Miongoni mwa tabia hatarishi kwa wanaume ni kutokuwa na mwamko wa kusaka matibabu, ikilinganishwa na wanawake.
Tabia hii imeelezwa kuwa kisababishi cha vifo vya mapema, kwani wengi hushindwa kujua hali zao za kiafya, ikiwemo magonjwa mbalimbali, hasa yasiyoambukiza na hivyo kukosa tiba za mapema.
Kiharusi ni miongoni mwa magonjwa yanayoongezeka kwa sasa, kikiathiri zaidi watu walio na shinikizo la juu la damu lisilodhibitiwa au kisukari, hasa kisichotibiwa.
Kiharusi, maarufu kama ‘stroke’ hutokea pindi damu imevuja juu ya ubongo baada ya mshipa wa damu kupasuka au imeshindwa kupita sehemu za ubongo zinazohitaji chakula na oksijeni ya kutosha.
Ongezeko la wagonjwa wanaopata kiharusi limeanza kuonekana nchini ambapo tangu Juni mwaka 2023, Taasisi ya Mifupa na mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) imekuwa ikipokea wagonjwa watatu mpaka sita kwa wiki waliopata kiharusi cha kupasuka mshipa wa damu.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa na MOI katika Wilaya ya Kinondoni unaonyesha kati ya waliopata kiharusi, asilimia 63 ilisababishwa na shinikizo la juu la damu ‘presha’, huku asilimia 49 kati yao hawakuwa wakijua hali zao za presha.
Kwa mujibu wa Daktari bingwa na mbobezi wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Alpha Kinghomella, umri pia umeshuka, kwani wagonjwa wanaopata kiharusi ni kati ya miaka 20 hadi 50 zaidi ikilinganishwa na miaka ya zamani.
Baadhi ya wanaume waliozungumza na Mwananchi wamesema, hufikia hatua ya kwenda hospitalini pale tu wanapoumwa na kutojiweza kabisa.
“Mimi sijawahi kwenda hospitalini, nikijisikia vibaya ninakunywa maji mengi au naenda kupumzika ingawa naogopa sana kunywa dawa mara kwa mara,” anasema Msafiri Ibrahim.
Kama ilivyo kwa Msafiri, ndivyo yalivyo maisha ya Omary Iddi, anayesema humeza dawa za kutuliza maumivu pekee anapohisi hayuko sawa kiafya.
“Naingia duka la dawa naomba zile za kutuliza maumivu nakunywa nimemaliza. Mara ya mwisho kwenda hospitalini mama yangu alitutembelea nikaumwa akanisisitiza sana twende kituo cha afya, miaka 12 sasa imepita sijaenda hospitali,” anasema Omary.
Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige anasema wanaume ni wazito kupima afya na wengi akijisikia vibaya anatafuta duka la dawa anameza dawa za kutuliza maumivu au anakunywa energy drink.
“Mwanamume ni mzito kwenda hospitalini, huko kwa sasa miongoni mwa vipimo vya lazima ni kuangalia shinikizo la damu. Wao wanahisi uchovu anakunywa energy au dawa kutuliza maumivu anaendelea na maisha.
“Mwanamke akipima mapema anagundulika na shinikizo la damu anaanza matibabu mapema na kama mjamzito kule kupima mara kwa mara, kunasaidia na kuna dawa maalumu anapewa na akijifungua inapungua. Wanaume ni wabishi na hawataki kukubali, wengi hawalali vizuri na lishe pia tatizo,” anasema.
Dk Mzige anasema maumbile ya mwanamke na mwanamume ni tofauti katika homoni zao na mwanamke huwa salama zaidi anapokuwa katika kipindi cha hedhi, lakini anapokoma changamoto huanza kutokea na ndiyo sababu huanza kupata magonjwa baada ya kukoma hedhi.
“Akiwa mtu mzima hapati damu ya mwezi, zile homoni alizokuwa nazo hazipo, zina athari nyingine katika maumbile yake kutokuwa na calcium ya kutosha kwenye damu yake na mengine na ndiyo maana shinikizo la damu linajitokeza kwa wazee zaidi.
“Vijana inaongezeka sababu ya lishe na mtindo wa maisha, unywaji wa pombe kali, bia, vinywaji vya kuongeza nguvu, vyakula vingine vina kemikali na wengi hawali mboga za majani na matunda zinazoondoa hizo kemikali,” anasema.
Dk Mzige, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya kabla ya kustaafu mwaka 2005, anasema: “Nina shinikizo la juu la damu huu ni mwaka wa 42 natumia kidonge kimoja kila siku na ninaishi. Tatizo hili ni kubwa, kati ya Watanzania watatu wenye umri wa miaka 24 mpaka 50, mmoja atakuwa na shinikizo la damu.”
