Mabanda kutumika kuhamasisha kujifunza sayansi na hisabati

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na mkazo wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), wadau wa elimu wamebuni mpango wa kujifunza kuanzia ngazi za chini kwa kuanzisha mradi wa ‘Banda Jami’.

Mradi huo unalenga watoto wenye umri wa kuanzia miaka 9-13 hadi, wenye lengo la kukuza uelewa wa kina wa masomo ya STEM, licha ya kuwepo watoto chini ya miaka hiyo ambao wanajifunza masomo ya mengine.

Serikali ilizindua mipango ya uhamasishaji inayolenga kuwashawishi  wanafunzi katika masomo ya STEM, kwa kutambua umuhimu wake katika Taifa.

Hilo limeweza kuchochea ufadhili wa masomo, kama vile Samia Scholarship, ambao hutolewa kwa wanafunzi wa kipekee wa sayansi kama sehemu ya kuonyesha juhudi ya kuthamini masomo hayo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 11, 2024, Mkurugenzi wa Mradi, Mbaki Mutahaba amesema wamejikita katika kutoa elimu hiyo kwa kutumia maudhui kutoka vipindi vya runinga vya Ubongo Kids ili kuwawezesha watoto kuelewa teknolojia na umuhimu wa takwimu.

“Mradi huu unaitwa ‘Banda Jamii’ na umeundwa ili kutoa programu mbalimbali za elimu kwa jamii kupitia kumbi za burudani, hasa zile zinazopendelewa na wenyeji pia kufahamu umuhimu wa kuanzisha elimu ya STEM mapema, hasa kwa watoto wenye umri wa miaka 9-13,” amesema Mbaki.

Amesema kwa sasa wameamua kutumia taasisi ya Rotary Sunset Club kwa kuwezesha wasilisho la maudhui yanayojulikana kwa jina la ‘Ubongo Kids’ kwa watoto wa kata ya Keko, mtaa wa Magurumbasi B, ambayo yanarushwa ndani ya ‘kibandaumiza’ kwa kukusanya watoto ili kujifunza.

Kufanya hivyo amesema itasaidia katika kukuza ari ya somo la hisabati na kuondoa wasiwasi wowote unaohusiana na somo hilo.

kwa upande mwingine mwalimu mshiriki wa mradi huo Christopher Maganga amesema kuna haja wa ushirikishwaji wa wazazi katika kuelewa umuhimu wa elimu ya STEM na kuhimiza watoto kuchangamkia masomo hayo bila woga.

“Katika jamii yetu, wazazi wengi hawana ujuzi na masomo ya STEM; kwa hiyo, kuanza kutoa elimu kwa watoto hao ndio mzizi wa kuwatia moyo katika masomo haya wakiwa bado wadogo.

chukua hisabati, kwa mfano; wanapoona wenzao wakitatua matatizo kwenye video, mara moja wanapata ujuzi pale pale,” amesema Maganga.

Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Taifa, Patrick Komba, ameonyesha kufurahishwa na mpango huo, akibainisha kuwa mchango wake katika kutoa stadi muhimu za maisha.

“Katika mradi huu, nimejifunza jinsi ya kujiwekea akiba nikiwa mwanafunzi hasa nikiwa sina cha kutegemea. ningependa kuwahimiza wanafunzi wenzangu waje kwenye jumba la jamii kujifunza pamoja na watoto wengine,” amesema Komba.

Mzazi mmojawapo, Blanke Munish, alipongeza mpango huo kwa kuweka mazingira salama na mazuri kwa watoto kujifunza, kuwaepusha na sintofahamu za mitaani.

“Nimefurahi kwa sababu mara nyingi, baada ya watoto kunywa chai ya asubuhi siku za Jumamosi, huwa tunawaacha waende matembezini. Sasa, badala ya kwenda nje, wanakuja hapa kujifunza pia kama inawezekana kuja mara mbili kwa wiki na wakati wa likizo, ili waepuke shughuli za mitaani,” amesema Blanke.

Makamu Mwenyekiti mtaa wa Keko Magurumbasi “B”, Abdalah Kilonga amesema mradi huo una dhamira wa kuweka vipaumbele vya ulinzi na usalama wa watoto, akionyesha thamani ya kuwapatia fursa za elimu ya STEM kamili na bila malipo.

“Tabia za mitaani siku hizi zinahusisha mambo ya ajabu, lakini kuwa hapa kunamaanisha wako salama zaidi. Watapata elimu ya kutosha ya STEM bure ili kujenga uelewa wa kutosha,” alieleza.

Related Posts