Dar es Salaam. Ubalozi wa Uswisi nchini, kwa kushirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), wamezindua maonyesho ya ‘Dialogues On Humanity’ ya kuadhimisha miaka 75 ya mikataba ya Geneva ya mwaka 1949.
Katika maonyesho hayo pia itaadhimishwa Siku ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu duniani.
‘Dialogues on Humanity’ ni maonyesho yanayozungumzia kuhusu utu wa binadamu na sheria za kivita zinazowataka wanaopigana vita wasiwadhulu raia na maeneo yanayotoa huduma za kijamii ikiwemo hospitali na shule.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya haki za binadamu, wanafunzi wa vyuo vikuu, wawakilishi kutoka asasi za kiraia na jumuiya ya wanadiplomasia.
Tukio hilo pia lilienda sambamba na mjadala wa jopo kuhusu mikataba ya Geneva ya 1949.
Wakati wa mjadala huo washiriki walibadilishana mawazo kuhusu shughuli za msalaba mwekundu sambamba na kusisitiza umuhimu wa mkataba huo katika kulinda haki za raia na watu wasio wapiganaji wakati wa migogoro, pamoja na mustakabali wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Balozi wa Uswisi nchini, Didier Chassot, amesisitiza wajibu wa pamoja wa mataifa yote na wadau katika kuzuia na kukomesha ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
“Hatua madhubuti zitakazochukuliwa katika ngazi ya kitaifa ni pamoja na kuridhiwa kwa itifaki za ziada, kupitishwa kwa sheria zinazotekeleza mikataba ya Geneva katika ngazi ya kitaifa, usambazaji wake ndani ya jeshi na miongoni mwa raia.
“Utekelezaji unaofaa pia unahitaji kuanzishwa kwa tume za kitaifa za utekelezaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuandaa ripoti za hiari za utekelezaji wa sheria hizo,” amesema
Balozi Chassot ameisifu Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kufuata na kuziheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu ndani na nje ya nchi.
Mwanafunzi wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joseph Masangula amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa vijana na uelewa wa mikataba ya Geneva.
“Iwapo vijana wataamua kuchangamkia fursa ya kujifunza na kuzielewa sheria hizi, itakuwa ni sehemu ya ajira ambapo nchi inaweza kuwaajiri kama washauri wa kisheria ili kuhakikisha wanasaidia na kuzingatia mikataba ya Geneva na mwelekeo wa sasa wa duniani,” amesema.