Serikali yatoa kauli changamoto za kikodi katika sekta ya madini

Dar es Salaam. Serikali imewataka wadau wa madini kuendelea kushikamana wakati huu ikiendelea kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo  za kikodi .

Imesema kuwa inafahamu changamoto ya kodi hususani kifungu cha 56 ya sheria ya fedha na urejeshwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT Refund).

Marekebisho yanayohitajika na wadau kwenye sheria ya fedha kutokatwa kwa kodi kwenye faida ya mtaji kwa mtu aliyepunguza hisa zake kwa kampuni nyingine, badala yake kifungu hicho kijikite kukata kodi kwa kampuni inayonunua kampuni nyingine.

Kwa mujibu wa sheria hiyo iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2023, inatambua kuwa kampuni moja inapotoa zaidi ya nusu ya hisa zake kwa kampuni nyingine itatambulika umiliki wake umebadilishwa hivyo, italazimika kulipa kodi ya mtaji wa faida jambo ambalo wadau wa madini walisema inawafukuza wawekezaji.

Hayo yameelezwa Mei 9, 2024 na Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa kwenye mkutano wa baina ya wizara yake na wanachama wa Chemba ya Migodi Tanzania, ambapo amesema suala la kubadilisha sheria linahitaji kuhusishwa na taasisi na wadau.

“Nitoe rai kwamba kwenye sekta ya madini tuendelee kushirikiana wakati Serikali ikishughulika na kutatua changamoto hizo,” amesema.

Dk Kisurwa amesema ili sekta ya madini ilete manufaa chanya Serikali na makampuni ya uchimbaji ni vyema kukawa na ushirikiano wa karibu unaolenga kuongeza tija na ufanisi.

Kuhusu ukuaji wa sekta ya madini, Dk Kiruswa amesema inachangia asilimia 9.1 kwenye pato la Taifa akitaja sababu zilizochangia ni uendelezaji wa miradi ya utafiti na uchimbaji.

Kufikia 2025, Dk Kiruswa amesema kama miradi iliyopangwa itatekelezwa kwa uhakika basi, sekta ya madini itachangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa kama ilivyopangwa.

Naye Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Benjamini Mchwampaka amesema Tanzania ina madini mengi lakini ni lazima kuwepo na sera zinazovutia uwekezaji, akisisitiza kinachohitajika ni mitaji kutoka nje ya nchi.

“Hiyo ndio inatusaidia kuendeleza migodi na hapo tunapata kodi ya Serikali, ajira na miundombinu hivyo ni muhimu kuwa na sera na sheria zinazovutia uwekezaji,” amesema.

Mjumbe wa Chemba ya Migodi Tanzania, Simon Shayo amesema baadhi ya masuala kikodi utaratibu wa utoaji wa leseni ni miongoni mwa mambo wanayotaka Serikali iangalie upya kero zilizopo na kuzifanyia kazi.

Related Posts