POWER IRANDA: Hizi ndizo siri za kiduku katika ngumi

UNAPOLITAJA jina la Twaha Kiduku, basi huwezi kuacha kumtaja kocha wake, Chanzi Mbwana Chanzi maarufu kama Power Iranda kwa kuwa ndiye aliye nyuma ya mafanikio ya mbabe huyo wa masumbwi nchini.

Power Iranda amekuwa taswira ya Kiduku anapokuwa nje ya ulingo na ndiye anayehakikisha bondia huyo anapigana masumbwi na kupata mafanikio katika mchezo huo ambao umegeuka kuwa ajira katika siku za karibuni.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na kocha huyo ambaye anaeleza mambo mengi tangu alipoanza kumnoa Kiduku, changamoto anazopitia na mengine mengi, lakini pia kuna mambo ambayo bondia huyo huyafanya na kumkera mkufunzi wake.

RATIBA YA KIDUKU
Power Iranda anaeleza kwamba Kiduku ana mazoezi mara moja tu kwa sababu pale wasipokuwa na pambano na huo ndiyo utaratibu waliojiwekea ili kujiimarisha zaidi katika mchezo huo.

“Kama hatuna mechi huwa anafanya mazoezi kwa siku mara moja tu, lakini kama tunajiandaa kwa ajili ya mechi asubuhi lazima akimbie barabarani mapema kabisa. Akitoka hapo ataingia gym kidogo na jioni tena atakuja gym kwa ajili ya kuhakikisha anauandaa mwili wake kuwa fiti wakati wote,” anasema.

“Kama kawaida anapomaliza mazoezi huwa nampangia muda wa kupumzika kulingana na mazoezi anayofanya maana ndio kazi yake. Mchana atapata chakula na jioni atarudi tena mazoezini, hivyo muda wa kupumzika nautoa kutokana na namna anavyofanya mazoezi na nimsifu Kiduku ana nidhamu ya hali ya juu sana maana anawahi kufika nyumbani na anapumzika kwa wakati.”

Anaongeza kwamba: “Bondia wangu naweza kujivunia kwamba hapendi starehe hata kidogo maana hanywi pombe, havuti sigara wala bangi na nashukuru kwamba anaelewa kwamba mchezo wa ngumi ni kazi yake hivyo huwa hajihusishi na mambo hayo kabisa.”

MSOSI NA SIKU YA PAMBANO
Kocha huyo anazungumzia pia suala la chakula anachokula bondia huyo, lakini anagusia pia ugumu katika kumpangia mlo kulingana na mazingira wanayoishi.

“Kulingana na namna tunavyoishi hatujafika kwenye levo ya kumpangia bondia wetu ale chakula gani, hiyo inatokana na kwamba Twaha anaishi kwake na mimi naishi kwangu. Kama tungekuwa tunakaa kambini ningeweza kumsimamia, lakini kwa sasa hilo haliwezekani maana Twaha anapenda sana kula chips mayai na wakati mwingine wali maharage. Sasa ukimpangia wakati hamkai wote programu haiwezi kufuatwa,” anasema.

Akizungumzia siku ya pambano inavyokuwa, Iranda anasema: “Kwanza mchezo huwa unaanza pale mnapopita uzito akimaliza kupima huwa anapumzika siku nzima mwenyewe akitafakari na kuweka sawa vifaa vyake kwa ajili ya kupambana na siku ya pambano huwa timu nzima tunakuwa naye tangu asubuhi kumjenga kisaikolojia, maana bondia anatakiwa awe na kocha wake ili ajengwe kisaikolojia ili acheze na kushinda basi.

PAMBALO ASILOLISAHAU
Power Iranda anasema tangu aanze kumnoa Kiduku kuna mapambano mawili ambayo yamewahi kumfanya amuonee huruma bondia wake la kwanza likiwa ni lile alilopigana jijini Mwanza na jingine alilopigwa Dar es Salaam.

