Wachimbaji waendelea kuiangukia Serikali mbadala wa zebaki

Butiama. Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa dhahabu wa Buhemba wilayani hapa,  wameiomba Serikali kuwaletea njia mbadala ili kuondokana na matumizi ya zebaki katika uchimbaji wao.

Wachimbaji hao wamesema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikieleza juu ya uwepo wa madhara ya kiafya ya moja kwa moja kwa watumiaji wa zebaki pamoja na mazingira, lakini hadi sasa hakuna njia mbadala ya kuwawezesha kuachana na matumizi ya kemikali hiyo.

Wakizungumza jana Alhamisi Mei 9, 2024 mgodini hapo wakati wa mafunzo juu ya matumizi salama na sahihi ya zebaki, wachimbaji hao wamesema mbali na kuelezwa uwepo wa madhara hayo lakini wanashindwa kuachana na kazi hiyo.

“Tunalazimika kutumia zebaki kukamatia dhahabu wakati wa uzalishaji hasa wakati wa kuosha na kuchoma kwa sababu hakuna njia nyingine.

“Kinachosikitisha hata Serikali inajua kuwa zebaki ina madhara makubwa lakini hadi sasa hatupewi suluhisho,” amesema Wambura Mseti.

Kwa upande wake Mwajuma Kebacha amesema wanawake ni waathirika wakubwa kwa sababu ndio wanaoosha mchanga kwa kutumia zebaki tena kwa mikono mitupu

“Mfano mimi nimefanya kazi hii kwa zaidi ya miaka 30 sijui nimeathirika kwa kiasi gani Mungu ndiye anayejua, ukumbuke kuwa hii  ndio njia yetu pekee ya kujipatia kipato,” ameongeza.

Naye Samson Wambura amesema anashangazwa na ukimya wa Serikali kuhusu suala hilo ilhali sekta yao ni miongoni mwa zinazolipa kodi kubwa serikalini, hivyo wanapaswa kupatiwa huduma bora kwa ajili ya uendelevu wa sekta hiyo.

“Tunalipa tozo zote kwa mujibu wa sheria, sasa kwa nini Serikali inashindwa kutuhudumia, kwa nini tunaadhirika bila hatua kuchukuliwa, tunaambiwa waathirika wakubwa ni wale wanaokutana na zebaki moja kwa moja, tunaomba Serikali ije na njia mbadala ili kutunusuru,” amesema Wambura.

Akizungumzia malalamiko hayo, Meneja wa  Usajili wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Musa Kuzumila amesema Serikali inafanya utafiti ili kuja na teknolojia rafiki na rahisi itakayoweza kutumiwa na wachimbaji wote.

“Yapo makubaliano ya kimataifa kuhusu matumizi ya zebaki ambapo mwisho wake ni mwaka 2032, hivyo Serikali inafanya kila iwezavyo kuhakikisha teknolojia rafiki inapatikana ili wachimbaji hawa waweze kufanya shughuli zao kwa usalama na kuzingatia uhifadhi wa mazingira,” amesema.

Amesema mbali na kufanya utafiti juu ya teknolojia rafiki lakini pia Serikali imeandaa mradi maalumu wa kudhibiti matumizi ya zabeki kwa wachimbaji wadogo nchini, ambapo katika mradi huo  watapewa elimu juu ya matumizi salama na sahihi ya zebaki ili wasidhurike wala kuharibu mazingira.

“Mradi huu unaratibiwa na Baraza la Taifa la  Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na kutekelezwa na washirika mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali lengo la mradi ni kuhakikisha kunakuwepo na matumizi sahihi na salama ya zebaki,” amesema.

Related Posts