Wabunge Mbeya wahamasisha uwekezaji kwenye madini, kilimo

Mbeya. Wabunge wa Mkoa wa Mbeya wamewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, kilimo cha mpunga na tumbaku.

Wabunge hao, Masache Kasaka wa Lupa (CCM) na Bahati Ndingo wa Mbarali (CCM), wametoa hamasa hiyo leo Ijumaa Mei 10, 2024 kwenye mkutano wa majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi uliofanyika mkoani humo.

Awali, Kasaka amesema fursa za uwekezaji ni nyingi hususan katika Wilaya ya Chunya na kuhamasisha wafanyabishara kuwekeza ili kuchochea fursa za kiuchumi na ajira kwa vijana.

“Tunawakaribisha Wilaya ya Chunya licha ya shughuli za uchimbaji wa madini, pia kuna fursa ya kilimo cha tumbaku ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika kuchangia pato la Taifa,” amesema.

Kasaka amesema katika kuunga mkono jitihada za Serikali, ni vyema sasa wafanyabiashara, wadau kuchangamkia fursa uwekezaji katika nyanja hizo kwa lengo la kukuza uwekezaji wa ndani.

“Rais Samia Suluhu Hassan anahamasisha sekta ya uwekezaji katika nyanja mbalimbali, na mimi kama mbunge ni sehemu yangu kutoa hamasa ili kuona tunafikia malengo ya Serikali,” amesema.

Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo amesema ni wakati wa wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye mpunga na kuongeza tija.

Mfanyabiashara, Peter Christopher amesema kama wadau wanaunga mkono hoja zilizotolewa na wabunge, lengo ni moja kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya madini na kilimo vinapewa kipaumbele.

“Ili kufikia malengo, ni vyema Serikali kutangaza maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya uwekezaji  wa ndani na nje ili kuvutia uwekezaji na kuchangia na kukuza pato la Taifa na mwananchi mmoja mmoja,” amesema.

Related Posts