BEKI anayetajwa kusajiliwa Yanga, Chadrack Boka kutoka FC Lupopo ya DR Congo, inaelezwa anapokuwa uwanjani ni mmyumbulikaji katika kufanya majukumu zaidi ya nafasi yake na pia ana kasi na nguvu.
Shuhuda wa hilo ni beki wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyesema baada ya kukutana naye kwenye mechi ya ligi kuu, aliona uwezo wake wa kupiga klosi, kushambulia na kukaba.
“Jamaa muda wote anapambana, unamuona kwenye maeneo mengi uwanjani, vitu vya kipekee kwake nilivyoviona, ana maamuzi ya haraka, mfano akipandisha kusaidia mashambulizi hajisahau kurudi kwa haraka kukaba,”alisema na kuongeza;
“Endapo kama atafanikiwa kusaini Yanga, itakuwa imepata beki atayewasaidia kuongeza nguvu safu ya mabeki, ukiachana na ubora wake wa kupiga klosi, anajitolea kwa timu yake, maana wakati tumecheza nao, muda wote alikuwa anapambana na ana uwezo wa kuwasababishia wapinzani wafanye makosa ambayo yanawapa faulo.”
Kwa upande wa mshambuliaji wa FC Lupopo, George Mpole anayecheza na Chadrack alisema kitu kikubwa alichokiona kwake ni nidhamu ya kazi, kuanzia kwenye mazoezi hadi wakati wa mechi.
“Nikimzungumzia uwanjani kama kweli Yanga itamsajili itakuwa imepata beki ambaye ana uwezo wa kupiga klosi, kukaba na kushambulia. Jamaa ana nguvu na kasi,” amesema Mpole.
“Nimeona hilo tukiwa tunafanya mazoezi. Binafsi nakuwa napata kipimo halisi kutoka kwake kabla ya kwenda kwenye mechi ya mashindano, kwani haogopi kujaribu kufanya majukumu mbalimbali uwanjani. Aina ya ukabaji wake anakukaba kama vile mnacheza na wapinzani na ndio kitu anachokuwa anakwenda kukifanya wakati wa mechi.
“Kuhusiana na tabia zake za nje, hiyo siwezi kulizungumzia, maana aina ya maisha ya DR Congo kila mchezaji anatoka nyumbani kwake, hivyo muda ambao tunakutana ni ule wa mazoezi na mechi, hivyo huwezi kumjua kwa haraka, halafu Lugha anayozungumza ni Kilingala na Kifaransa na sijamuona akizungumza Kiingereza ambacho huenda tungekuwa tunaelewana kwa uharaka.”
Chadrack anatajwa kuja kuziba pengo la beki wa pembeni, Joyce Lomalisa ambaye inaelezwa hatakuwa sehemu ya Yanga msimu ujao.