Vitengo vya habari viendeshwe kwa weledi

KLABU za michezo ni taasisi kama taasisi nyingine zenye malengo ya kufikia na wadau wa kutumikia. Zinaweza kuwa taasisi za hiari au za kibiashara kutegemea walivyoamua waendeshaji wake.

Klabu yoyote ya michezo ingependa ikue katika kufikia wadau wake. Ulimwengu wa sasa hauruhusu taasisi kuwasha taa yake na kuifunika.

Mawasiliano yamekuwa ni mahitaji muhimu kwa taasisi yoyote katika karne hii. Klabu, kama zilivyo taasisi nyingine, zinatakiwa kutoa habari kwa umma na kuueleza kinachofanyika ndani ya klabu, matarajio ya muda mfupi na muda mrefu, mafanikio n.k.

Matumizi ya mitandao ya kijamii yamechukua kasi sana katika ulimwengu wa sasa. Watu sehemu mbalimbali duniani hufuatilia kinachoendelea kwenye klabu zao kwa kuingia kwenye tovuti zao lakini zaidi kwenye mitandao ya kijamii hasa kwa kizazi kipya.

Taswira ya klabu itaonekana kupitia kazi za kitengo cha habari. Kitengo cha habari cha klabu kupitia taarifa na machapisho yake ndicho kinaweza kuonyesha taswira ya klabu.

Mathalani mwekezaji au hata mchezaji aliyeko nje ya nchi, atashawishiwa kujiunga na klabu husika kwa taarifa anazozipata kwenye mitandao ya klabu.

Katika mambo yanayonisumbua kuyaelewa katika uendeshaji wa klabu za soka hapa nchini, ni nafasi na majukumu ya ofisa habari wa klabu na msemaji wa klabu.

Inafikia mahali hata kutofautisha yupi ni yupi inakuwa mtihani. Hali inapokuwa hivyo inasikitisha sana kwani umuhimu na nafasi ya habari katika taasisi ni sawa na damu katika mwili wa binadamu.

Bila damu usafirishaji wa mahitaji muhimu katika sehemu mbalimbali za mwili wa binadamu hauwezi kufanyika na binadamu atakufa.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika kuhimiza weledi wa uendeshaji wa klabu (Club licensing) pamoja na mambo mengine lilihimiza klabu kuwa na maofisa habari.

Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wadau wanajua kinachoendelea kwenye klabu kwa manufaa ya kiutawala, kibiashara na kisoka.

Wakati klabu hapa nchini zimeitikia takwa hili labda kwa asilimia kubwa, bado maofisa habari hawajatumika au niseme hawajatumiwa ipasavyo.

Mathalani, hivi karibuni maofisa habari wa klabu za Yanga na Simba wamekuwa na muda mwingi wa kuamka na kuangalia upande wa pili wanafanya au wanasema nini kuliko kuongea na viongozi wa klabu na viongozi wa timu ili wapate nini cha kuwajulisha wadau.

Kwa sababu tambo na vijembe vingi huwa vinahusu timu, basi maofisa habari nao huzama kwenye timu zaidi na hata kufikia kuwafunika benchi la ufundi katika mawasiliano yao kuhusu timu ingawa wengi kama siyo wote, huwa wanapungukiwa na mambo mengi ya kiufundi katika kuendesha timu.

Kwa ofisa habari, ni bora kuwa kimya kuliko kulumbana kulikopitiliza hata kule kwa mashabiki. Ofisa habari ni kioo cha klabu. Hivyo akifanya vibaya na klabu imefanya vibaya.

Viongozi wa klabu pia wanatakiwa kuwapa maofisa habari wigo wa majukumu yao. Nani alikuambia ili uwe ofisa habari mzuri lazima upige vijembe upande wa pili?

Kama vijembe ni muhimu kwa nini klabu zisiajiri wapiga vijembe wa klabu na kuwaacha maofisa habari wakifanya kazi kwa mujibu wa taaluma zao.

Kwani ofisa habari anapokuja kutumika kwenye soka iwe ndiyo amefika mwisho wa weledi kwenye taaluma yake? Ofisa habari anapoadhibiwa kwa kauli mbaya anakuwa ametumwa hivyo na mwajiri wake au wana uhuru kiasi cha kuongea wanachotaka?

Kwa wenzetu walioendelea, tumezoea adhabu za kutoa maneno machafu zinawaendea walimu na mara chache na  manahodha, kwani wao wanaongea baada ya mchezo na wanakuwa hawana muda na utulivu wa kutosha kuandaa maneno ya kusema.

Hawa wanapokosea wanaweza kusamehewa kwa sababu habari si taaluma yao.

Nilibahatika kuajiriwa na Young Africans au Yanga zaidi ya miaka 12 iliyopita. Kuripoti ofisini pale Jangwani nikakuta klabu ikiendeshwa bila hata anuani ya baruapepe na barua zikiandikiwa steshenari.

Ilikuwa kawaida kwa wakati ule kwani hata klabu zenye maofisa habari wa kuajiriwa zilikuwa za kutafuta kwa tochi, yawezekana ilikuwa ni Simba na Yanga tu.

Hatua ya kwanza niliyoiona ya muhimu wakati huo, ilikuwa ni kuimarisha kitengo cha habari na mawasiliano. Tukawachukua vijana wenye taaluma za mawasiliano wakafanya kazi kwa kujitolea na baadhi yao wakaja kuajiriwa kwa mikataba.

Kundi hili la vijana lilitusaidia sana na halikutafuta umaarufu. Walitushauri namna ya kuingia katika ulimwengu mpya wa kidigitali kwa kununua vifaa na teknolojia pepe ikiwemo kufungua tovuti, mitandao ya kijamii, kufunga mtandao wa wifi katika jengo lote na mambo mengine ambayo yaliweka msingi wa kitengo imara cha habari kiichopo sasa.

Ninavyoongea hivi vijana hawa kina Dismas Ten, Baraka Kizuguto na wengine wanafanya kazi nzuri katika utumishi wa soka hapa nchini na kimataifa.

Kuwa ofisa habari inaweza kuwa njia ya kufika mbali katika taasisi ikiwa watu watajikita katika utumishi wa klabu kuliko unazi wa timu.

Ni vizuri maofisa habari wanapoajiriwa wakatumika kujenga uhusiano kati ya klabu na wadau na kueleza mipango na matarajio ya klabu.

Idara ya habari hurahisisha kazi ya idara ya masoko kwa kupeleka nje jina zuri la klabu ambayo ndiyo bidhaa sokoni.

Habari ni kila kitu katika maisha. Kama ilivyo hadithi ya mnara wa Babeli, binadamu asipoweza kufanya mawasiliano yake vizuri hawezi kufanikisha malengo yake vizuri.

Taasisi zinazokwenda kufanikiwa katika nyakati hizi ni taasisi zitakazoweza kuwafikia wadau wengi duniani kwa taarifa nzuri na za kuvutia lakini zaidi za kueleweka.

Klabu za soka, pamoja na kuwa na kazi ya kuburudisha umma, bado zina kazi ya kuupa umma taarifa na elimu na kuwa na weledi wa kutosha kuvutia pia watu na taasisi makini.

Klabu zinapaswa kujitangaza kama chapa za kibiashara na kuelewa chapa hiyo haiuzwi tu nyumbani bali pembe nne za dunia.

Kuweza kufanikisha hili, ni muhimu kufanya uwekezaji katika rasilimali watu na teknolojia katika vitengo vyao vya habari na kuhakikisha nidhamu katika upashaji wa habari.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Related Posts