Hatima ya Zuma kuwania urais Afrika Kusini yasubiri Mahakama

Afrika Kusini/ AFP. Mahakama ya Juu nchini Afrika Kusini imeanza kusikiliza rufaa kuhusu iwapo Rais wa zamani, Jacob Zuma atastahili kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Zuma (82) anaongoza chama kipya cha upinzani, Umkhonto we Sizwe (MK), ambacho wachambuzi wanasema kinaweza kuwa na athari kubwa kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu wa Mei 29, mwaka huu na pia wasiwasi wa kiusalama endapo atazuiwa.

Aprili mwaka huu Mahakama ilisema kiongozi huyo wa zamani alikuwa huru kugombea, baada ya Tume ya Huru Uchaguzi kumzuia, ikisema Katiba inakataza mtu kushikilia ofisi ya umma ikiwa atapatikana na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya mwaka mmoja jela.

Mawakili wake waliipinga hoja hiyo wakisema kifungo cha Zuma kilitokana na shauri lililoendeshwa kwa msingi wa kesi ya madai na siyo jinai.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini ilikata rufaa kwenye Mahakama ya Juu ya nchi hiyo dhidi ya uamuzi wa mahakama ya chini, uliompatia ruhusa Zuma kushiriki uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.

Zuma ambaye alilazimika kujiuzulu urais mwaka 2018 na kufungwa jela mwaka 2021, ametofautiana na chama tawala cha African National Congress ANC na amekuwa akikipigia kampeni chama chake kipya cha MK.

Utafiti wa kura za maoni unaashiria kuwa ANC itapoteza uungwaji mkono mkubwa baada ya kuwa madarakani kwa miaka 30 ikiwa Zuma atashiriki uchaguzi.

Chama cha MK kinatoa kitisho kwa ANC haswa katika jimbo la nyumbani kwa Zuma la KwaZulu Natal.

Related Posts