SAKATA la kanuni mpya za ukokotoaji mafao ya wastaafu (kikokotoo) kupunja pensheni za watumishi, pamoja na ucheleweshaji wa malipo yake, limeendelea kutikisa Bunge, baada ya wabunge kuhoji hatua zinazochukuliwa na Serikali kuzifanyia marekebisho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Suala hilo limeibuka tena bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 10 Mei 2024, licha ya Serikali kupitia kwa Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi), kuahidi kukifanyia maboresho kwa kuzingatia tathimini itakayotolewa na watalaamu wa watakwimu bima, ili kunusuru uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro, alihoji mpango wa Serikali katika kurekebisha kikokotoo ili kuongeza kiwango cha mafao ya mkupuo wa kwanza. Pia, alihoji Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inalipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuiongezea ukwasi iendelee kunufaisha wanachama wake.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, Patrobas Katambi, amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao ikijumuisha malipo ya mkupuo hivyo itazingatia ushauti wa watalaamu kuhusu uendeshaji, usimamizi na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii katika kubadilisha kanuni hizo.
Kuhusu Serikali kulipa madeni katika mifuko ya hifadhi ya jamii, Katambi amesema Serikali imeanza kufanyia kazi suala hilo ambapo imelipa kiasi cha Sh. 2.1 bilioni kati ya Sh. 4.6 bilioni , ambazo inadaiwa na mfuko wa PSSSF.
Pia, amesema Serikali kupitia Hazina inafanyia kazi malipo ya fedha kiasi cha Sh. 430 bilioni, ambazo inadaiwa na mfuko wa NSSF.
Naye Mbunge Viti Maalum, Sophia Mwakagenda alihoji kwa nini Serikali isifanye marekebisho ya kanuni hizo haraka, ili kuwasaidia watumishi wanaostaafu, ambapo Katambi alimjibu akisema Serikali inafanya taratibu kuangalia namna gani kikokotoo kitawanafuisha wastaafu.
Kwa upande wake Mbunge Viti Maalum (CCM), Husna Sekiboko, alihoji lini Serikali itawalipa wastaafu waliokwama kupata mafao yao kutoka ana sababu mbalimbali, hususan wale ambao walistaafu kabla ya mifuko ya hifadhi ya jamii haijaunganishwa.
Katambi alimjibu akisema “namuomba mbunge aniletee taarifa za wanaolalamika sababu rekodi yetu inaonyesha madeni yaliyorithiwa baada ya mifuko kufanyiwa maunganisho yamelipwa na wengine wanaendelea kufanyiwa uhakiki kwa ajili ya kulipwa.”
Baada ya mjadala huo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliagiza Serikali kurekebisha sheria ya kuadhibu mifuko ya hifadhi ya jamii inayochelewa kulipa mafao ya wastaafu, ikiwemo kwa kuitoza riba kama wanavyotozwa riba waajiri wanaochelewa kuwasilisha michango ya watumishi wao.
“Ushauri wa jumla kama ambavyo waajiri wakichelesha fedha sheria inawataka walipe riba na upande wa mifuko inapochelewesha mafao tuweke riba ili wawe wanawaisha. Tutarajie mabadiliko ya sheria na wao wakibanwa watawaisha,” amesema Spika Tulia.