MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umefanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana, kuhusu masuala matano yenye lengo la kuimarisha haki hizo nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mkutano huo ulifanyika tarehe 7 Mei 2024, jijini Dodoma, baina ya ujumbe wa THRDC ulioongozwa na Mratibu wake, Onesmo Olengurumwa na Balozi Chana pamoja na watendaji wa wizara hiyo iliyopewa mamlaka ya kuratibu na kusimamia masuala ya haki za binadamu.
Olengurumwa ametaja masuala hayo yaliyojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni, namna ya kumalizia uandaaji wa mpango wa haki za binadamu awamu ya pili, uandaaji wa mpango wa haki za binadamu katika maeneo ya biashara, uandaaji wa sera ya kuwalinda watetezi wa haki za binadamu pamoja na uboreshaji masuala ya elimu ya haki za binadamu shuleni.
Masuala mengine ni uboreshaji juu ya namna Serikali ya Tanzania inavyowasilisha taarifa zake za masuala ya haki za binadamu katika jumuiya za kimataifa, ikiwemo vyombo vya usimamizi wa haki hizo katika Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU).
“Tumekuja kuonana na wizara yetu kama kawaida na utaratibu wetu wa kuwa na mikutano ya mara kwa mara na wizara hii sababu ndio wizara mama inayolinda na kuratibu haki za binadamu nchini. Tumekutana na waziri na watendaji wa wizara kujaidliana masuala yenye lengo la kuimarisha haki za binadamu ikiwemo katika maeneo ya biashara,” alisema Olengurumwa.
Kwa upande wake Afisa Uchechemuzi wa THRDC, Wakili Nuru Maro, amesema ziara hiyo ina tija na kuwa wataendelea kushirikiana na serikali katika masuala yote ya utetezi wa Haki za Binadamu ili kuwa na jamii salama.
“Bunge la bajeti linaendelea na ndio Serikali inajadili vipaumbele vya mwaka katika kutekeleza mipango ya maendeleo. Watetezi wa haki za binadamu tumekuwa tukishirikiana na wizara katika masuala ya upatikanaji wa haki za binadamu na kuangalia namna gani tunakomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia,” alisema Maro.