Dk Tulia ataka mifuko ya hifadhi ya jamii inayowacheleweshea wastaafu mafao ibanwe

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kupeleka bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Wastaafu ili kuweka riba kwa mifuko ya hifadhi ya jamii inayochelewesha mafao kwa wastaafu.
Dk Tulia alisema hayo jana baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko.
Sekiboko katika swali lake alisema wapo wastaafu wa Mfuko wa Taifa wa Pensheni kwa Wafanyakazi walipelekwa katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) baada ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuunganishwa mwaka 2018.
Alisema hadi leo wapo watumishi wanaodai mafao yao, akitaka kufahamu nini kauli ya Serikali kuhusu madai hayo.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema rekodi zao zinaonyesha mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kuunganishwa imelipa madeni zaidi ya asilimia 78 na kiasi kilichobaki kinaendelea kuhakikiwa.
Alisema sehemu ya madeni ambayo bado hayajalipwa ni kutokana na usahihi wa nyaraka lakini wale wote ambao, nyaraka zao zilikuwa hazina dosari wameshalipwa.
Baada ya majibu hayo, Dk Tulia alisema wastaafu wanaostaafu hivi sasa wanasubiri miezi mitatu na wengine 12, kulipwa mafao yao. Alisema lengo la kuwepo kwa mifuko hiyo ni kumwekea mstaafu mazingira ya kutoshuka kwa maisha aliyokuwa anaishi kabla ya kustaafu.
Spika alisema mstaafu akikaa miezi sita bila kulipwa wakati alitakiwa kulipwa malipo yake mara anapostaafu wanamfanya kuishi katika mazingira magumu.
“Sasa anatakiwa afanye nini ili alipwe kwa maana sisi wabunge simu zetu zimejaa sms (ujumbe mfupi wa maneno). Mmejipanga vipi ili mtu anapostaafu apate mafao yake,” alihoji Spika Tulia.
Naibu Waziri Katambi akijibu swali hilo alisema wamejipanga na jambo hilo kwa kufanya uboreshaji, akieleza hivi sasa taarifa za wastaafu wanaoelekea kustaafu zinaandaliwa mapema, miezi sita kabla ya muda wa kustaafu.
Alisema suala la wastaafu kudaiwa kupeleka nyaraka limebaki kuwa ‘zilipendwa’ akieleza hulipwa mafao yao ndani ya siku 60 baada ya kustaafu.
Hata hivyo, alisema wasiolipwa baada ya siku hizo ni wale ambao wana dosari zilizo wazi.
Katambi alisema katika ofisi zao, hawana taarifa za ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu.
Aliwaomba wabunge walio na taarifa kuhusu ucheleweshaji wampelekee ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Baada ya majibu hayo, Dk Tulia alisema kama sheria hiyo inatoa adhabu ya riba kwa waajiri ambao wanachelewesha michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii, basi sheria hiyo iweke riba kwa mifuko ya hifadhi ya jamii inayochelewesha mafao kwa kuwa iko kimya.
“Nitegemee sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria ili nayo (mifuko ya hifadhi ya jamii) iwekewe riba inapochelewesha mafao ya wastaafu. Wakibanwa watahakikisha wanalipa fedha za wananchi kwa wakati,” alisema.

Kikokotoo bado moto
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda alihoji Serikali iwapo haioni haja ya kufanyia marekebisho kanuni ili wastaafu waweze kulipwa mafao yao waliyofanyia kazi.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema Serikali ilishafanya utaratibu kuwezesha kufanya tathimini ili kuangalia ni jinsi gani inaweza kuwanufasha wastaafu.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro alihoji Serikali ina mpango gani wa kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuongeza ukwasi na wastaafu waendelee kunufaika na unachama.
Naibu Waziri Katambi alisema kulikuwa na madeni yaliyorithiwa na Mfuko wa PSSSF ambayo yalitokana na wafanyakazi kutochangia katika mfuko wa PSSF kabla ya mwaka 1999.
Alisema Serikali iliamua kubeba deni la Sh4.6 bilioni ambalo tayari wameshaanza kulipa kupitia hati fungani ya Sh2.176 bilioni.
Alisema pia kulikuwa na deni la Sh430 bilioni ambalo ni la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambalo jana Katibu Mkuu wa Hazina alifanya kikao na mfuko huo.
Katambi alisema fedha zimeshasainiwa na deni litakwenda kulipwa. Alisema Serikali itaendelea kuangalia mifuko hiyo na masilahi ya wafanyakazi nchini wanaolitumikia Taifa.
Katika swali la msingi, Ruhoro amehoji Serikali ina mpango gani wa kuirekebisha Kanuni ya kikokotoo ili kuongeza kiwango cha mafao ya mkupuo wa kwanza kwa wastaafu.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema ni muhimu kuzingatia ushauri wa wataalamu kuhusu uendeshaji, usimamizi na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa unazingatia utaalamu wa sayansi ya watakwimu-bima (actuarial science).
“Sheria inaitaka mifuko kufanya tathimini ya kupima uhimilivu kila baada ya miaka mitatu na kutoa ushauri na mapendekezo mbalimbali ikiwemo maboresho ya mafao ya wanachama ambapo kanuni mpya imeanza kutumika Julai 2022,” alisema.
Alisema uamuzi wa kubadilisha kanuni ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu ni lazima utokane na tathimini ya kina ya kisayansi ya watakwimu-bima kama ilivyoelezwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2024.

Wasikie wadau hawa 
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya alisema anakubaliana na Dk Tulia kwa sababu mafao anayoyapata mstaafu ndiyo yanayomwezesha kuanza msingi wa maisha ya kustaafu.
“Na kwa sababu hakuna sheria wala kanuni inayoubana mfuko wa hifadhi ya jamii ndiyo maana kunakuwa na ucheleweshaji. Ukicheleweshewa mafao hakuna chochote utafanya,” alisema.
Alisema kukiwa na sheria ya kuwabana itaongeza ufanisi wa kuwalipa wastaafu mafao na pensheni kwa wakati.
Alisema juzi alipigiwa simu na mmoja wa wastaafu, ambao walikuwa wakilalamikia kupita kwa miezi miwili bila kulipwa pensheni zao za kila mwezi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU), Dk Paul Loisulie alisema ni jambo jema kuongeza kipengele katika sheria kitakachouwajibisha mfuko uliochelewesha mafao, hivyo kuleta uwajibikaji.
“Hii itakuwa nzuri kwa sababu mfuko utashughulika na aliyewachelewesha na mstaafu pia atapata haki yake kutoka kwa mfuko uliochelewesha mafao yake au pensheni, hivyo itawakumbusha kutoa huduma kwa wakati,” alisema.
Mwanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo, alisema ingawa suala hilo limechelewa sana lakini ni jambo zuri likifanywa haraka.
Alisema kutokana na kusemwa na kiongozi wa mhimili wa Bunge, halitachukuliwa kama siasa badala yake litachukuliwa kwa uzito mkubwa.
Mtembo alisema kwa sababu Tanzania inaenda katika uchaguzi mkuu mwakani, suala hilo likizungumzwa na vyama vya wafanyakazi inaonekana kama wanalenga kukichafua chama tawala, lakini kwa sababu limesemwa na kiongozi huyo, Serikali itachukua hatua.
“Waendelee kutupigania, sasa tuna matumaini kuwa wakimaliza hilo wataenda kutafuta na suluhu ya kikokotoo ambacho tunakilalamikia kwa muda mrefu ili hata mstaafu akipata mafao yake kwa wakati basi yawe ya kuridhisha,” alisema.

Related Posts