Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemwagiza Katibu Tawala Mkoa wa huo (RAS), Misaile Musa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, kuwalipa fidia ya Sh1.74 bilioni waliopisha ujenzi wa Barabara ya Mianzini -Timbolo, kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Rufani.
Makonda ametoa maagizo hayo jana katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Arusha, katika baraza la wazi la kusikiliza mashauri ambayo hayajapatiwa ufumbuzi, katika kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Awali, kabla ya uamuzi huo Makonda aliwasikiliza wananchi hao waliowakilishwa na Fanuel Simalai, aliyeeleza licha ya kushinda kesi mahakamani hadi sasa hawajapewa fidia hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kanda ya Arusha, George Njooka, alisoma nakala ya hukumu ambayo halmashauri ilikata rufaa, Mahakama ya Rufani kupinga ushindi walioupata wananchi hao, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama.
Wananchi walishinda kesi Mahakama Kuu lakini halmashauri ikapeleka maombi Mahakama ya Rufaa kukata rufaa nje ya muda ila Mei 25, 2020 Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na halmashauri, hivyo wananchi hao wanaruhusiwa kulipwa fidia hizo.
Alieleza Januari 18, 2023, wananchi hao walienda Mahakama Kuu wakiomba kukazia hukumu, lakini mpaka sasa hawajalipwa.
“Baada ya Hukumu ya Mei 2, 2014 wanasheria wa Serikali walikata rufaa kwa niaba ya halmashauri kutupilia mbali rufaa na Mahakama ya Rufani iliona hoja ni za msingi kwamba halmashauri haikuchukua hatua stahiki katika kufuatilia rufaa yao, waliitelekeza kwa hiyo ikaifuta kwa gharama na hakuna rufaa iliyopo Mahakama ya Rufaa na iliondolewa Agosti 25, 2020,” alisema.
Awali, kabla ya uamuzi wa Makonda, mwanasheria wa halmashauri hiyo, Eliasifiwe Kileo hakutoa ufafanuzi na maelezo kuhusu mwenendo wa suala hilo jambo lililoonyesha kumchukiza Makonda.
“Unaweza ukapata picha kwamba wananchi wanaweza kuzungushwa, kuteseka na kuichukua Mahakama kumbe haina kosa na imeshamaliza kazi yake, ndiyo maana nikasema kikao hiki kama wewe ni mtenda haki na heshima yako kwenye jamii itapanda,” amesema Makonda.
“Kwa mfano mwanasheria wa wilaya kweli hata hii taarifa ulishindwa nini kuisema, wenzako wamekazia hadi hukumu, unataka hii kesi iwe miaka mingapi mnazunguka? RAS nakuagiza watumishi waliokaa muda mrefu kwenye vituo uwahamishe kama huyu mwanasheria mwandikie barua mhamishe, amekaa pale miaka tisa,” amesema.
“Katibu Tawala waandikie halmashauri walipe deni lao, lazima tuheshimu amri za Mahakama. Waandikie halmashauri kwamba maelekezo ya mkuu wa mkoa ni kulipa deni,” amesema.
Kuhusu madalali wa Mahakama, Makonda amemwelekeza Katibu Tawala huyo kuhakikisha taasisi zote za mikopo mkoani humo zinasajiliwa kwa kuwa nyingi hazijasajiliwa zinatoa mikopo bila kufuata taratibu.
“Wako watu walioumizwa na matapeli, wengine wametumia njia ya kudanganya hizo ni hukumu kumbe mahakamani haijawahi kufika, nitumie hadhara hii madalali wa Mahakama wote lazima tuwasajili na kuwatambua, na hakuna kutekeleza amri yoyote ile kwenye eneo bila kumjulisha mkuu wa wilaya kwenye eneo lake ili tubaini matapeli,” amesema Makonda.
Ametoa mfano wa tukio la kampuni ya udalali iliyopiga mnada na kuuza nyumba ya Calist Nassoro, ambaye alikopa Sh3 milioni kwenye Saccoss mwaka 2016, akiagiza nyumba hiyo irejeshwe kwa mmiliki huyo baada ya kubaini kukiukwa kwa taratibu.
“Jana nimekutana na mwenyekiti wa bodi ya ile Saccos na ofisa mikopo na watendaji wake hawajawahi kutoa kibali cha kuuzwa kwa nyumba ile na mwanasheria amejiridhisha pasipo shaka na wao wenyewe wameniambia hawakubaliani na kuuzwa kwa nyumba. Yule muhusika walimpa kibali cha kukusanya madeni si kwenda kuuza nyumba,” amedai.
Amesema, “nimeagiza akamatwe, ashitakiwe na bahati nzuri hadi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilishafanya uchunguzi wa suala hili na kubaini kampuni hiyo haikuwa na mamlaka ya kuuza, ile nyumba inarejeshwa kwa mmiliki,” amesema.
Amesema moja ya kesi zilizofika mbele yake jana ni mtu mmoja kuuza eneo mara mbili kwa watu wawili tofauti, mara ya kwanza aliuza mwaka 2019 kwa Sh26 milioni na alipewa Sh25 milioni na kisha kuuza eneo hilo kwa mtu mwingine.
“Alivyohojiwa alikiri amepokea Sh25 milioni biashara na mkataba hausemi milioni moja iliyobaki italipwa lini, na hata alipolipwa kiasi kilichobaki aliuza upande wa pili,” amesema.
Amesema ikiwezekana wataweka kila wilaya wanasheria wa kujitolea ili kusaidia wananchi wasio na uwezo, ambao wengi wanashindwa kesi kutokana na kushindwa kufuata taratibu za kisheria.