Akizungumzia ukubwa wa tatizo, Dk Kinghomella anasema kiharusi hutokea damu inapovuja juu ya ubongo, mishipa kupasuka au kuna ugonjwa ulikuwepo hapo kabla ambao mara nyingi ni vivimbe vidogo vidogo vinavyoota juu ya mshipa wa damu unaoenda kwenye ubongo.
Anasema panapokuwa na mabadiliko ya presha au msukumo wa damu ndani ya mishapa ya damu, vivimbe hivyo huwa vinapasuka vyenyewe na kusababisha kiharusi.
“Sisi tunaona asilimia 40 ya wagonjwa wote wa kiharusi, maana zipo za aina mbili, ipo hii inayotokana na kuvuja kwa damu kichwani, na ile ambayo damu hushindwa kupita kufika sehemu mbalimbali za ubongo kwa sababu mishipa ya damu inakuwa imeziba.”
Anasema tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu ni kubwa zaidi na machapisho mbalimbali yanaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa hupata kiharusi cha aina hiyo.
“Hii asilimia 60 wanatibiwa Mloganzila, sisi tunatibu asilimia 40 kwa sasa, kwa wiki moja tunaweza tukapata wagonjwa wa kiharusi wanaofikia watatu mpaka sita, hii inaonyesha tatizo ni kubwa. Inawezekana jamii haielewi au haina ufahamu wa kutosha kuhusu magonjwa haya na visababishi vyake,” anasema.
Dk Kinghomella anataja visababishi mbalimbali, ikiwemo shinikizo la juu la damu na wale wenye kisukari cha muda mrefu ambao hawajatibiwa au kinatibiwa lakini ile sukari haikai kwenye ule usawa unaohitajika.
Anataja sababu nyingine ni matumizi ya dawa za kulevya au unywaji dawa bila ushauri wa daktari, unywaji vinywaji vikali, pombe kali au kunywa kupita kiasi.
“Kuna sababu nyingine za magonjwa ya kurithi au kitaalamu vivimbe vidogo vidogo kama shinikizo la damu siyo kubwa sana hivi vivimbe haviwezi kupasuka, kwani hatari inakuwa ni ndogo sana chini ya asilimia 1, lakini kama kutakuwa na mabadiliko ya presha au msukumo wa damu kuna uwezekano vivimbe hivi kupasuka,” anasema.
Dk Kinghomella anasema kutokana na mtindo wa maisha vivimbe vya kurithi vinakuwa hatarini kutokana na mtindo wa maisha.
“Zamani tulitibu wenye shinikizo wakiwa na miaka 50 mpaka 60, lakini siku hizi tunaona chini ya miaka 50 mpaka 20 ambao ni nguvu kazi ya taifa, wana harakati nyingi katika kumudu maisha na wanakuwa bize na hawa ndio wanaokuja wamepata kiharusi na hawakujua wana shinikizo la damu au kisukari,” anasema.
Anaongeza kuwa wengi hawafanyi uchunguzi wa afya zao: “Tukitibu kiharusi tunaanza kutibu magonjwa mengine yanayoibuka na kugundulika, lakini yalikuwa ya muda mrefu na ndiyo yamesababisha kiharusi.”
Kwa mujibu wa Dk Kinghomella, kwa sasa wapo kwenye hatua za awali za kukusanya takwimu za wagonjwa na kwamba kuna andiko linalotarajiwa kuchapishwa miezi tisa baadaye.
“Tunakusanya hizi takwimu na kuzichakata kitaalamu, ili umma wa Watanzania wajue aina ya kiharusi na watu tunaowapata na kiharusi cha aina gani, ili tuweze kuwalewesha wananchi na matibabu yake yakoje,” anasema.
Anafafanua kuwa utafiti huo ambao MOI wameanza kuufanya utasaidia kutoa picha kamili ya hali halisi nchini, ili wale walio katika hatari watenge muda wa kufanya vipimo.
“Serikali sasa imeweka mifumo ya CT Scan kila mkoa na ni kifaa kimojawapo cha kugundua kama mtu amepata kiharusi ama la, tutumie vifaa hivi kubaini mapema magonjwa haya,” anasema.
Dk Kinghomella anatoa rai kwa wagonjwa waliowahi na wanaopata maumivu ya kichwa ambayo hayajawahi kutokea.
“Kama unaumwa kichwa muda wote na unakunywa dawa tu, kama una presha inazidi kuwa juu na unakunywa dawa bado haisaidii au una matatizo ya sukari imekaa muda mrefu kila ukicheki ipo juu unabadilishiwa dawa ipo juu, fika tukufanyie uchunguzi kama kuna tatizo ambalo linaweza kuambatana na kiharusi huko mbeleni,” anasema Dk Kinghomella.