Pamba yavunja kambi, bodi yaachiwa msala

KIKOSI cha Pamba Jiji kilivunja kambi yake juzi (jumatano) wachezaji na benchi la ufundi wakipewa mapumziko na kuruhusiwa kuondoka, huku hatima ya kinachofuata ikiachiwa bodi ya klabu hiyo.

Pamba uilivunja kambi yao baada ya mchezo maalum wa kukabidhi ubingwa wa Championship, kati ya timu hiyo dhidi ya Ken Gold (bingwa) kwenye Uwanja wa Azam, jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezo huo ulikuwa wa mwisho kwa kikosi cha Pamba Jiji msimu huu baada ya kufanikiwa kupanda kwenda Ligi Kuu baada ya miaka 24 ikimaliza nafasi ya pili na alama 67 nyuma ya vinara Ken Gold waliovuna pointi 70.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Moses William aliliambia Mwanaspoti kwamba wachezaji na makocha wameruhusiwa kutawanyika huku akiwataka mashabiki na wadau kuwa wavumilivu wakati bodi ya klabu ikipitia ripoti ya timu.

“Tumevunja kambi jana (Jumatano) baada ya mechi na Ken Gold wachezaji na makocha wameruhusiwa kutawanyika, tunawashukuru watu wote waliotusaidia tangu tumeanza mpaka hapa tulipofikia,” alisema William na kuongeza;

“Makocha wameshawasilisha ripoti yao ya ufundi kwa viongozi na bodi ya klabu baada ya hapo kitakachofuata wataambiwa na kupewa mrejesho wa nini kinatakiwa kufanyika,” alisema

Hata hivyo, Mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Evarist Hagila, alinukuliwa na Mwanaspoti, akisema baada ya furaha na sherehe za kuipongeza timu bodi itakutana kupitia na kujadili ripoti ya benchi la ufundi, kuanza mikakati ya msimu mpya na kufanya uamuzi sahihi..

Nini ushauri wako, tuandikie: 0658-376417

Related Posts