FURAHA imerejea Simba. Mabadiliko yaliyofanywa kwenye benchi la ufundi na kumrejesha Juma Mgunda yameanza kulipa. Ametumia mechi nne tu kubadilisha mambo ndani ya klabu na sasa imefikia hatua wakongwe wamesema apewe timu.
Si hao tu, hata mashabiki baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam juzi na kufufua matumaini ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao, walisikika Uwanja wa Mkapa wakipiga kelele kushinikiza Mgunda aaminiwe apewe timu ingawa mwenyewe amesisitiza anatekeleza kwanza kazi aliyopewa ya kumaliza msimu.
Nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel amesema viongozi wa timu hiyo wanatakiwa kubadili mitazamo yao kwa sababu hapakuwa na sababu ya kumwondoa Juma Mgunda tangu mwanzo kutokana na mwenendo wake.
Gabriel ambaye alikuwa mshambuliaji tishio Msimbazi alisema;
“Hata kipindi kile alichopewa timu kwa mara ya kwanza, Simba ilikuwa na mwenendo mzuri na hiki anachofanya sasa inaonyesha ni kocha mwenye uwezo mkubwa ambaye kama angeendelea wakati ule hadi leo pengine timu ingekuwa na hatua kubwa.”
Aliongeza; “Simba ina wachezaji wengi wazuri, kinachotakiwa ni kuaminiwa tu kitu ambacho anaonekana kufanya Mgunda, amekuwa akiwajenga wachezaji wake na ndio maana tumeona timu ikibadilika kwa haraka, kama tumepoteza miwili hadi mitatu kwa makocha wazawa bila matunda tugeukie na wazawa ambao tayari wanaonyesha viashiria vya kufanya vizuri.”
Beki wa zamani wa Simba, George Masatu alisema, “Ninashauri aaminiwe tu kama ambavyo imekuwa kwa makocha wa kigeni ambao wamepita, basi iwe hivyo kwa Mgunda, pia tusimchukulie poa kwa sababu ni Mtanzania mwenzetu, ameonyesha kuwa na kitu basi aachiwe timu moja kwa moja.”
Mgunda mwenyewe akizungumzia endapo anaweza kusalia kwenye kikosi hicho alisema: “Hayo maoni ya mashabiki nayasikia, wakiona nafanya kazi nzuri ni jambo linalotia faraja lakini kwa sasa nimepewa jukumu la kumalizia mechi zilizosalia za ligi baada ya hapo tutakuwa na maamuzi.”
Tathmini ya jumla inaonyesha kuna sababu tano zimerejesha thamani ya Mgunda Simba;
MABADILIKO YA KIKOSI
Kwenye mechi hizo nne amefanya mabadiliko makubwa ya kikosi akiibua mseto mpya wa kuwarudisha mchezoni kundi ambalo lilikuwa linasotea benchi kwenye utawala wa Kocha Abdelhak Benchikha.
Mgunda amewatumia Edwin Balua, Ladack Chasambi, Mzamiru Yassin na Kennedy Juma aliyemweka benchi Henock Inonga na Simba kuonyesha kutulia na katika mechi hizo nne ni mechi moja tu wekundu hao waliruhusu mabao mawili kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo kwenye mchezo wa kwanza wa kocha huyo na baada ya hapo ikacheza mechi tatu ikishinda zote na kufunga mabao tisa na kusomba pointi 10.
Simba imeshinda mechi kubwa dhidi ya Azam, Mgunda akiwakosa wachezaji wake wenye majina makubwa Clatous Chama,Said Ntibazonkiza, Shomari Kapombe na Inonga ambaye alikuwa benchi kocha huyo akilipa kisasi cha kupoteza dhidi ya matajiri hao kwa bao 1-0, wakati akiwa kocha wa muda hapo nyuma.
SAIKOLOJIA KASHINDA
Thamani kubwa ya Mgunda ni kujua namna ya kuwatengeneza wachezaji wake kisaikolojia silaha ambayo ilikuwa inambeba hata wakati akiwa Coastal Union, akaifanya pia sasa aliporejea Simba.
Mgunda amewajaza wachezaji wake ujasiri upya na kuanza kurudisha ushindani baada ya kushtuka wakati akirejea kwenye timu hiyo kwa kipindi hiki hatua ambayo imeirudishia nguvu timu hiyo.
