N’Djamena/AFP. Idadi kubwa ya wanajeshi na maofisa wa polisi wanashika doria kwenye mitaa ya mji mkuu wa Chad, N’Djamena, baada ya kiongozi wa kijeshi Mahamat Déby kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais kwa zaidi ya asilimia 61.
Waandishi wa habari wa AFP walisema idadi ya wanajeshi mitaani Ijumaa ilionekana kuwa kubwa zaidi kuliko baada ya chaguzi zilizopita.
Hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa Alhamisi usiku, walinzi wa Rais walikuwa wameegesha magari mengi ya kivita kwenye makutano ya njia kuu.
Succes Masra, mgombea wa upinzani ambaye pia ni waziri mkuu wa Déby, alitangaza Alhamisi usiku kwamba ameshinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi.
Masra alisema ushindi umenyakuliwa “kutoka kwa watu” na kutoa wito kwa wafuasi wake “kupinga hilo kwa utulivu”.
Jenerali Déby (40) alitawazwa kama kiongozi wa Chad na jeshi baada ya baba yake, Idriss Déby Itno, kuuawa wakati wa vita na vikosi vya waasi Aprili 2021.
Ushindi wake unamaanisha kuwa utawala wa miaka 34 wa familia ya Déby, bado utaendelea.
Masra aonya mapema
Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu Januari mwaka huu, alikuwa ameonya kwamba timu ya Deby ingechakachua matokeo ili kuhakikisha anashinda.
Masra aliwataka wananchi wa Chad “kujikusanya kwa amani lakini kwa uthabiti ili kuthibitisha ushindi wao.
Tume ya Uchaguzi imesema Masra imepata asilimia 18.53 pekee ya kura.
Utawala ulikuwa umewanyamazisha watu wa upinzani kwa muda mrefu na mpinzani mkuu wa Deby aliuawa Februari 2024.
Hakuna ulinzi ulioimarishwa karibu na makao makuu ya chama cha Transfoma cha Masra, kusini mwa mji mkuu siku ya Ijumaa.
Lakini wanachama waliokuwa na silaha nzito za walinzi wa Rais waliovalia bereti zao nyekundu walikuwa nje kwenye barabara kuu pamoja na idadi kubwa ya magari ya kivita, waandishi wa habari wa AFP waliripoti.
Polisi wa kupambana na ghasia waliovalia sare nyeusi wakiwa wamefunika nyuso zao pia walikuwa mitaani.