“Sitasahau siku ambayo tulipoteza pambano tukiwa Mwanza tukipigana na bondia Asemahle Wallem raundi ya tatu tu lililopigwa Julai 29, 2023. Nakumbuka tulifanya maandalizi makubwa, lakini tukapoteza lile pambano. Ule ulikuwa ubingwa mkubwa na tulitakiwa kuushinda lakini tukapoteza. Pale nilijiskia vibaya sana na sikulala usingizi mpaka tunarudi Morogoro,” anasema.

“Pambano jingine ni pale tulipocheza na Med Sebyala wa Uganda katika kuwania mkanda wa PST Desemba 27, 2023 pale niliumia kwamba tumeshinda, lakini bondia Twaha alicheza chini ya kiwango ndiyo maana katika pambano na Aprili 11 Twaha alipopigana na Harpreet Singh wa India tulijipanga na bondia kupigana na kumaliza pambano kabla ya raundi zote kuisha.

“Mabondia wa Kihindi ni wazuri sana maana wale wanapenda sana kula chakula asilia na wanazingatia kile wanachoambiwa. Nilimfuatilia Harpreet Singh alikuwa vizuri maana alishakwenda kupigana mpaka Urusi na am

eshashinda kwa TKO mara sita, hivyo hakuwa kizembe.”
Kocha huyo anazungumzia maeneo ambayo Kiduku alipata wakati mgumu kabla ya kubadilika na sasa yupo fiti.

“Twaha yuko fiti kwa asilimia mia moja, lakini changamoto iliyokuwepo ni kwamba alikuwa akikosa unyumbulifu, utimamu wa miguu, uharaka wa ngumi pamoja na kucheza kwa kuulinda mwili wake usiguswe na mpinzani na kweli tulivyoyajaribu haya yote kuna mabadiliko tuliyaona na naamini ataendelea kufanya vizuri maana anatambua kwamba hii ni kazi yake,” anasema.

KIDUKU KUTAFUTA KOCHA
Iranda pia anazungumzia namna alivyojisikia baada ya kusikia Kiduku anatafuta kocha mpya atakayerithi mikoba yake.
“Ni kweli nimesikia maneno mengi kwamba Twaha atafute kocha mwingine mimi sifai. Niliposikia niliwajibu kwa kitu kimoja kwamba mti wenye matunda hauishi kupigwa mawe,” anasema.

“Tangu niaze kuwa kocha wake tumetwaa mataji tisa, leo ndio nionekane sifai? na tulipompiga Dulla Mbabe tukachukua gari aina ya Crown kila mtu alinisifia leo naonekana sio kitu tena? Nilimwambia Twaha azibe masikio na akafanya hivyo mpaka sasa tunaendelea vizuri.

“Yale ni maamuzi yake na timu kwa ujumla, na bondia ‘profesheno’ mara nyingi huwa hana mwalimu mmoja ana uamuzi wa kuwa na kocha zaidi ya mmoja, na kwa mabondia ambao walibadilisha makocha katika kipindi cha neema mara nyingi huwa hawafiki mbali, na nashukuru mimi na Kiduku hatuna shida na kazi zinaenda kama kawaida.”

Iranda anasema mara nyingi anapokuwa na bondia huwa hafikirii sana suala la maslahi, badala yake hutaka afikie malengo kwanza maana kwenye ubondia kuna maisha baada ya ngumi
“Na mimi utaratibu wangu ni kwamba bondia anayepita kwangu nataka maisha yake yawe mazuri,” anasema na hiki ndicho anachojivunia pia Kiduku.

“Ninajivunia mambo mengi. La kwanza nimekuwa maarufu kupitia Kiduku. Nimejenga urafiki na watu katika maeneo mengi kupitia ndondi na Kiduku, hivyo naishi maisha ya kawaida sana pamoja na umaarufu nilionao.”

AMGOMEA KIDUKU, HATAKI AMBURUZE
Power Iranda anasema katika maisha yake ya ukocha wa ngumi siku zote huwa haruhusu kupangiwa nini cha kufanya na bondia anayemfundisha.

