Jeshi la nchi hiyo limesema vikosi vyake vinaendelea kuwalenga wanamgambo wa Hamas kwenye maeneo tofauti mashariki mwa mji huo.
Limesema wanamgambo kadhaa wa kundi hilo wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Lakini taarifa ya jeshi hilo haikutoa idadi kamili ya wapiganaji wa Hamas iliyowaua.
Israel imetangaza vilivile bado inadhibiti kwa kiasi fulani eneo la mpaka kati ya Gaza na Misri ulipo mji wa Rafah.
Mpaka huo umekuwa muhimu sana katika kupitisha misaada ya kiutu kuingia Gaza tangu kuanza kwa vita miezi saba iliyopita.
Tangazo hilo la Israel linadhihirisha serikali mjini Tel Aviv imedhamiria kutanua operesheni yake ya ardhini kwenye mji wa Rafah licha ya miito ya kimataifa ya kuitaka isitishe mpango huo.
Tel Aviv yashikilia msimamo wake licha ya shinikizo la kimataifa
Israel imeshikilia msimamo wake ikisema dhima ya operesheni hiyo ni kulitokomeza kabisa kundi na Hamas na kuzifunga njia zinazotumika kuingiza silaha kwa ajili ya kundi hilo kutokea upande wa Misri.
Katika siku za karibuni shinikizo la kupingwa kwa operesheni hiyo limeongezeka ikiwemo kutoka kwa mshirika wa jadi wa Israel, Marekani ambayo imekwenda umbali wa hata kutishia kuacha kuipatia Israel silaha iwapo itafanya hujuma nzito kwenye mji wa Rafah.
Marekani, mataifa kadhaa ya magharibi na Umoja wa Mataifa kwa pamoja wana wasiwasi operesheni kwenye mji huo uliofurika watu itakuwa na taathira kubwa kibinadamu na kuzidisha mzozo wa hali ya kiutu ambayo tayari imezorota sana kwenye Ukanda wa Gaza.
Wakaazi zaidi wa Rafah waamriwa kuondoka kupisha operesheni ya kijeshi
Siku ya Jumamosi, Israel ilitoa ilani ya kuwataka watu zaidi wa mji wa Rafah waondoke kwenda mahali iliposema ni salama.
Mji wa Rafah unakadiriwa kuwahifadhi kiasi Wapalestina milioni 1.3 waliokimbia vita maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.
Hadi sasa zaidi ya watu 150,000 wamelazimika kuuhama baada Israel kuamuru wafanye hivyo kabla ya kuchacha kwa operesheni yake ya kijeshi.
Katika hatua nyingine jeshi la Israel limesema makombora kadhaa yamefyetuliwa kutokea mji wa Rafah yakikilenga kituo cha mpakani cha Kerem Shalom.
Kituo hicho kililazimika kufungwa kwa muda mapema wiki hii baada ya mashambulizi kama hayo ya makombora.
“Maroketi manne yamebainika yamerushwa kutokea Rafah,” imesema taarifa ya jeshi la Israel, na kuongeza kwamba roketi moja liliangushwa na mifumo ya ulinzi ya Israel na mengine yalidondoka kwenye maeneo yasiyo na watu.
Hamas yatoa mkanda wa video wa moja ya mateka wa Israel
Wakati hayo yakijiri kikosi cha wapiganaji cha kundi la Hamas cha Al-Qassam Brigades, siku ya Jumamosi kimetoa mkanda wa video unaomwonesha moja ya mateka wa Israel inaowashikilia kwenye Ukanda wa Gaza.
Mkanda huo umemwonesha mwanaume huyo akiwa hai na ametambuliwa kuwa ni Nadav Popplewell.
Ameonekana akizungumza kwenye mkanda huo wa sekunde 11 pekee uliambatana na maneno ya lugha ya Kiarabu na Kiebrania yanayosomeka: “Muda unayoyoma, serikali yenu inawadanganya”.
Kwenye video hiyo mateka huyo, ambaye pia ni raia wa Uingereza, anaonekana kuwa na jicho lililovia damu na anazungumza akiwa chini ya shinikizo.
Hata hivyo hana dalili zozote nyingine za majeraha.
Popplewell alitekwa nyara akiwa nyumbani kwake mnamo Oktoba 7 mwaka jana wakati Hamas ilipofanya shambulizi kubwa ndani ya ardhi ya Israel.
Mama yake, Hanna Peri, naye alitekwa lakini aliachiwa huru wakati wa makubaliano ya kusitisha vita yaliyodumu kwa wiki moja mwezi Novemba.
Inakadiriwa Hamas bado inawashikilia zaidi ya mateka 100 wa Israel na mataifa mengine iliyowachukua wakati wa uvamizi wao.