Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema nishati safi ya kupikia inajumuisha
mbinu zote zinazomuwezesha mtu kuandaa chakula bila kuathiri misitu.
Amesema hayo wakati akishiriki mjadala wa Nishati Safi
ya Kupikia kwenye kipindi cha Mizani kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha
TBC1 tarehe 08 Mei, 2024 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali katika kuhimiza
nishati safi unalenga si tu la kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na
mkaa bali pia kuhamasisha ubunifu wa nishati mbadala.
Amesema lengo namba saba la nishati safi ya kupikia ni
lengo endelevu la dunia na linajibu malengo mbalimbali yaani ugunduzi na tafiti
kwa watu mbalimbali kugundua unafuu wa nishati.
Halikadhalika, Dkt. Jafo ameeleza kuwa ubunifu
unaozungumziwa ni namna mtu anavyoweza kutumia nishati za aina mbalimbali
zikiwemo majiko ya gesi, majiko ya umeme, majiko, majiko ya nishati jadidifu na
mbinu nyingine zozote zitakazomfanya mtu apike chakula.
“Malengo ya Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi
na kuangalia namna gani wanavyoweza kuja na ubunifu hasa katika kumpa unafuu
mwananchi wa kawaida kwa mfano anaweza kuwa na elfu mbili halafu akajaziwa
gesi,” amesema.
Ameongeza kuwa juhudi za Serikali zimewezesha kampuni
nyingi kuwekekeza katika gesi na wananchi kufungiwa majumbani kwao, hivyo
kuleta fursa katika nishati safi ya kupikia.
Pia, baadhi ya kampuni zimewezesha shule kadhaa kuwa
na mifumo ya gesi ambapo wanatumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia wanafunzi
hivyo kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha watu Zaidi ya
mia moja kuacha kutumia kuni na mkaa.