Sitta ang’ang’ana wanafunzi watibiwe bure, Serikali yagoma

MBUNGE wa Urambo, Margaret Sitta, ameishauri Serikali iweke utaratibu wanafunzi wapatiwe huduma za afya bure kama inavyotoa huduma za elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Sitta ametoa ushauri huo leo Ijumaa, bungeni jijini Dodoma, akiuliza swali la Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda, aliyehoji Serikali haioni haja ya kuwalipia wanafunzi gharama za matibabu wanapougua shuleni.

Margaret Sitta

Ni baada ya Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, kusema Serikali imeweka utaratibu maalum kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ambapo wanafunzi wanajiunga kwa makundi kupitia shule wanazosoma kwa kuchangia Sh. 50,400 kwa mwaka, ambapo unawasaidia kupata matibabu wakiwa masomoni na wakati wa likizo.

“Baadhi ya wazazi watashindwa kulipa hiyo bima, kama ilivyo elimu bure na afya iwe bure, amesema Sitta.

Dk. Mollel amesema ushauri huo utekelezwaji wake ni mgumu kwa kuwa huduma za afya ni ghali hivyo Serikali ikifanya hivyo itashindwa kufanyia kazi vipaumbele vingine katika sekta hiyo.

“Ni kweli kuna wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia hii 50,400 lakini kuna utaratibu wa kiserikali kuwasaidia wasiojiweza na wamekuwa wakitibiwa bure. Hili la kusema kwamba afya iwe bure kama ilivyo elimu ni ngumu sababu kutibu peke yake kisukari inahitaji Sh. 321 bilioni. Huo ni ugonjwa mmoja na hapa bungeni tunapitisha bilioni 200 kwa ajili ya dawa kwa hiyo utaona ugumu wake,” amesema Dk. Mollel.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliishauri Serikali kuandaa utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia duni kunufaika na bima hiyo ili waweze kupata huduma za afya.

Related Posts