kampuni zote za simu nchini zikiwemo Tigo, Airtel, Halotel, na Vodacom ili kurahisisha namna ya kusajili na kujiunga na Kikoba mtandaoni.
Ukiwa na Kikoba mtandaoni ni salama zaidi, ni rahisi kuona miamala yako, na inaleta uwazi kati ya kikundi chenu cha Kikoba.
Amesema kuwa Kutakuwa na aina mbili za Vikoba yaani Kikoba cha kawaida ambacho Kwa mara ya kwanza katika historia, mteja ataweza kusajili au kujiunga na Kikoba kupitia mtandao wake wa simu kwa kupiga code fupi tu. Kwa mfano: Tigo Kikoba (*150*01 #), Airtel Kikoba (*150*60#), Halotel Kikoba (*150*21 #), na M-Koba ya Vodacom (*150*00# ). Kwa Kikoba hiki, mtu ana uwezo wa kusajili Kikoba na marafiki na familia walio kwenyem tandao mmoja.
Aina nyingine ni Kikoba Mix Kikoba hiki hakizingatii mitandao yao, Kikoba Mix inawawezesha watu kutoka mitandao tofauti kuunganika pamoja na kuunda Kikoba kwa namba zao. Na ili ufungue Kikoba Mix, piga *150*21# upelekwe moja kwa moja kwenye menyu ya TCB, na fuata maelekezo rahisi.
Uzinduzi wa Kikoba unakuja katika wakati huu ambapo watu wengi wanatamani kuwa na Uwezo wa kuamua namna na wakati wa kufanya miamala yao.
TCB Benki ikiwa benki inayoelewa mahitaji wa wateja wake imejikita katika kuleta mapinduzi ya kidigitali katika huduma za kibenki kwa kuzindua huduma hi ya KIKOBA itakayowanufaisha kiuchumi wateja wake na Watanzania wote kwa ujumla.