AKILI ZA KIJIWENI: Hasira za Gamondi zipo kwa wengi

JUZI pale Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ilikuwa imebaki kidogo watu waone Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akimchapa vibao refa Abdallah Mwinyimkuu.

Ilikuwa ni baada ya kumalizika kwa mechi baina ya timu yake na Kagera Sugar ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kocha huyo raia Argentina alionekana kutofurahishwa na uamuzi wa kukataa bao la Joseph Guede kwa kile kilichotafsiriwa na mwamuzi msaidizi ameotea lakini picha za marejeo ya runinga zinaonyesha mfungaji hakuwa ameotea.

Kiuhalisia hakuna kocha au mtu yeyote ambaye anapenda au kufurahia kuona timu yake inakataliwa bao linaloonekana halali kwani inatumia nguvu na rasilimali nyingi katika maandalizi.

Lakini badala ya kutaka kuwapiga marefa, njia sahihi ni kuungana kwa pamoja na kukemea makosa ya kizembe ya waamuzi, pia kuzihamasisha mamlaka ziboreshe viwango vya marefa.

Kilichotokea sio jambo geni na tayari wapo wengi walioathirika na uchezeshaji usioridhisha wa marefa kama ambavyo imetokea kwa bwana Miguel Gamondi.

Huyo huyo Gamondi na timu yake wamewahi kunufaika na makosa hayo ya waamuzi kwa nyakati tofautiĀ  kama ilivyotokea katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar pale wapinzani wao walipokataliwa bao lao halali.

Sasa dawa sio kupigana vita hii mwenyewe na badala yake kunapaswa kuwe na nguvu zilizokusanywa kwa pamoja ili wahusika waone uzito wake.

Marefa nao wajitahidi kuchezesha vizuri aiseeeh ili kuepuka kujiweka matatizoni kwa kufungiwa au kupigana kama kilichotaka kutokea kwa Gamondi.

Related Posts