WANAFUNZI GEITA WAWEKA BAYANA SABABU ZINAZOCHANGIA UTORO

 

Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala akisalimiana na Wanafunzi wa Sekondari ya Bung’wangoko ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa inayoendelea mkoani Geita na wadau wa elimu.



Wadau wa elimu pamoja na wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) wakiwa katika ziara kutembelea shule mbalimbali mkoani Geita.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bung’wangoko wakiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yanayoendelea mkoani Geita na wadau wa elimu.


Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala akizungumza katika moja ya ziara za wadau wa elimu wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yanaoendelea mkoani Geita.


Wadau wa elimu pamoja na wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) wakiwa katika ziara kutembelea shule mbalimbali mkoani Geita.


Wadau wa elumu na wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) wakiwa katika mkutano na wazazi, wanafunzi, viongozi na walimu katika Shule ya Msingi Chabulongo.


Na Joachim Mushi, Geita

BAADHI ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chabulongo na Sekondari ya Bung’wangoko wamesema miongoni mwa sababu zinazowafanya washindwe kuhudhuria shuleni mfululizo ni kushinda na njaa wawapo shuleni. 

Wakizungumza katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, kwenye mikutano ya Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa inayoendelea mkoani Geita na wadau wa elimu wamebainisha kuwa kushinda na njaa shuleni kunachangia utoro kwa baadhi ya wanafunzi.

“…Fikiria unafika shuleni saa 12 asubuhi unakaa kuanzia muda huo hadi saa 12 jioni unaporudi nyumbani, unashinda njaa na unaendelea kufundishwa na baadhi yetu tunatembea umbali mrefu kuja na kurudi shuleni ndio maana unajikuta unakata tamaa mapema na kuanza utoro,” alisema mmoja wa wanafunzi kidato cha tatu Sekondari ya Bung’wangoko.

Aidha pamoja na changamoto hiyo baadhi ya wanafunzi wameeleza kuwa wanalazimika kutohudhuria masomo mfululizo kwa kuwa wapo wazazi ambao huwazuia kuja shule na kuwatumia katika shughuli za mashambani, kama kilimo pamoja na uvunaji wa mazao. 

Mdondoko wa wanafunzi kuacha shule ni mkubwa katika Sekondari ya Bung’wangoko, kwani kwa mujibu wa taarifa fupi ya shule hiyo, liyotolewa kwa wadau wa elimu kwenye Juma la Elimu, kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2023 hadi Machi 2024 jumla ya wanafunzi waliotoweka ni 89 kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala akizungumza na wadau wa elimu mara baada ya majadiliano na wazazi, walimu, wanafunzi, viongozi na washiriki wengine wa Maadhimisho ya Jumla la Elimu leo, katika Sekondari ya Bung’wangoko amewataka wazazi kukubali kuchangia chakula cha watoto wao mashuleni ili kupunguza changamoto ya utoro.

Pamoja na hayo, amewataka wazazi kushirikiana na viongozi maeneo yao na wadau wengine kujenga mabweni kwa wanafunzi ambao hutembea umbali mrefu na kukutana na changamoto kadhaa zinazowafanya washindwe kumaliza masomo yao. 

“Ni haki ya mtoto kupata elimu bila vikwazo, tuache kuwakatisha masomo watoto kwa kuwatumikisha shughuli za kilimo kipindi cha masomo…walimu wamesema katika vikao wapo baadhi ya wazazi hufika shuleni na kuomba ruhusa ya mtoto kuacha kuja shule msimu wa mavuno ili tu akasaidie kuvuna mazao shambani hasa watoto wa kike hii sio sawa,” alisema Bi. Martha Makala akizungumza na wadau wa elimu.

“Kipindi cha mavuno watoto wanatega kwenda shule wakisingizia wanakwenda kufanya kazi mashambani, tuache kuwatumia watoto mashambani huku tukijua wanastahili kuwa shuleni na kuendelea na masomo, tusiwakatishe watoto kwenda shuleni kwa kisingizio wanaenda kuvuna mashambani,” alisisitiza Mratibu huyo wa Mtandao wa Elimu Tanzania.

Related Posts