“Mimi huwa siruhusu mtu nayemfundisha awe staa kwangu, maana sina adabu pale unaponikosea heshima, hivyo kwa Kiduku sijawahi kukubali aniendeshe kwa kuwa yeye ni staa. Huo ustaa wake akaufanye kwa mabondia wenzake ila sio kwangu,” anasema. “Mimi ndio staa kwake na ninamuarisha kile ninachotaka na anafuata na bondia ambaye atajaribu nitamfukuza mara moja. Lakini kwa Kiduku bado sijakutana na changamoto hiyo.”

Iranda anasema kitendo cha Kiduku kumpiga Singh kibarua chake kimekuwa salama maana aliongelewa mengi na kama bondia wake angepigwa angekuwa katika wakati mgumu.

“Kabla ya lile pambano nilisimangwa sana. Kiukweli niliumia maana walianza kunisema kwamba sio kocha badala yake eti ni mbeba vyuma. Hata katika lile pambano tulikuja kitofauti na tuliposhinda sikuona mtu akinyanyua tena mdomo, hivyo ajira yangu iko salama na tunajiandaa na pambano huko mwezi Septemba.”

Wakati wa mahojiano haya Power Iranda aliyetokea kwenye mieleka na kuja kuwa kocha mkubwa wa ngumi hapa nchini, anasema bondia Hassan Mwakinyo hamjui na hamhusu.

“Kwa sasa huyo bondia sio mtu wangu. Atakapokuwa kwenye himaya yangu nitaweza kumzungumzia, lakini kwa sasa kama unataka azungumziwe mtafute meneja wake,” anasema.

KIDUKU KUPUMZIKA WIKI
Kama hujui iwapo Kiduku anakuwa pambano kubwa na kali, kocha huyu huwa anampa mapumziko marefu ili kurejesha ubora, kupona vizuri majeraha na pia kutafakari mwelekeo wa mchezo huo ipasavyo.

“Twaha baada ya pambano alilotumia nguvu nyingi kama la yule Mhindi, huwa nampa wiki nzima ya kupumzika ili aweze kurudisha nguvu alizotumia na ninamwambia atumie muda mwingi kunywa maji mengi, juisi ili aweze kurejesha nguvu aliyotumia kwenye kupigana kisha baada ya hapo ndio tunaanza tena mazoezi,” anasema.

Pamoja na hayo, lakini suala la Kiduku kula chipsi mayai bado ni ishu na kocha huyo anasema amejaribu mara kadhaa kuhakikisha kwamba anamshawishi aache au apunguze, lakini imekuwa ngumu kuacha.

“Kama kocha wake nimeshawahi kujaribu kumkataza kula chipsi mayai, lakini ile ni hulka yake. Nimeshindwa kumkataza maana ndicho chakula anapenda na anasema akila ugali huwa anaota usiku, sasa ukishasikia mambo hayo inakuwa changamoto nimeamua nimuache ale anachopenda,” anasema Power Iranda

HUYU NDIYE IRANDA
Power Iranda katika historia yake hajawahi kucheza ngumi, na wala hajawahi kupanda kwenye ulingo, bali alikuwa mcheza mieleka maarufu hapa nchini miaka ya 1980 na mchezo wake mkubwa ilikua ni kuvuta magari makubwa, kufanya mazoezi ya nguvu jambo lililomfanya awe mmoja wa wanamichezo maarufu.

Kutokana na umahiri huo, alifanikiwa kufanya mambo mengi akisafiri huku na kule na maonyesho yake mara nyingi yalijaza watu katika kumbi na hata viwanja alivyotumia.

Hata hivyo, baada ya kustaafu mchezo wakati akiishi Dar es Salaam, aliamua kuhamia mjini Morogoro anakoendesha maisha yake, huku akifundisha ngumi.

“Baada ya kuja Morogoro nilikutana na aliyekuwa kocha wa Francis Cheka, Saleh Kilamba akaniangalia akaniambia kwamba ninafaa kucheza ngumu kutokana na mwili wangu ulivyokuwa, lakini kwa kuwa umri ulishanitupa mkono ikabidi nikae naye niwe kocha msaidizi wa Cheka yeye akiwa kocha mkuu na nilikuwa na kipaji. Aliponiongezea vitu ndio nikawa kocha hadi leo,” anasema.

Related Posts