Stand United, Copco tiketi iko Kambarage

 Mwanza. BAADA ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United, Copco imesema inaenda kumaliza dakika 90 za marudiano ikihitaji sare au ushindi ili kujihakikishia kubaki salama kwenye Championship msimu ujao.

Timu hiyo ikicheza nyumbani kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza iliishindilia Stand United mabao 2-0 katika mchezo wa mchujo (play off) hatua ya kwanza na keshokutwa Jumapili itakuwa Kambarage mjini Shinyanga kukamilisha dakika 180.

Copco inashuka uwanjani kuwakabili chama hilo la Wana la mjini Shinyanga ikihitaji ama sare au ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kubaki championship msimu ujao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Faisali Hau amesema ushindi huo ni mtaji mzuri na hatua ya kutoruhusu bao nyumbani ni ishara njema kwao kwani itawasaidia katika mechi ya marudio.

Amesema wanawafuata wapinzani kwa umakini kuhakikisha hawaruhusu bao ili kuweza kufikia malengo yao, akieleza kuwa vijana wako fiti kiakili, kiushindani na kisaikolojia.

“Tunaeda kupambana kumaliza salama sakika 180 kuibakiza timu salama championship, tunajua ugumu wa mechi hiyo ila tutawaandaa vyema vijana kutofanya makosa” alisema Hau.

Kwa upande wake, Kocha wa Stand United, Seleman Kitunda amesema makosa yaliyofanywa na mabeki wake hatarajii kujirudia na sasa wanarejea Kambarage kufa na kupona kumaliza kazi.

“Vijana walikosa umakini haswa eneo la beki na kuruhusu mabao mepesi, lakini mechi haijaisha tunakwenda kusawazisha matokeo na kupata ushindi ili tubaki kwenye ligi,” amesema kocha huyo.

Related Posts