DC James ashangaa udumavu wilaya yenye vyakula tele

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James amesema tatizo la udumavu kwenye wilaya hiyo halitokani na uhaba wa vyakula isipokuwa mpangilio mbovu wa ulaji.

Amesema ni aibu kuitwa mkuu wa wilaya kwenye eneo lenye vyakula vya kutosha lakini udumavu ni mkubwa.

James amesema hayo jana Mei 9, 2024 kwenye maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Tarafa ya Kiponzelo iliyolenga kutafuta soko la mazao yao pamoja na kubadilisha fikra ya jamii kuhusu ulaji.

Shirika la World Vision kupitia mradi wake wa Kihanga, unaotekelezwa Tarafa ya Kiponzelo umefanikiwa kuwekeza kwenye kilimo cha mbogambo, matunda, maharagwe, ufugaji wa samaki na uundwaji wa vikundi vya kiuchumi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, James amesema mazao wanayozalishwa na wananchi hao yasaidie kupambana na udumavu badala ya kuuza yote.

“Mnafahamu mtu mwenye udumavu hata uwezo wa kufikiri unapungua? Udumavu hauathiri mwili peke yake hata uwezo wa kufikiri unaathirika. Mnataka tutengeneze kizazi cha aina gani? Hapana, hakuna sababu ya kuwa mkuu wa wilaya na udumavu huu.

“Uwezo wa kuondoka kwenye udumavu tunao, vyakula hivi hivi mnavyoonyesha leo ndio tuvitumie kupata lishe bora kwetu na watoto wetu,” amesema.

Akitoa mfano, James amesema watu wengi hudhani nyanya ni kiungo cha mboga na sio tunda.

 “Msingoje kukutana na nyanya kwenye mchuzi, nyanya ni matunda. Wafundishe wanao (watoto) kuwa nyanya ni matunda, akila nyanya ina virutubisho kama matunda mengine,” amesema.

James amesema vita ya udumavu haihitaji fedha nyingi isipokuwa mtizamo chanya kuhusu ulaji wa vyakula vinavyopatikana kwenye maeneo yao.

“Vyakula hivi mnavyoonyesha ndivyo vitasaidia kwenye mapambano ya udumavu, kila kitu kipo hapa, tule kwa mpangilio. Nyama, matunda, samaki, mbogamboga, vyote mnavyo hapa,” amesema Herry.

Awali, Meneja wa World Vision Kanda ya Kati na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Pudensiana Rwezaula amesema baada ya utafiti kuonyesha mikoa yenye vyakula vya kutosha ndiyo yenye tatizo la udumavu, waliamua kuja na mradi wenye uwezo wa kubadilisha fikra.

Amesema mbali na uwekezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya kilimo, walifanikiwa kuwafundisha kuwa wanazungukwa na rasilimali ambazo wakizitumia ipasavyo zitaweza kuwafanikisha kiuchumi.

Awali, baadhi ya wananchi wa Kiponzelo wamesema tofauti na zamani, kwa sasa mazao wanayozalisha yanaanza kutumika kwanza nyumbani.

“Napeleka matunda sokoni lakini kwanza watoto wangu wanakula, mtizamo kuhusu maisha yetu umebadilika,” amesema Erick Paul, mkazi wa Kiponzelo.

Related Posts