Thiago Silva kama kawa amemalizia hisani nyumbani

YUKO wapi yule aliyesema hisani inaanzia nyumbani? Wazungu huwa wanaandika kwa Kiingereza chao kizuri ‘charity begins at home’. Ni kweli. Lakini Wabrazil nao wangeweza kuendeleza sentensi hiyo na kuandika ‘hisani pia inaishia nyumbani’.

Wiki ile nyingine nilimuona Mbrazili Thiago akilia katika viunga vya uwanja wa mazoezi wa Chelsea, Cobham. Labda ana hisia kali na Chelsea baada ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya miaka ya karibuni iliyopita. Thiago alikuwa akiaga hatakuwepo tena Chelsea.

Anastahili. Miaka 39 ni migumu kucheza katika kiwango cha juu Ulaya. Septemba mwaka huu anatimiza miaka 40. Lakini wapi kwingine angeweza kwenda? Saudi Arabia kuungana na Cristiano Ronaldo au Marekani kuungana na Lionel Messi?

Kama ulikuwa unawaza hivyo ulikuwa unapotea. Wabrazili bwana huwa wananiacha hoi. Pesa ina maana kubwa kwao, lakini  kuna maana kubwa zaidi. Ghafla nikamuona Thiago akiwa na tabasamu na familia yake wakiwa wamevaa jezi za Fluminense. Klabu ya Ligi Kuu Brazil.

Sikushangaa. Kwa Wabrazili hisani inaanzia nyumbani na inaishia nyumbani. Wanaanza kwa kuonyesha vipaji nyumbani. Ghafla rafiki zetu wenye pesa nyingi Ulaya wanakwenda kuwachukua na kuzipa timu zao uhai wa kipesa.

Wanakwenda Ulaya wanavuna pesa. Wanaiteka dunia. Mwisho wa siku hawana tamaa zaidi ya kwenda kuchota pesa Marekani au Uarabuni. Wanarudi zao nyumbani katika klabu zilezile walizoanzia maisha. Kama sio klabu zilezile, basi wanaamua tu kurudi nyumbani. Na nyumbani kwao ni kuzuri hasa. Nimekwenda mara mbili.

Angalia wachezaji wengi mahiri wa Brazil waliotamba Ulaya. Walikipiga Ulaya wakatamba. Klabu zao za mwisho kustaafu zilikuwa Brazil. Ronaldo de Lima alianzia Cruzeiro. Alitamba Ulaya. Aliamua kustaafia wapi? Corinthians. Hakwenda Marekani wala Uarabuni.

Ronaldinho Gaucho. Alianzia soka lake Gremio. Alizurura alikoweza lakini hakwenda Marekani wala Uarabuni. Alistaafu akiwa amevaa jezi ya Fluminense. Labda angefurahi zaidi kupata nafasi ya kustaafia na jezi ya Gremio, lakini hakupata nafasi hiyo. Hata hivyo alilazimisha kustaafia Fluminense.

Kwa Rivaldo nayo ilikuwa vivyo hivyo. Alitoka zake kwake akiwa ameanzia katika klabu ya Mogi Mirim na baada ya kutamba Ulaya alihakikisha kwamba anarudi Brazil kustaafia katika jezi za timu hiyo. Wabrazili ndivyo walivyo.

Mwaka 2007 nilikwenda Brazil na timu ya taifa ya Tanzania. Tukafikia katika kambi ya vijana ya Fluminense. Miongoni mwa picha maarufu zilizobandikwa katika ukuta wao ni picha ya Marcelo. Mmoja kati ya walinzi bora wa pembeni kuwahi kutokea Brazil.

Tulikuwa tumepishana naye. Ndio kwanza alikuwa amekwenda kujiunga na Real Madrid. Baada ya kucheza Real Madrid kwa muda mrefu kisha akaibukia Olympiacos, Marcelo aliamua kutafuta sehemu ya kustaafu. Wapi kwingine zaidi ya nyumbani? Alirudi zake Fluminense na mpaka leo anacheza hapo. Hakwenda Qatar wala Marekani.

Mifano kama hii ni mingi. Na sasa ameongezeka Thiago. Hajanishangaza sana. Kwa pesa ambazo zipo Saudi Arabia kwa sasa sijashangaa kwanini amezitupia kisogo na kuamua kurudi katika klabu ambayo alianzia maisha kama Marcelo, Fluminense.

Mchezaji pekee mwenye jina kubwa wa Brazil aliyeamua kwenda Marekani ni Ricardo Kaka. Labda kwa sababu hana utamu wa nyumbani kwa sababu ya ulokole wake. Ukweli ni kwamba Wabrazili halisi hauwaambii kitu kuhusu nyumbani.

Hata klabu mpira haujaisha vyema akili yao inakuwa nyumbani. Rafiki yangu Adriano aliamua kurudi nyumbani huku Ulaya ikiwa haijamalizana naye. Alirudi mapema tu akiwa na miaka 28. Kama umewahi kufika Brazil kuna kitu utakielewa.

Maisha yao ya kijamii ni mazuri. Wana vyakula vizuri na ni moja kati ya nchi zinazozalisha chakula kwa wingi duniani. Wana utamaduni wao wa kufurahia maisha kwa kutabasamu kila wakati. Kucheza ngoma. Kunywa bia pamoja lakini huku nchi yao ikiwa na hali ya hewa nzuri. Kuna joto zuri ambalo linawafanya washinde katika fukwe zao.

Wanafunga barabara na kuamua kunywa zao bia. Hawana hofu sana na maisha. Brazil ni miongoni mwa nchi ambazo zina idadi kubwa ya watu kama ilivyo kwa China, India, Nigeria na wengineo. Lakini umewahi kukutana na idadi kubwa ya Wabrazili nje ya nchi yao? Hapana. Wanafurahia maisha yao nyumbani.

Ndio maana wachezaji wa Brazil akili inakuwa nyumbani kwa sababu kadhaa. Kwanza wanapenda kurudi katika tamasha lao kubwa la ngoma maarufu kama Carnival. Lakini pia pindi wanapopata majeraha barani Ulaya na kwingineko huwa wanaomba wakatibiwe nyumbani ili wawe karibu na ndugu zao.

Lakini katika kustaafu ndio huwaambii kitu. Neymar ni miongoni mwa wachezaji walioamua kwenda kuchukua pesa za Waarabu. Amekwenda mapema kuliko ilivyodhaniwa, lakini muda si mrefu utasikia anarudi kwao kukipiga katika klabu yake ya zamani Santos.

Kinachotokea ni kwamba wanaanza na hisani ya kwanza kwa kuuzwa kwenda nje. Timu zao za Brazil zinapata pesa. Lakini wanaporudi Brazil baada ya kuvuna umaarufu mkubwa Ulaya huwa wanasaidia timu zao kupata mapato kwa sababu mashabiki wanavutika kwenda viwanjani kwa sababu yao. Nani hataki kwenda kutazama mechi ya Fluminense kumcheki Marcelo? Na sasa hivi ataungana na Thiago.

Lakini pia kwa hizi timu kubwa za Brazil ambazo wanarudi huwa wanazipa uzoefu mkubwa katika michuano mikubwa ya Amerika Kusini kama ile ya Copa Libertadores. Dani Alves alirudi zake nyumbani na akajiongezea taji hili katika orodha ya mataji mengi ambayo tayari alishakusanya Ulaya.

Related Posts