Iringa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka wakuu wa taasisi zote za umma kutumia Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-office) katika utendaji kazi na kuachana na matumizi makubwa ya karatasi katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.
Wito huo umetolewa jana Alhamisi Mei 9, 2024 wakati akifunga kikao kazi na mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji wanataaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania yaliyoanza Mei 6 hadi 9 Mei, 2024 Mjini Iringa.
Simbachawene amesisitiza kuwa matumizi ya mfumo wa ofisi mtandao katika utendaji kazi sio hiari wala ombi tena bali ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona tija zaidi katika utendaji kazi wa Serikali.
“Waajiri walio wengi serikalini hawachangamkii matumizi ya mfumo wa e-office, badala yake wamekuwa wakiendelea kutumia karatasi zaidi na makabati ambayo hata hivyo, hayazingatii utaratibu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali,” amesema.
Simbachawene amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wataalamu wa menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka kwa usalama na ustawi wa Taifa.
Pia, amewafahamisha washiriki hao kutambua kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana kubwa ya kutunza kumbukumbu na nyaraka zake muhimu, kwa hiyo hawana budi kulinda dhamana hiyo na kuitendea haki kwa ustawi na maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa kwa yeyote atayebainika kutoa au kuvujisha siri za Serikali atachukuliwa hatua za kinidhamu na kuwajibishwa kwa mujibu wa Taratibu, Kanuni na miongozo ya kiutumishi.
Amewapongeza waajiri waliowaruhusu maofisa kushiriki kikao kazi na mafunzo hayo maalumu na kuwalipa posho ya kujikimu na nauli.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwalaumu waajiri waliowazuia watumishi wa kada hiyo kushiriki kikao kazi hicho ambacho ni utekelezaji wa sehemu ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati wa kikao kilichofanyika Zanzibar.
Kikao kazi hicho na mafunzo maalumu, yamewakutanisha wanataaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania takribani 1,500 kutoka taasisi mbalimbali za umma Tanzania Bara na visiwani chini ya kaulimbiu isemayo,
“Misingi bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, uadilifu na utunzaji siri ni nguzo ya kitaaluma.”