Staa mmoja wa Simba anayecheza nafasi ya kiungo ameliambia Mwanaspoti: ”Siyo kwamba tulikuwa na timu mbovu lakini kundi kubwa la wenzetu ni kama lilikata tamaa, timu ilikuwa haipati matokeo lakini wengine walikuwa wanaona kama hawathaminiki tena kocha aliyetoka alikuwa mkali sana hili lilipoteza nafasi ya wachezaji kujiamini na kuonyesha makali yao lakini huyu kocha aliyekuja anataka kila mchezaji ajiamini na ajione ana thamani ya kuitumikia Simba,” alisema kiungo huyo raia wa kigeni.
MATOKEO SAHIHI
Mgunda ukiacha kipindi cha nyuma ambacho hata Yanga ililazimika kugawana nayo pointi ikisawazisha baada ya wekundu hao kutangulia kupata bao, safari hii amerudi kwa kishindo akiwa na ushindi wa mechi tatu na akipata sare moja matokeo ambayo yameirudisha Simba nafasi kubwa ya kushika nafasi ya pili ikipeleka presha kwa Yanga kama inautaka ubingwa inatakiwa kushinda mechi zao mbili zijazo.
Matokeo hayo ya mechi nne tu hasa mechi dhidi ya Azam yamewashushia presha hata mabosi wa Simba ambao ilikuwa ngumu kwao kupita hata mbele ya mashabiki wao baada ya timu hiyo kukosa matokeo mazuri kabla ya ujio wa Mgunda.
GHARAMA ZIMEPUNGUA
Simba inapambana kupunguza gharama za uendeshaji hususan bajeti ya mishahara ikikumbuka Benchikha alikuwa akichukua zaidi ya Sh100 milioni kwa mwezi kama mshahara wake pamoja na benchi lake. Endapo wekundu hao watafanya maamuzi ya kwenda na Mgunda itapunguza kiasi gharama hizo na malipo mengine ya vibali kutoka kwa makocha wa kigeni.
MTIHANI KWA MGUNDA
Ni mechi mbili tu. Tena ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Dodoma Jiji. Simba inaona ushindi wa mechi hizo mbili zinatosha kuwahakikishia nafasi ya pili katika mbio za kuiwania wanapoendelea kukimbizana na Azam FC.
ISHU YA CHAMA, INONGA, LUIS
Simba imempa ofa ngumu kiungo wake Clatous Chama, pia ikamuweka njiapanda beki wake Henock Inonga huku ikijipanga kuachana na winga Luis Miquissone.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema Chama ameshapewa ofa mpya ambayo inaweza kumbakisha kiungo huyo lakini haitakuwa na presha yoyote ya kubadilika endapo Mzambia huyo atakuwa na ofa zingine kuishinda hiyo ya wekundu hao.
Chama ambaye mkataba wake unafikia tamati mwisho wa msimu huu, mezani ana ofa kubwa mbili kutoka Yanga na Azam lakini mabosi wa klabu yake hawataki kuingia mtego wa kushindana na ofa hizo ikitaka kiungo huyo kufanya maamuzi ya mwisho.
“Sioni kama tutampa ofa kubwa zaidi ya hiyo ni uamuzi wake kuamua kama atakubaliana na hilo au vinginevyo kuna mambo mengi tunayapima kwenye hizi ofa ambazo tunawapa wachezaji wetu, kama ataona kuna ofa kubwa zaidi huko nje Simba haitashindana nazo,” alisema bosi huyo ambaye yumo kwenye bodi ya wakurugenzi wa Simba.
Mbali na ishu ya Chama kwa upande wa Inonga Simba itampa nafasi beki huyo kuleta ofa ambayo atataka kwenda baada ya beki huyo kubakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
“Inonga ishu yake iko tofauti kuna mambo ambayo hatuyafurahii, ni beki mzuri ila tunataka kufanya maamuzi magumu kwa kuwa amebakiza mwaka mmoja wa mkataba wake kama atakuwa na ofa ya kutakiwa na klabu yoyote tutaikaribisha mezani na tutafanya maamuzi ya kumuachia.
“Kuna Luis Miquissone naye matarajio yetu ya kumrudisha yamekuwa tofauti kwa hiyo naye tunaweza kuachana naye na kutafuta mchezaji mwingine huyu ni mchezaji ambaye analipwa fedha nyingi na tunataka kupunguza bajeti yetu ya mishahara ambayo sasa imefikia Sh600 milioni kwa mwezi,” alidokeza kiongozi mzito ndani ya Simba.